Kwenye makubaliano yaliyofikiwa Novemba 27, mwaka 2024, yaliyolenga kuumaliza uhasama wa zaidi ya mwaka mmoja kati ya Israel na kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah, Israel ilitakiwa kuwaondoa wanajeshi wake kikamilifu kutoka Lebanon katika kipindi cha siku 60.

Na kwa upande wa kundi la Hezbollah ilikuwa liondoe vikosi vyake katika eneo la kaskazini mwa Mto Litani, takriban umbali wa kilomita 30 kutoka kwenye eneo la mpaka kati ya Lebanon na Israel, na miundombinu yake ya kijeshi katika eneo hilo ilibidi ibomolewe.

Hata hivyo, mwaka mmoja baadae baada ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano, Shirika la Habari la Ufaransa, AFP limebaini kupitia picha za setilaiti kutoka Planet Labs PBC kwamba Israel imeweka kambi za wanajeshi wake katika maeneo matano ambayo inayaona kuwa ya kimkakati, ikisema kwamba inataka kuhakikisha kundi la Hezbollah halifanyi shughuli zozote za kijeshi kusini mwa Lebanon.

Lebanon-Beirut 2025 | Wanajeshi wa ebanon wakimarisha ulinzi baada ya shambulio la Israel dhidi ya Hezbollah
Wanajeshi wa Lebabon wakionekana kuweka ulinzi baada ya Israel kutekeleza shambulizi dhidi ya Hezbollah nchini humoPicha: Anonymous/Middle East Images/IMAGO

Kambi hizo ziko katika eneo la Mstari wa Buluu unaotenganisha Lebanon kutoka Israeli na Milima ya Golan, ambao ni mpaka uliowekwa wakati wa makubaliano. Nafasi hizi zinaruhusu jeshi la Israel kudhibiti vijiji kadhaa vya mpakani nchini Lebanon, Israel inasema hatua yake hiyo ni muhimu katika kuzilinda jamii za Israel zilizo karibu na maeneo hayo ya mpakani.

Jeshi la Israel lafanya ubomoaji wa kimfumo dhidi ya Hezbollah

Israel ina uwezo wa kuvitazama moja kwa moja vijiji vya Kfar Kila, Aita al-Shaab, Maroun al-Ras, Aitaroun, Blida, Markaba na Hula ambavyo ni miongoni mwa maeneo yaliyoharibiwa zaidi na mashambulizi ya ardhini ya Israel. Picha za setilaiti zinaonyesha kwamba majengo yote karibu na kituo cha kijeshi cha Hatzivivoni, kati ya Hula na Markaba, yameharibiwa kabisa.

Picha za setilaiti pia zinaonyesha kwamba barabara za kuyafikia maeneo haya zimepanuliwa kwa kiasi kikubwa ili kurahisisha usafiri wa magari. Kama ilivyo katika Ukanda wa Gaza, jeshi la Israel linafanya ubomoaji wa kimfumo wa majengo na miundombinu katika vijiji vilivyo karibu na mpaka, eneo ambalo pia lililipuliwa kwa mabomu mengi.

Mzozo wa Mashariki ya kati baina ya Israel na wanambambo wa Hezbollah
Isral yaidisha mashambulizi yake dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah kusini mwa LebanonPicha: Gali Tibbon/AFP/Getty Images

Kulingana na ulinganisho wa picha za setilaiti na watafiti wa Marekani Corey Scher na Jamon Van Den Hoek kutoka Chuo Kikuu cha Oregon, ambao mara ya mwisho ulisahihishwa mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu wa 2025, kijiji cha Kfar Kila, kimeonesha kuwa kimeharibiwa kwa asilimia 65, huku kijiji cha Aita al-Shaab kikiwa kimeharibiwa kwa asilimia 57 na kile cha Yarin uharibifu wake ukiwa ni wa asilimia 55.

Kulingana na watafiti, ishara zote zinaashiria kuwa Jeshi la Israel linaendelea kuziimarisha ngome zake zilizopo kusini mwa Lebanon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *