
Mkuu wa Baraza Kuu la Mpito la Sudan, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan, amesema kuwa serikali yake iko tayari kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono juhudi za kibinadamu, maendeleo na jitihada za kijamii za nchi hiyo.
Al-Burhan ndiye Kamanda wa Jeshi la Sudan SAF na ametoa matamshi hayo mbele ya waandishi wa habari huko Port Sudan akiwa pamoja na Ramtane Lamamra, Mjumbe Muhtasi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan.
Kwa mujibu taarifa hiyo, Jenerali Al-Burhan amethibitisha nia ya serikali yake ya kufikia amani kamili na endelevu kote nchini Sudan kwa njia itakayolinda maslahi ya taifa na matakwa ya wananchi wa Sudan na kuongeza usalama na utulivu katika ngazi za kitaifa na kikanda.
Mkuu huyo wa Jeshi la Sudan SAF amesisitiza tena kwamba, serikali yake imejitolea kuendeleza ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa ili kuimarisha amani na kuboresha hali ya kibinadamu, akisisitizia umuhimu wa kuendelea Umoja wa Mataifa kuisaidia Sudan katika nyanja zote.
Kwa upande wake, Lamamra amesema kuwa, ziara yake hiyo imefanyika kwa amri ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyempa jukumu la kufuatilia hali ya kisiasa, usalama na hali ya kibinadamu nchini Sudan.
Amebainisha kuwa, bado kuna fursa ya kuanzisha mazungumzo kati ya Wasudan wenyewe kwa wenyewe, mazungumzo ambayo yanaweza kusaidia kukomesha umwagaji wa damu nchini humo na kufikia utulivu wa kudumu. Amesisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa utaendelea kutoa msaada wowote unaohitajika wa kuhakikisha amani, maelewano na utulivu wa kudumu unarejea nchini Sudan.
Tangu tarehe 15 Aprili 2023, makundi mawili ya kijeshi ya SAF na RSF yamekuwa yakipigana nchini Sudan na kuisababishia maafa makubwa nchi hiyo.