“Haya si marekebisho ya kawaida ya kiufundi,” amesema. “Ni marekebisho makini na yenye kuzingatia na yanayojumuisha dharura na azma ya mageuzi tunayoitekeleza.”

Makadirio yaliyorekebishwa yanahusiana na bajeti ya mpango wa mwaka 2026 na akaunti ya msaada kwa operesheni za kudumisha amani kwa kipindi cha mwaka 2025/26.

Kwa mara ya kwanza, yanajumuisha matokeo ya awali ya Mpango wa UN80, ambao ni juhudi kubwa za kuboresha na kurahisisha mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Maamuzi magumu, punguzo la asilimia 15 katika bajeti ya kawaida

Guterres amefafanua upunguzaji mkubwa, kwa bajeti ya kawaida ya 2026 wa Dola bilioni $3.238 bilioni, ikiwa ni punguzo la asilimia 15.1 ikilinganishwa na mwaka uliopita na kupunguzwa kwa nafasi za wafanyakazi 2,681, sawa na asilimia 18.8. “Hatua hizi ni upunguzaji mkubwa wa bajeti unaoathiri watu halisi, familia, na maisha yao na hatupaswi kamwe kupoteza mwangwi wa kipengele hiki cha kibinadamu,” amewaambia wajumbe.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa upunguzaji huu wa bajeti umelengwa kwa makini ili kuepuka kuathiri majukumu ya msingi ya Umoja wa Mataifa. “Hatujachukua mbinu ya kupunguza kwa kiwango sawa kwa kila sehemu,” amesema. “Tumelinda uwiano kati ya amani na usalama, maendeleo endelevu na haki za binadamu.”

Ameainisha uamuzi wake wa kutohusisha UNRWA na programu za maendeleo ya Afrika katika upunguzaji, akisema kupunguza hapo “kungeleta matokeo mabaya.”

Mfumo mpya wa kiutendaji: kuunganisha, kuhamisha na kuokoa gharama

Makadirio yaliyorekebishwa yanaingiza mabadiliko makubwa katika operesheni za Umojawa Mataifa, ikiwa ni pamoja na jukwaa la kiutawala la pamoja, kuunganisha mishahara kimataifa kati ya New York, Entebbe na Nairobi, na mapitio ya kazi zinazoweza kuhama hadi nchi zenye gharama ya chini.

“Hii ni sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza matumizi ya biashara na kufanikisha akiba ya muda mrefu,” amesema Guterres.

Tangu 2017, Umoja wa Mataifa umeokoa dola milioni 126 kwa kumaliza mikataba ya makazi ya kibiashara mjini New York, ameongeza.

Kuunganisha zaidi makazi kunatarajiwa kuokoa dola milioni 24.5 kila mwaka kuanzia 2028.

“Tunalinganisha rasilimali na vipaumbele, kuboresha operesheni za ndani, na kuzingatia changamoto ya mazingira ya kifedha.”

Upunguzaji mkubwa kwa operesheni za kisiasa

Operesheni maalum za kisiasa pia zitaathirika, na bajeti iliyorekebishwa ya 2026 ya Dola milioni 543.6 milioni, ikwa ni punguzo la asilimia 15 kutoka mpango wa awali na asilimia 21.6 chini ya bajeti ya 2025.

Hii ni pamoja na kupunguzwa kwa nafasi 1,215. Guterres amesema upunguzaji huu unatokana na kufungwa kwa operesheni, ufanisi na juhudi za “kuimarisha utamaduni wa ufanisi.”

“Haya ni maamuzi makini si kwa hesabu tu,” amesema. “Tulipitia mahitaji kwa makini, kurahisisha wafanyakazi, na kutafuta njia za kupunguza marudio huku tukiboresha uwezo wa kitaifa.”

programu za mapema za kujiuzulu, usawa, na uwiano wa kikazi

Akitambua athari za kibinadamu za upunguzaji wa bajeti wa nguvu kazi, Guterres ameeleza hatua za kupunguza athari ikiwa ni pamoja na programu za mapema za watu kujiuzulu na upanuzi wa nafasi za ndani. “Hii itatupa fursa ya kupunguza kwa kiasi kikubwa kuondolewa kwa wafanyakazi bila hiari,” amesema. “Pia itapunguza athari kwa uwiano wa kijiografia na kupunguza gharama za kuondolewa.”

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa mpangilio wa wafanyakazi utashughulikiwa kwa haki na utunzaji. “Tutafanya kila juhudi kuhakikisha wenzetu wanasaidiwa wakati wa kipindi hiki cha mabadiliko,” amewahakikishia wajumbe.

Mpango wa UN80: Kipimo cha UN yenye mnepo

Guterres amesema Mpango wa UN80 unaoendelea sasa kwa sehemu tatu unawakilisha mabadiliko makubwa katika mfumo wa Umoja wa Mataifa. Sehemu ya 2 inalenga kuboresha mipango na utekelezaji wa dhamana, Sehemu ya 3 inalenga mabadiliko ya kimuundo. “Mapendekezo haya yanagusa Sekretarieti, fedha, programu na mashirika maalumu,” amesema na kuongeza kuwa “Lengo lake moja ni kubadilisha jinsi tunavyofanya kazi.”

Amebainisha hatua 15 mpya za kuongeza mwonekano thabiti, kuimarisha ripoti na kulinganisha vipimo vya matokeo. Mpango mpya wa Hatua uliozinduliwa wiki tatu zilizopita unatoa mfumo wa kujiweka kwa ushirikiano na uwajibikaji.

Onyo kuhusu rasilimali: Madeni bado hayajalipwa

Katibu Mkuu ametoa onyo kali kuhusu hali dhaifu ya kifedha ya Umoja wa Mataifa. “Madai sasa yanasimama katika dola bilioni 1.586 “ amesema, akibainisha kuwa dola milioni 709 kutoka 2024 bado hazijalipwa na dola milioni  877 milioni za mwaka 2025 bado hazijapokelewa. “Nimekuwa nikiwahimiza Nchi Wanachama kulipa kwa wakati na kikamilifu.”

Amesema kusitishwa kwa muda kwa kurejesha mikopo kunaweza kuwa muhimu ili kulinda operesheni.

Licha ya hali ya kifedha, Guterres amesisitiza azma ya Umoja wa Mataifa ya kufanikisha malengo yake. “Mahitaji ya Nchi Wanachama na watu tunaowahudumia yanaongezeka. Dhamira yetu haijawahi kuwa muhimu au husika zaidi kuliko sasa,” amesema.

Akimalizia hotuba yake, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa hatua: “Pamoja, tunaweza kuhakikisha Umoja wa Mataifa haupo tu kwa ajili ya madhumuni yake bali pia unaofaa kwa zama zijazo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *