Yanga imemaliza mechi mbili za kwanza za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa kundi B ikiwa na pointi nne ilizokusanya katika mechi mbili dhidi ya FAR Rabat na JS Kabylie.

Katika mechi hizo zote mbili, Yanga haijaruhusu nyavu zake kutikiswa na ni timu mbili tu ambazo hadi sasa hazijafungwa bao katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambazo ni Yanga na Pyramids FC tu ya Misri.

Wakati mashabiki wa Yanga wakitambia makali yao kwenye mechi mbili zilizopita za Ligi ya Mabingwa, takwimu zinaonyesha nyota wawili wa kikosi chao ndio wamekuwa na mchango mkubwa zaidi katika kuifanya timu hiyo isipoteze mchezo na kutoruhusu bao hadi sasa katika makundi.

Wachezaji hao ni Kipa Djigui Diarra na Beki Ibrahim Abdullah ‘Bacca’.

Diarra anaongoza katika chati ya makipa wamecheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao ambapo amefanya hivyo mara mbili.

Kipa huyo pia ana wastani wa asilimia mia moja wa kuokoa hatari na anashika nafasi ya tatu kwa kuokoa hatari katika dakika 90 ambapo anaokoa wastani wa mashambulizi 3.5 kwa mchezo.

Beki Ibrahim Bacca ndiye kinara wa kuondosha hatari ndani ya kikosi cha Yanga ambapo katika mechi mbili zilizochezwa, amefanya hivyo mara 19 sawa na wastani wa mara 9.5 kwa mchezo.

Kutoruhusu bao katika mechi mbili za mwanzo za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kumeifanya Yanga imalize nuksi ya muda mrefu ya kufungwa mabao katika mechi mbili za mwanzo za hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika.

Kabla ya hapo, hakuna msimu ambao Yanga ilicheza hatua hiyo iwe katika Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho Afrika bila nyavu zake kutikiswa.

Mwaka 1998, Yanga ilifungwa idadi ya mabao matatu katika mechi zake mbili za mwanzo za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mwaka 2016 katika Kombe la Shirikisho Afrika, ilifungwa mabao mawili katika mechi zake mbili za mwanzo ambapo ilifungwa bao 1-0 katika kila mchezo.

Katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2018, Yanga ilifungwa mabao manne katika mechi mbili za mwanzo za kundi D.

Msimu wa 2022/2023 ilifungwa mabao matatu katika mechi mbili za mwanzo za Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika.

Msimu wa 2023/2024, Yanga ilikubali nyavu zake zitikiswe mara nne katika mechi mbili za kwanza za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Na msimu uliopita katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ilifungwa mabao manne katika mechi mbili za mwanzo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *