
Musoma. Makao makuu ya Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria ( LVBC) chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yamezinduliwa hatua ambayo imeelezwa kuwa pamoja na mambo mengine itaimarisha zaidi utafiti, uratibu na ubunifu kuhusu masuala ya kimazingira, kijamii na kiuchumi yanayoathiri Bonde la Ziwa Victoria.
Ofisi hizo za LVBC imejengwa Jijini Kisumu nchini Kenya kwa gharama ya zaidi ya Sh13 bilioni fedha ambazo zimetokana na michango kutoka Serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Rais William Ruto Novemba 29,2025 wakati wa uzinduzi wa ofisi hizo, Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Maeneo Kame na Maendeleo ya Kikanda, Beatrice Askul amesema maendeleo hayo yanaonyesha nia ya pamoja ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya kulinda ikolojia ya ziwa hilo.
Amesema ulinzi wa ikolojia unafanyika kupitia uratibu wa sera zinazotegemea sayansi, juhudi za pamoja za kupambana na uchafuzi wa mazingira, usimamizi wa uvuvi wa mipakani, kuimarisha mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kulinda mazingira ya Bonde la Ziwa Victoria.
“Makao haya ya kisasa yatatumika kama kituo cha umahiri katika utunzaji wa mazingira, utafiti, ubunifu na uongozi wa sera katika eneo la Bonde,” amesema Askul
Askul amesema Serikali ya Kenya imedhamiria kuendeleza ushirikiano ndani ya jumuiya kwa kushughulikia changamoto za miundombinu duni katika bonde hilo kupitia mpango kabambe wa uboreshaji wa miundombinu kama vile upanuzi wa reli, ujenzi wa barabara za mipakani na vituo vya uratibu wa masuala ya usalama wa usafiri majini.
“Kenya imejitolea kikamilifu kushirikiana na nchi wanachama wengine kujenga ukanda wenye nguvu, ulioungana na wenye ustawi zaidi, ili kutimiza ajenda hii, Kenya inaongoza miradi mikubwa ya miundombinu ikijumuisha upanuzi wa reli ya kisasa,” amesema.
Awali Katibu Mtendaji wa LVBC, Dk Masinde Bwire, alisisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi za kulinda mazingira ya Ziwa Victoria, huku akisema ofisi hizo zitakuwa kitovu cha kutafuta suluhu za changamoto za kimazingira na kijamii na kiuchumi zinazoikumba eneo hilo.
Dk Bwire amesema ujenzi wa jengo hilo la kisasa ulianza rasmi mwaka 2020 na kwamba mradi huo umegharimiwa kikamilifu na nchi zote wanachama wa jumuiya kwa mgawanyo sawa.
Dk Bwire amesema moja ya majukumu ya kamisheni yake ni kuhakikisha kunakuwepo na matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo ndani ya bonde la Ziwa Victoria rasilimali hizo ni pamoja na bonde la mto Mara.
Aliongeza kuwa makao hayo makuu yanakuwa kituo cha kwanza cha jumuiya nchini Kenya.
Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Veronica Nduva, alisema bonde la Ziwa Victoria linakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinahitaji ushirikiano wa pamoja ili kuzitatua.
Alisema uwepo wa makao makuu ya Kamisheni hiyo ni moja ya mikakati iliyowekwa ili kupambana na changamoto hizo kwani watendaji wa kamisheni hiyo watakuwa na sehemu sahihi na rafiki kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao.