Umoja wa Ulaya umekumbwa na changamoto nzito katika kuzishawishi nchi wanachama zikubali kuchangia fedha za kuendelea kuiunga mkono Ukraine kwenye vita vyao na Russia.

Kwa mujibu wa Pars Today, gazeti la Berliner Zeitung la nchini Ujerumani limesema katika makala yake kwamba: Umoja wa Ulaya umekumbwa na hali ngumu katika kuchangisha fedha za kupambana na Russia na kuendelea kuiunga mkono Ukraine.

Kwa mujbi wa gazeti hilo, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amepata pigo kubwa katika suala hilo. Uingereza, kiongozi asiye na mpinzani kwenye muungano unaoiunga mkono Ukraine imekataa kujiunga na mfuko wa kugharamia masuala ya kijeshi wa EU, na kimsingi mazungumzo kuhusu kujiunga London na mfuko huo wa euro bilioni 150, yameshindwa. Kufeli mazungumzo hayo kunaashiria kurudi nyuma katika uhusiano baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya baada ya Brexit, hasa wakati huu ambapo Ulaya inajitahidi kujipanga upya katika vita vyake dhidi ya Russia. Pia kushindwa mazungumzo hayo ni pigo kwa sekta ulinzi ya Uingereza ambayo kama ingelishirikiana na Umoja wa Ulaya, ingeliweza kufaidika na mpango huo.

Nchi ya Ukraine imesambaratishwa vibaya na vita

Von der Leyen pia amepata pigo katika mzozo wa matumizi ya mali za Russia zilizofungiwa na taasisi ya Euroclear huko Brussels. Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Bart de Witt ameongeza pingamizi lake kwa mpango wa Kamisheni ya Ulaya wa kutumia euro bilioni 140 za benki kuu ya Russia kama mkopo kwa Ukraine. Amesema mkopo huo utaleta mvurugano katika masoko ya fedha ya EU na kwamba walipa kodi wa Umoja wa Ulaya watalazimika kulipa kiasi chote cha fedha hizo kama baada ya vita vya Ukraine, nchi za Ulaya zitalazimishwa kurejesha fedha hizo kwa Russia. De Witt pia yuko chini ya shinikizo kutoka Russia, ambayo sasa inataka taarifa kamili ya mapato ya riba kutoka kwenye mali zake zilizofungiwa katika mabenki ya Ulaya.

Kwa miezi kadhaa sasa, Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, pia amekuwa akijaribu kuwasilisha mpango wa kutumia mali za Russia zilizofungiwa katika Umoja wa Ulaya kwa njia isiyo ya moja kwa moja ili kutoa msaada wa kifedha kwa Ukraine. Hata hivyo, hakuna makubaliano ya kisiasa yaliyoweza kufikiwa katika mkutano uliopita wa EU kutokana na upinzani wa Ubelgiji. Idhini ya Ubelgiji ya mpango huo ni muhimu kwa sababu mali hizo zinashikiliwa na taasisi ya kifedha ya Ubelgiji iitwayo Euroclear.

Kamisheni ya Ulaya imetumbukia kwenye shimo na wimbi la changamoto za kisiasa, kiuchumi na kisheria katika juhudi zake za kutafuta kufadhiliwa kifedha Ukraine, changamoto ambazo zimeuparaganya utekelezaji wa sera za hizo za misaada kwa Ukraine. Tangu vilipoanza vita vya Russia dhidi ya Ukraine, Umoja wa Ulaya umeshaipa Kyiv misaada mingi ya fedha, ikiwa ni pamoja na mikopo, ruzuku na misaada ya kuimarisha mifumo mbalimbali ya kiutawala ya Ukraine. Hata hivyo, kuendelea misaada hiyo kunahitaji kuweko rasilimali endelevu na makubaliano kati ya wanachama wa EU. Lakini suala hilo ni ngumu kufikiwa kwa sababu mbalimbali.

Moja ya changamoto kuu ni kutokubaliana nchi wanachama wa EU kuhusu jinsi ya kukusanya misaada hiiyo. Baadhi ya nchi zinapendelea kutoa msaada kwa jina la ruzuku ili Ukraine isikumbwe na madeni makubwa katika siku zijazo, huku nchi nyingine zikisisitizia wajibu wa kutumiwa mikopo midogo au mikopo inayofadhiliwa na masoko ya fedha ya Ulaya. Mvutano huo wa misimamo na mitazamo ya wanachama wa Umoja wa Ulaya imepunguza kasi ya kuchukua maamuzi kunakoishia kwenye kuchelewa kupewa misaada Ukraine.

Kyiv mji mkuu wa Ukraine ulivyosambaratishwa vibaya na vita. Umoja wa Ulaya hauna fedha za kukabiliana na changamoto zote hizi

Changamoto ya pili ni suala zima la kutumiwa mali za Russia zinazoshikiliwa na nchi za Ulaya. Baada ya kuanza vita huko Ukraine, Umoja wa Ulaya uliamua kuzuia sehemu kubwa ya mali za serikali na za watu binafsi wenye uraia wa Russia. Mjadala wa hivi sasa ni kuhusu iwapo mali hizo zinaweza kutumika kuisaidia Ukraine au la. Baadhi ya nchi zinasema kuwa, hatua hiyo ni hatari kwa upande wa sheria za kimataifa na itakuwa na athari mbaya kwa masuala ya kifedha ya barani Ulaya. 

Kiujumla ni kwamba, Kamisheni ya Ulaya imekumbwa na changamoto nyingi katika kutafuta fedha za kuisaidia Ukraine kuendelea na vita. Miongoni mwa changamoto hizo ni kukosekana kauli moja kati ya wanachama, changamoto kwenye masuala ya kisheria yanayohusiana na mali za Russia, mashinikizo ya kiuchumi ndani ya nchi za Ulaya, kupungua misaada ya Marekani baada ya kuingia madarakani Donald Trump, na uzorotaji katika kuchukua maamuzi. Mambo haya yanaonesha kwamba misaada endelevu kwa Ukraine inahitaji kuweko ubunifu wa mifumo ya kifedha, makubaliano mapana ya kisiasa, na usimamiaji makini wa rasilimali ili kuuwezesha Umoja wa Ulaya kukabiliana na mashinikizo ya ndani na nje na husun mashinikizo ya kivita na kiuchumi yanayotokea Ukraine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *