Angalau watu kumi na wawili, akiwemo mchungaji, wametekwa nyara siku ya Jumapili, Novemba 30, wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa la vijijini katikati mwa Nigeria, tukio la hivi karibuni katika mfululizo wa utekaji nyara wa watu wengi nchini humo katika wiki chache tu. 

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Nigeria inakabiliwa na utekaji nyara wa watu wengi mara kwa mara, kitendo ambacho kimeenea tangu kutekwa nyara kwa wasichana wa shule wapatao 300 na Boko Haram huko Chibok, katika Jimbo la Borno (mashariki), mwaka wa 2014. Hata hivyo, wiki za hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la vitendo hivi, na kumfanya rais wa Nigeria kutangaza “dharura ya usalama wa taifa” mnamo Novemba 26.

Katikati mwa Nigeria, kanisa linalopatikana katika kijiji cha Ejiba, kilichoko katika eneo la Yagba Magharibi katika Jimbo la Kogi, “lilishambuliwa mnamo Novemba 30 na majambazi,” Kingsley Femi Fanwo, kamishna wa habari wa jimbo hilo, ameliiambia shirika la habari la AFP. “Watu kumi na wawili hawajulikani walipo, na polisi, waliofika kwa helikopta, wanaendelea na msako wao. Walimteka nyara mchungaji na baadhi ya waumini,” ameongeza.

Makundi yenye silaha, yanayojulikana kama “majambazi”, yanatishia majimbo mengi kaskazini-magharibi na katikati mwa nchi, ambapo yamekuwa yakilazimisha fidia ili kuwaachilia huru mateka, kushambulia vijiji, kuua wakazi, na kuchoma nyumba baada ya kuzipora.

Alipotangaza “dharura ya usalama wa taifa” mnamo Novemba 26, Rais Bola Tinubu alibainisha kwamba maeneo ya ibada yanapaswa kuhakikisha uwepo wa usalama wakati wa mikusanyiko, hasa katika maeneo nyeti. “Maeneo ya ibada yaliyo nje kidogo ya miji yanapaswa pia kufikiria upya kufanya ibada katika maeneo yenye uhalifu mkubwa hadi hali itakapoimarika,” Kingsley Femi Fanwo amesema katika taarifa.

Katika wiki mbili zilizopita, mamia kadhaa ya watu walitekwa nyara kote nchini, wakiwemo zaidi ya wanafunzi 300 kutoka shule ya Kikatoliki katika Jimbo la Niger (katikati mwa Nigeria) na waumini 38 wa kanisa katika Jimbo la Kwara (magharibi mwa Nigeria), ambao wameachiliwa huru.

Kuongezeka kwa utekaji nyara kunakuja muda mfupi baada ya madai ya Donald Trump kwamba Wakristo nchini Nigeria “wanauawa” na “magaidi.” Kulingana na serikali ya Nigeria na wataalamu wengi, utekaji nyara huo unawaathiri Wakristo na Waislamu bila ubaguzi na hasa unasababishwa na madai ya fidia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *