DAR ES SALAAM:MSIMU wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) utatangazwa kwa lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili, hatua inayolenga kuikuza lugha hiyo na kuiweka Afrika Mashariki katika ramani ya kimataifa ya utangazaji wa michezo.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni “Wanafamilia Tuna Kikao, Chimbo ni SuperSport”, Mkuu wa Masoko wa DStv Tanzania, Ronald Shelukindo, alisema dhamira ya kampuni hiyo ni kuhakikisha Watanzania wanafuatilia kwa ukaribu michuano hiyo na kufurahia utamaduni wa soka Afrika.
Shelukindo amesema msimu mpya wa AFCON umezinduliwa rasmi na DStv imethibitisha kuonesha mbashara mechi zote 52, ikiwemo michezo ya Kundi la Tanzania ‘Taifa Stars’ katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026 nchini Morocco.
“Mechi zitatolewa kwa lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili, Kiingereza, Kireno, Kifaransa na baadhi ya lugha za Kiafrika ili kuhakikisha mashabiki wanapata burudani kwa uelewa mpana,” amesema Shelukindo.

Katika kuongeza wigo wa utazamaji, kampuni za Canal+ na SuperSport zimethibitisha kuonesha mbashara michuano yote ya CAF TotalEnergies Morocco 2025, ambayo inatajwa kuwa miongoni mwa michuano mikubwa na yenye ushindani zaidi katika historia ya Afrika.
Taarifa ya pamoja ya CAF, Canal+ na SuperSport imeeleza kuwa Canal imepata haki za urushaji katika nchi zinazotumia lugha za Kifaransa, Kiingereza, Kireno na lugha mbalimbali za Kiafrika, huku SuperSport ikihudumia zaidi mashabiki wa Afrika Mashariki, Kusini na maeneo mengine ya bara hilo.
Ameongeza kuwa matumizi ya Kiswahili katika matangazo yatasaidia mashabiki wa Afrika Mashariki kupata ufahamu mpana zaidi wa michezo na kuwafanya wahusike moja kwa moja na matukio yanayoendelea uwanjani.