Tabora. Watumishi watatu wa kada ya afya akiwemo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Urambo wamesimamisha kazi, huku wengine wawili wakiendelea kuhojiwa, kufuatia sakata la mgonjwa kubakwa na tabibu na matukio mengine ya uzembe kazini.

Agizo hilo limetolewa leo Desemba 1,2025  na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha wakati wa ziara maalumu ya kamati ya usalama ya mkoa wilayani Urambo.

 Mbali na mambo mengine ziara hiyo imefanyika kufuatia kuwapo  matukio tofauti kwa baadhi ya watumishi kutoa huduma mbaya za afya kwa wananchi ikiwemo sakata la kubakwa mgonjwa lililotokea Novemba 24,2025.

Hatua ya kuwasimamisha imechukuliwa siku moja baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kutoa maelekezo ya kuchukuliwa hatua kwa muhusika wa kitendo hicho cha ubakaji.

Dk Mwigulu alitoa maelekezo hayo Jumapili Novemba 30, 2025 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara viwanja vya Magufuli, Leganga wilayani Arumeru, baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na vurugu za Oktoba 29, 2025.

Ambapo alimwagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi, kumsimamisha kazi mganga mmoja mkoani Tabora, anayedaiwa kumchoma mgonjwa sindano ya usingizi kisha kumbaka.

“Mtumishi wa umma ambaye atakiuka mambo ya maadili, nidhamu kazini, kusikiliza kero na kutotatua kero, lugha mbaya na mengine wala asihamishwe afukuzwe, Watanzania wako wengi vijana wako wengi hatuna uhaba wa vijana wenye maadili.”

“Leo nimepata taarifa kule Urambo, Tabora jambo la ajabu kabisa na niwapongeze uongozi wa Mkoa wa Tabora kuanzia Mkuu wa Mkoa kwa kuchukua hatua, wasingeliona hili na kuchukua hatua ningewafukuza wao leo.”

“Alikuwepo mganga mmoja pale Urambo, ameenda kumtibu binti wa miaka 18 ana tatizo la uzazi, amemaliza kumsikiliza amemdanganya anatakiwa kutibiwa kwa kuchomwa sindano ya usingizi, akiwa kwenye sindano ya usingizi amembaka. Mambo ya ajabu kabisa amembaka,”alisema Dk Mwigulu na kuongeza.

“Mungu ni mwema dawa ya usingizi ikaisha, hajamwekea hiyo dawa, binti kaamka kaona, nesi aliyekuwa anasaidia ameona, yule binti ameolewa na mume wake alikuwepo, mambo ya ajabu kabisa, madaktari wamejiridhisha kwamba mgonjwa amebakwa,” alisema.

Akielezea tukio hilo mwathirika ambaye jina lake limehifadhiwa kwa kuheshimu utu wake amesema kuwa mnamo Novemba 24,2025 akiwa na muwe wake walienda katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo kwa ajili ya matibabu zaidi  kufuatia kuwa na tatizo la uzazi na kupokewa na tabibu huyo,  ambaye alitumia chumba cha upasuaji kumuhudumia mgonjwa huyo.

“Alinibaka kwenye chumba hichohicho.”

Amesema wakati tabibu amemuelekeza kwamba dawa hiyo atakua anaingiza sehemu za siri kila siku kidonge kimoja na asishiriki tendo la ndoa, alishangaa kuona tena akimuelekeza kuvua nguo ili amuingizie dawa ambapo ametumia uume wake.

“Mimi tulivyofika na mume wangu mganga akaniita akanibonyeza tumbo akasema twende tukapime tumbo (Ultrasound) tulivyoleta majibu akasema nimsubiri chumba cha upasuaji alivyokuja akasema inabidi anipitishie dawa sehemu za siri, akasema nivue nguo nilale chini, nikavua nikalala ndio akanibaka huku amenibana mdomo,”amedai mwanamke huyo.

Mama mzazi wa mwathirika   amesema wakati akiwa nyumbani akapigiwa simu na mtoto wake akamuambia kwamba amebakwa wakati akipewa huduma katika hospitali ya wilaya, ambapo baada ya kufika hospitali kutoa taarifa akaahidiwa kuwa linafanyiwa kazi tukio hilo.

“Nimeumia sana moyoni kwa kweli kwa sababu mwanangu ameenda kupata huduma halafu mtoa huduma anambaka na tena mwanangu kaniambia amebakwa bila hata kutumia kinga na siku hizi kuna maradhi mengi.”

“Mpaka sasa mwanangu hana huduma aliyopata kutokana na tatizo lake kwani licha ya kuwa na uhitaji wa kushika mimba, tumbo lake linamuuma sana na ndio maana wakaenda hospitali yeye na mume wake ili kupata ufumbuzi. Japo  ufumbuzi waliopata ni kubakwa inaniuma sana,”amesema mama wa mwathirika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *