Mkutano wa 22 wa Nchi Wanachama wa Mkataba huo unaofahamika pia kama Mkataba wa Ottawa umeanza wiki hii mjini Geneva Uswisi huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kufuatia hatua za baadhi ya nchi kujiondoa au kusitisha utekelezaji wa baadhi ya wajibu, hatua ambayo haikutarajiwa ndani ya mkataba.
Katika ujumbe kwa njia ya video video kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu ameeleza wasiwasi wake kuhusu kudhoofika kwa misingi ya kibinadamu iliyowekwa kulinda raia dhidi ya silaha zisizobagua.
Amezitaka nchi kuongeza juhudi za kuhamasisha wanachama wapya na kuimarisha ahadi za waliopo.
Kazi ya kugundua mabomu ya kutegwa ardhini Syria.
Mabomu ya ardhini ni janga lisiloisha
Guterres amesisitiza madhara makubwa na ya muda mrefu ya mabomu ya ardhini, akiitaja kuwa ni “miongoni mwa silaha katili na zisizobagua zaidi kuwahi kutengenezwa.”
“Huwa zinaendelea kuua na kulemaza muda mrefu baada ya vita kumalizika. Na wanne kati ya waathiriwa watano ni raia mara nyingi watoto,” amesisitiza.
Katika maeneo mengi yenye migogoro, mabomu ya kutegwa ardhi bado ynaendelea kuumiza jamii hata miongo kadhaa baada ya mapigano kukoma. Waathiriwa hukabiliana na safari ndefu za matibabu na ukarabati, pamoja na changamoto za kijamii na kiuchumi.
Uchafuzi wa ardhi kutokana na mabomu pia huzuia ufikaji wa misaada ya kibinadamu, kuchelewesha ujenzi na kuzuia maendeleo endelevu.
Mfumo uliowahi kufanikiwa, lakini uko chini ya shinikizo
Licha ya changamoto za sasa, Mkataba wa Ottawa umeleta mafanikio makubwa kwa zaidi ya miaka 25.
Idadi ya vifo na majeraha imepungua kwa kiasi kikubwa, akiba kubwa ya mabomu ya ardhini yameteketezwa, na maeneo mengi yaliyokuwa yameathirika yamesafishwa.
Jumla ya nchi 166 zaidi ya robo tatu ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa sasa ni sehemu ya mkataba huo.
Uanachama wa hivi karibuni wa Visiwa vya Marshall na Tonga unaonyesha mwendelezo wa maendeleo chanya.
Hata hivyo, Katibu Mkuu ameonya kuwa mafanikio haya yako hatarini endapo nchi zitaanza kulegeza utekelezaji wa wajibu wao.
Mfanyakazi wa UNMAS akondoa mabomu ya kutegwa ardhini nchini Sudan Kusini
Kufufua ahadi ya kimataifa kwa udhibiti wa silaha
Kampeni ya Katibu Mkuu kuhusu udhibiti wa silaha za kibinadamu na hatua dhidi ya mabomu inayoratibiwa na UNODA na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uteguzi wa Mabomu UNMAS, pamoja na Kikundi cha Uratibu cha Mashirika ya Kimataifa ya Kukabiliana na mabomu inataka kuchukuliwa hatua za haraka za pamoja.
Kampeni hii inalenga kuimarisha sheria za kimataifa za kibinadamu, kuendeleza ushirikiano, na kuhakikisha kuwa ahadi za mkataba zinatafsiriwa katika matokeo halisi yanayowalenga watu.
Mkutano wa 22 wa Nchi Wanachama unatoa fursa muhimu ya kuthibitisha upya madhumuni ya Mkataba na kuimarisha juhuduza kudhiiti unyanyapaa dhidi ya matumizi ya mabomu ya ardhi yanayouwa watu.
“Lazima tujitolee tena kulinda maisha, kuheshimu sheria za kimataifa na kurejesha matumaini kwa jamii zinazotishiwa na mabomu ya kutegwa ardhini,” amesema.