Madrid, Hispania. Real Madrid imeshindwa kurudi kwenye kilele cha Ligi Kuu Hispania maarufu kama La Liga baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Girona.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Montilivi ilishuhudiwa wenyeji, Girona wakianza kutangulia mbele baada ya Azzedine Ounahi kufunga bao mwishoni mwa kipindi cha kwanza akimalizia kwa ustadi pasi ya Viktor Tsygankov.
Hata hivyo, katika kipindi cha pili dakika ya 67 mshambuliaji wa Madrid, Kylian Mbappé alibadilisha matokeo baada ya kupachika bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti iliyosababishwa na beki wa Girona, Hugo Rincon kumchezea vibaya Vinicious Junior ndani ya eneo la hatari.
Madrid iliendelea kufanya majaribio mengine ya kupata bao la ushindi lakini hayakuweza kuzaa matunda hadi dakika 90 za mwamuzi, De Burgos zilipomalizika.
Matokeo hayo yameifanya Los Blancos ishindwe kurejea katika kilele cha La Liga huku mahasimu wao Barcelona wakiwa ndiyo vinara baada ya kupata matokeo ya ushindi katika mchezo wao wa juzi ilipoichapa Deportivo Alaves mabao 3-1.
Kwa upande wa Girona wao wamefufua matumaini ya kupambana kubaki katika La Liga ikifikisha pointi 12 ikiwa nafasi ya 18 sawa na Osasuna iliyopo nafasi ya 17.
Madrid imeshindwa kupata matokeo ya ushindi katika michezo miwili mfulilo ya La Liga baada kupata sare katika mchezo uliopita ilipokuwa ugenini dhidi ya Elche.
Vijana wa Xabi Alonso watakuwa na kibarua kingine ugenini Desemba 3, 2025 ambapo watavaana na kikosi cha Athletic Bilbao katika Uwanja wa San Mames.