
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema viongozi wake wamezuiwa kumwona mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu aliyepo katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam.
Lissu yupo mahabusu kwa kesi ya uhaini inayomkabili kwa takriban miezi minane sasa, tangu alipokamatwa Aprili 2025, akiwa mkoani Ruvuma kwa ziara ya chama hicho.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Magereza, Elizabeth Mbezi amesema hana taarifa iwapo kuna zuio la viongozi wa Chadema kumwona Lissu.
Taarifa ya kuzuiwa kumwona kiongozi huyo, imetolewa leo, Jumapili Novemba 30, 2025 na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Brenda Rupia.
Brenda kupitia taarifa hiyo, amesema viongozi hao wamezuiwa kuingia katika gereza hilo siku za karibuni walipokwenda kumuona kiongozi wao huyo.
“Katika siku za karibuni, viongozi wa chama akiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema na Katibu Mkuu, John Mnyika, wamezuiwa kuingia Gereza la Ukonga kumwona Mwenyekiti Lissu,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mnyika alipofika gerezani leo aliambiwa na askari magereza kuna maelekezo ya kutoruhusu kiongozi yoyote wa Chadema kuonana na Lissu.
“Hatua hii inaashiria zuio lisilo la kawaida, linalokiuka haki za msingi za mahabusu akiwa gerezani la kutembelewa na kuonwa na ndugu na jamaa zake,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Imeeleza Chadema inachukulia hatua hiyo kama uvunjaji wa haki za msingi za wafungwa na mahabusu na matumizi ya vyombo vya dola kuwanyanyasa wanasiasa wa upinzani.
Kutokana na hatua hiyo, chama hicho kimelitaka Jeshi la Magereza litoe maelezo kwa nini wanazuia Lissu asionane na viongozi wenzake.
Pia, kimetaka wadau wa ndani na nje ya nchi kufuatilia mwenendo huo kilichouita hatari kwa mustakabali wa demokrasia na maisha ya Lissu.
“Chadema inawaeleza wanachama na wananchi kwamba kitachukua hatua za kisheria, kisiasa na kidiplomasia kuhakikisha haki za Lissu na viongozi wa chama hazikiukwi.”
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Elizabeth amesema hana taarifa iwapo kuna zuio la viongozi wa Chadema kumwona Lissu gerezani.
Pia, amesema hana hata taarifa kuhusu viongozi wa chama hicho kwenda katika gereza hilo kumwona na kuzuiwa.
“Sina taarifa kama kuna zuio na sina taarifa kama kuna viongozi walienda kumwona wakazuiwa,” amesema Elizabeth.