London, England. Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, amepongeza kikosi chake kwa kupambana kikiwa na wachezaji 10 na kuizuia Arsenal kuendelea kupaa kileleni mwa Ligi Kuu England.
Maresca hakuishia hapo kwani alielezea madai ya upendeleo na utofauti wa maamuzi ya waamuzi dhidi ya timu yake.
Maresca amekiri kuwa Moises Caicedo alistahili kadi nyekundu aliyopewa dakika ya 38 kufuatia kumchezea vibaya Mikel Merino, lakini alishangazwa kwa nini mwamuzi Anthony Taylor hakumtoa nje beki wa Arsenal, Piero Hincapié, aliyempiga Trevoh Chalobah kiwiko na kumuacha na shavu lililovimba.
Kocha huyo amesema tukio hilo limeendeleza mlolongo wa maamuzi ya ajabu, akirejea pia mechi ya awali dhidi ya Tottenham ambapo Rodrigo Bentancur hakupata kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Reece James, tukio ambalo Maresca anasema tukio hilo lilikuwa sawa kabisa na la Caicedo.
“Kadi nyekundu ya Moises ni ya haki, ndiyo. Lakini kwa nini ile ya Bentancur dhidi ya Reece haikutolewa? Nachemka kuelewa namna wanavyotafsiri makosa. Zote ni kadi nyekundu, kwa nini moja itolewe na nyingine isiwe?” alisema Maresca kwa hasira.
Kuhusu tukio la Chalobah, Maresca amefichua kuwa mwamuzi amedai hakukuwa na kiwiko:
“Nimemuuliza mwamuzi, akaniambia siyo kiwiko. Lakini mchezaji ana jicho jeusi na alitiwa barafu wakati wa mapumziko!”
Hincapié alipewa tu kadi ya njano, huku Arsenal ikimaliza mchezo na jumla ya kadi sita katika dabi hiyo ya London iliyokuwa na ukali wa hali ya juu.
Maresca ameongeza kuwa licha ya yote, ameridhishwa na namna timu yake ilivyocheza hadi kufunga kupitia Chalobah kabla ya Merino kusawazisha.
“Arsenal kwa sasa ndiyo timu bora Premier League na hata Ulaya. Lakini 11 dhidi ya 11 tulikuwa bora kuliko wao. Tukifika Februari au Machi tukiwa kwenye nafasi hii, basi tutakuwa kwenye mbio za ubingwa,” ameongezea Maresca kocha wa Chelsea.
Arteta: “Tulikosa wachezaji, ratiba ilikuwa ngumu”
Kwa upande wa Arsenal, kocha Mikel Arteta amesema kikosi chake kimepambana kadiri ya uwezo wake licha ya kuwa pungufu ya wachezaji kadhaa muhimu akiwemo nahodha na washambuliaji wake wa kwanza.
Arsenal ililazimika kucheza bila Saliba na Gabriel, huku Leo Trossard, Havertz na Gabriel Jesus pia wakiwa nje kutokana na majeraha.
“Tumecheza mechi tatu ngumu sana ndani ya muda mfupi. Tumepoteza wachezaji na ratiba haikutupa nafasi ya kupumua. Kwa ujumla ni wiki ngumu lakini yenye mambo mazuri,” amesema Arteta.
Kuhusu hali ya Saliba, Arteta amesema:
“Hatuna uhakika bado. Atapimwa tena kesho ili tujue ukubwa wa tatizo.”