Maelfu ya waandamanaji jana Jumamosi walimiminika kwenye eneo la katikati mwa mji mkuu wa Uingereza, London katika maandamano ambayo ni sehemu ya kampeni ya “Komboa Mateka Wapalestina”, wakitaka kuachiliwa huru Wapalestina zaidi ya 9,100 wanaoshikiliwa katika magereza ya kutisha ya utawala wa kizayuni wa Israel, wakiwemo zaidi ya wanawake na watoto 450.

Huku wakipeperusha bendera za Wapalestina na kuvaa utepe mwekundu unaoashiria kuwekwa kizuizini bila kufunguliwa mashtaka, waandamanaji hao walilaani mwenendo wa kawaida wa utawala wa kizayuni wa kuwatesa, kuwabaka, kuwakamata kiholela na kuwanyanyasa kinyama wananchi madhulumu wa Palestina.

Waandamanaji hao waliushutumu utawala ghasibu wa Israel kwa kuendesha mfumo uliojikita kwenye ubaguzi wa rangi wa apathaidi na mauaji ya kimbari, na kutoa wito wa kukomeshwa mara moja vifungo vya kuwarundika Wapalestina kwa halaiki.

Umati wa waandamanaji waliokusanyika katika jiji la London ulielekeza pia hasira zake kwa serikali ya Uingereza, ukiikosoa kwa kuwafungulia mashtaka wanaharakati wanaopinga usafirishaji wa silaha kuelekea Israel huku ikiendelea kuufadhili na kuvipa kinga ya kisiasa vitendo vya utawala huo wa kizayuni huko Ghaza na kwenye maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.

Kampeni hiyo  ya ‘Komboa Mateka Wapalestina’ imeenea pia kote barani Ulaya ambapo huko Paris, Ufaransa na Athens, Ugiriki jana hiyohiyo kulishuhudiwa umati mkubwa wa watu walioandamana kuonyesha uungaji mkono wao kwa Palestina huku makumi ya maelfu ya watu wakijaza mitaa na barabara mbalimbali kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina.

Siku ya Ijumaa, waandamanaji walikusanyika nje ya ubalozi wa Israel huko Copenhagen, Denmark chini ya kauli mbiu ya “Walete Nyumbani”, wakionyesha majina na simulizi za Wapalestina wanaoshikiliwa bila kufunguliwa mashtaka.

Ripoti ya Shirika Lisilo la Kiserikali la Madaktari kwa ajili ya Haki za Binadamu-Israel (PHRI) imeorodhesha vifo vya wafungwa wa Kipalestina wasiopungua 94 vilivyotokea wakati Wapalestina hao wakiwa kizuizini kwenye jela za Israel. Shirika hilo limesisitiza kuwa idadi halisi ya vifo huenda ikawa kubwa zaidi ya hiyo iliyotajwa. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na PHRI, Wapalestina hao walikufa kutokana na mateso, kushambuliwa, kupuuzwa makusudi kwa kutopatiwa matibabu au kutokana na hali mbaya sana ya utapiamlo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *