
Mbeya. Hali imeendelea kuwa tete kwa Mbeya City baada ya kupoteza mchezo wa tatu mfululizo katika Ligi Kuu, huku mashabiki wakionekana kumkatia tamaa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Malale Hamsini wakimtaka aondoke.
City iliyowahi kushuka daraja na kukosa Ligi Kuu misimu miwili, imerejea msimu huu, ambapo ilikuwa na mwanzo mzuri ikiwamo matokeo ya suluhu ya bila kufungana dhidi ya Yanga na sasa hali imeonekana kubadilika.
Katika mechi tatu mfululizo, imepoteza mbili ugenini dhidi ya Mashujaa bao 1-0 kisha kulala 2-0 mbele ya Coastal Union na leo ikiwa uwanja wake wa Sokoine imelimwa bao 1-0 na Namungo na kujikuta ikiingia lawama na mashabiki wake.
Baada ya mchezo huo mashabiki wa Mbeya City walijikusanya nje ya uzio na kuanza kumuimba kocha Malale aondoke hawamtaki wakidai kutoridhishwa na mwenendo wa matokeo kwa timu yao.
Katika mchezo huo ambao umepigwa saa 8 mchana, Namungo ilicheza vizuri ukilinganisha na wenyeji wa mechi hiyo na kufanikiwa kuondoka na pointi tatu zilizowapaisha nafasi ya nne kwa pointi 12 baada ya mechi nane huku City ikishuka nafasi ya 10 kwa pointi nane na mechi tisa.
Mchezaji Fabrice Ngoy ndiye alikuwa na mchezo bora kwa bao lake kuamua dakika 90 na kuihakikishia Namungo ushindi huo wa ugenini na kutangazwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Namungo chini ya Kocha wake Juma Mgunda inafikisha mechi tatu mfululizo bila kupoteza ikiwa ni ushindi michezo miwili dhidi ya Dodoma Jiji 2-0 na 1-0 dhidi ya Mbeya Citya na sare ya 1-1 mbele ya Azam FC.