Barcelona, Hispania. Mkurugenzi wa Michezo wa Barcelona, Deco, amesema kuwa Marcus Rashford alibebeshwa jukumu kubwa akiwa na umri mdogo Manchester United jambo ambalo lilichangia sana kushuka kwa kiwango chake katika klabu hiyo.

Rashford, ambaye kwa sasa yuko Barcelona kwa mkopo, alipanda chati kwa kasi kubwa baada ya kuibuka mwaka 2016 chini ya Louis van Gaal, akifunga mabao mawili katika mechi yake ya kwanza Ulaya.

Tangu wakati huo amekuwa miongoni mwa wachezaji waliotarajiwa kuiongoza United, licha ya kupitia misimu yenye changamoto na mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha zaidi ya watano katika kipindi chake.

Deco, amesema:

“Yuko mwenye furaha akiwa nasi. Marcus ni mchezaji mzuri sana. Alikabili jukumu la kuwa mchezaji muhimu United klabu kubwa sawa na sisi akiwa bado kijana sana.

“Ameumia pia kwa sababu ya mabadiliko ya kizazi ndani ya United. Miaka mitano iliyopita wamekuwa na ugumu kujijenga upya. Yeye amekuwa sehemu ya hilo, sio rahisi kwa mchezaji anayetarajiwa sana.

“Tulitafuta mchezaji wa aina yake, anayeweza kucheza nafasi zote tatu za mbele. Tumempata kwa mkopo kwa sababu alitaka sana kucheza Barcelona. Alivumilia hadi tukamaliza taratibu za fedha. Tumefurahi kuwa naye.”

Barcelona wana chaguo la kumsajili moja kwa moja mwishoni mwa mkopo wake, ingawa bado haijathibitika kama watalitimiza. Hata hivyo, Rashford ameonyesha thamani yake Catalonia, akifunga mabao mbili dhidi ya Newcastle aliporejea England mapema msimu huu.

Akiwa Barcelona, tayari amefunga mabao sita na anaonekana kurejea katika kiwango chake, tofauti na kipindi chake cha mwisho Old Trafford ambako licha ya kufikia msimu wa mabao 30, pia alikumbana na ukosoaji mkubwa kila mambo yalipokwenda vibaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *