Nigeria. Mwimbaji maarufu wa Nigeria, Blessing Akiode Mariam, anayejulikana zaidi kama Candy Bleakz, ameibua wasiwasi mtandaoni baada ya video yake kusambaa ikimwonyesha katika hali ya kutetemeka muda mfupi baada ya kudaiwa kuporwa huko Cape Town, Afrika Kusini.

Katika video hiyo, msanii huyo alionekana akiwa na mshtuko mkubwa, huku akisimulia jinsi alivyoporwa mali zake za thamani licha ya uwepo wa maafisa wa usalama karibu na eneo la tukio.

Candy Bleakz alieleza jinsi alivyokerwa na kitendo hicho, akidai askari hao walishindwa kuchukua hatua ingawa, kwa maelezo yake kulikuwa na nafasi ya wazi kumkamata mwizi huyo.

Pia aliongeza kama tukio hilo lingetokea Nigeria, huenda mtuhumiwa angekamatwa na mali zake kurejeshwa.

Amesema watuhumiwa bado walikuwa karibu kabisa wakati huo, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.

Candy Bleakz pia alifichua vifaa vya thamani ya takribani Naira 10 milioni viliibiwa.

Video hiyo pia ilimuonyesha akiwa na jeraha lililokuwa likivuja damu usoni, ambalo baadaye alilifunika kwa leso alipokuwa akiendelea kuzungumza.

Tukio hilo limezua mijadala mtandaoni, huku mashabiki wengi wakionyesha wasiwasi juu ya usalama wake na kutoa wito wa kuimarishwa kwa ulinzi kwa wageni na wasanii wanaosafiri kwenda nje ya nchi, hususani wanapokuwa Afrika Kusini kunakoelezwa kuna usalama mdogo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *