Moshi. Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wamelalamikia majengo na maeneo ya wazi yaliyotelekezwa kwa muda mrefu, wakidai yanatumika kufanyia vitendo viovu ikiwamo vya danguro na maficho ya wahalifu, hali inayohatarisha usalama wa wananchi.

Mwananchi imepita katika baadhi ya maeneo ya mitaa ya Msufini, Upinde, Msaranga na Mtaa wa Hindu katika manispaa hiyo na kushuhudia baadhi ya majengo ambayo yametelekezwa kwa muda mrefu bila kufanyiwa uendelezwaji.

Wakizungumza na Mwananchi hivi karibuni kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa mji huo, wamedai kuwa wakati wa usiku majengo hayo pamoja na baadhi ya vichochoro vimekuwa kero kwa kuwa, watu hutumia kufanya madanguro, kuvutaji bangi na wakati mwingine wizi.

Adelina Mushi, mmoja wa wakazi wa Moshi amesema licha ya kutoa taarifa mara kadhaa kwa viongozi wa mitaa, bado hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kuzuia matumizi mabaya ya majengo hayo.

“Hizi nyumba ambazo zipo tu miaka mingi hazijaendelezwa, zimekuwa kero kwa wananchi, usiku unashuhudia watu wakiingia bila kujali, asubuhi unakuta mabaki ya vitu vinavyoashiria kuwa palitumika kama danguro, tunaomba mamlaka zichukue hatua,” amesema mkazi huyo.

Pia, amesema hali hiyo imekuwa ikiathiri usalama wa watoto wa kike, hasa wale wanaolazimika kupita karibu na maeneo hayo nyakati za asubuhi au jioni.

Mushi amesema majengo hayo ambayo yameachwa bila kutumika kwa muda mrefu, yamegeuka kuwa kimbilio la watu wasiokuwa na nia njema, hali inayochochea ongezeko la vitendo vya kihalifu kwenye maeneo ya makazi.

Mkazi mwingine, Genesis Kiwelu amesema katika manispaa hiyo yapo majengo ambayo yametelekezwa kwa zaidi ya miaka 30 na hayajafanyiwa uendelezwaji, hivyo hayaleti taswira nzuri ndani ya mji huo.

“Yapo majengo ambayo yapo zaidi ya miaka 35 au 40, yapo vilevile na hujui yanafanya kazi gani, yamekuwa yakikaa tu, katika hali ya uchakavu na hata ukipita hayaleti sura nzuri ya mji wa Moshi,”amesema Kiwelu.

Pia, ameshauri Serikali iangalie namna ya kuwatambua wanaomiliki majengo hayo ili wajue mipango yao na kutafuta njia rahisi ya kudhibiti vitendo viovu katika majengo hayo.

“Haya majengo yanapoachwa hivi, matumizi yake ni lazima yawe mabaya na usalama wa watu unakuwa sio mzuri lakini pia yanaharibu vijana wetu kwa kuwa wapi watu wasio wema ambao wanayafanya kama madanguro wakati wa usiku, yanaharibu jamii yetu kwa jumla,” amesema Kiwelu.

“Serikali ichukulie umuhimu wake kuona sasa haya majengo yanapatiwa ufumbuzi wa kutosha, kama yametelekezwa  Serikali ione namna itafanya mpango wa maeneo haya yaboreshwe kufuatana na mpango mji.”

Stela Bundala, mkazi wa manispaa hiyo, amesema wapo wananchi jioni na usiku wanaogopa kupita maeneo hayo kutokana na kuwapo vitendo vibaya, kama vile ubakaji.

“Yapo majengo yamekaa muda mrefu sana na yamekuwa ni hatarishi kwa wakazi wa Moshi, wafanyabiashara na wafanyakazi wa maeneo haya, kwa sababu yanaweza kuwa ya kuhifadhi wezi, lakini kutengeneza wavuta bangi ambao wanajificha au mali za wizi zinaweza kufichwa kule na zaidi kutumika kama danguro,” amesema.

 Viongozi wa mitaa wakiri tatizo

Wenyeviti wa mitaa hiyo, wamekiri baadhi ya maeneo hayo kutumika ndivyo sivyo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Msufini, Elieth Mshana amesema baadhi ya vijana wamekuwa wakiyatumia majengo hayo kama sehemu ya kufanyia uhalifu na matukio mengine ambayo hayafai kwenye jamii.

“Majumba haya yamekuwa yakitumika kwenye mambo maovu na imekuwa ni tatizo, licha ya kwamba hatujawahi kulifanyia kazi japo ni tatizo ambalo lipo.

“Kuna vijana walikuwa wanaiba vyuma na walikuwa wakitumia maeneo haya kama sehemu ya kuhifadhia vifaa vya wizi, wanalala huko na wanapikia huko pamoja na kufundisha vijana wadogo kufanya maovu, kama kuvutia bangi, ulawiti na kufanya kama sehemu ya danguro,” amesema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Rengua, Ladislaus Lyimo amesema yapo maeneo ya wazi (vichochoro) ambayo yamekuwa yakitumika kama sehemu ya kufanyia uovu na alishapokea malalamiko kutoka kwa wananachi wa maeneo hayo.

“Kuna  maeneo kunapokuwa wazi watu wanayatumia kama madanguro, ukienda pale Barabara ya Upinde, watu wanatumia kufanyia vitendo viovu, kuna eneo kama Boma Road ambako kunafanyika vitendo viovu pia.

“Nilishapokea malalamiko kwa wananchi kuhusu haya maeneo kwamba vijana wanakwenda kukaa katika hayo maeneo na kufanya vitendo viovu kama vibaka na kufanya danguro,” amesema.

Akizungumzia majengo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amesema wamepokea maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi hao, kuhusu nyumba hizo ambazo hazijaendelezwa kwa muda mrefu.

Amesema Serikali kupitia watendaji wake wa mtaa na vijiji watapita kufanya uhakiki katika maeneo hayo ili kufahamu wamiliki wa hayo majengo.

“Katika ufuatiliaji tumeona, lakini tumepokea maoni ya wananchi ya uwepo wa nyumba ambazo hazijamalizwa kwa muda mrefu na zimetelekezwa kwa muda mrefu, zimebaki kama mapagale.

“Tunao mpango mrefu kupitia watendaji wetu wa mtaa na wenyeviti, kupita kufanya uhakiki wa nyumba hizo ili tuweze kujua kwenye kila mtaa au kata hayo mapagale nani anayemiliki, yuko wapi na kujua mpango wake wa kumalizia hizo nyumba,” amesema.

Mnzava amesema nyumba ambazo hazijaendelezwa ni changamoto ya kiusalama katika jamii ambayo imestaarabika, huku akatoa wito kwa wamiliki wote kuweka mpango wa umaliziaji wa majengo hayo.

“Nitoe wito na kuwataka wamiliki wote wa majengo hayo katika maeneo yetu ya Wilaya ya Moshi, kufanya usafi katika nyumba hizo, waweke mpango wa umaliziaji ili sasa yawe makazi rasmi, kwa kuwa kubaki hivyo inaharibu mandhari na taswira ya mji wetu wa Moshi.

“Nataka wilaya yetu iendelee kuwa salama na mandhari yetu ya Moshi iendelee kuwa nzuri ya kuvutia, lakini kuepusha maficho ya uhalifu ndani ya mji wetu wa Moshi,”amesema Mnzava.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *