Dar es Salaam. Serikali imethibitisha pamoja na changamoto ya kupungua kwa ufadhili wa rasilimali za nje, upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs) upo kwa asilimia 100 ukiwezeshwa kwa fedha za ndani.

Aidha, dawa zilizopo kwa sasa na zile wanazotegemea kuzipokea ndani ya miezi sita ijayo, zitatosheleza matumizi kwa kipindi cha hadi Oktoba 2026.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Desemba Mosi 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge na Wenye Ulemavu), William Lukuvi wakati akitoa tamko la Siku ya Ukimwi Duniani yenye kaulimbiu isemayo,”Imarisha mwitikio, tokomeza Ukimwi”.

“Pamoja na kupungua kwa misaada yote Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake amejaza hilo pengo kwa fedha za ndani, ameanzisha Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (ATF), ambao amehakikisha anaweka mfumo endelevu wa uchangiaji na dawa zinapatikana kwa asilimia 100.

Amesema nchi itakuwa na akiba ya kutosha mpaka Oktoba 2026, tunaendelea kutoa dawa kwa kadri ya mipango inavyokwenda, akiondoa hofu iliyokuwepo na mashaka kwamba pengine kutokana na kupungua misaada dawa zingekosekana.

“Serikali imefidia gharama hizo zote na sasa huduma zinaendelea kama zilivyokuwa zimepangwa, tumeshirikiana na wadau wote kama fedha zimeokolewa kwenye sherehe za maadhimisho zitabaki kushughulikia afua za VVU Ukimwi, zitabaki ndani ya mfuko wa Serikali,” amesema.

Pia, Lukuvi amesisitiza huduma zitaendelea kutolewa bila gharama yoyote, akiwasihi waviu kuendelea kutumia huduma hizo kwa kuwa Serikali inatoa huduma bure, akitoa wito kwa wananchi kupima na kujikinga kwa kuepuka tabia hatarishi.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi amesema pamoja na changamoto ya kupungua kwa wafadhili wa nje katika utoaji wa rasilimali za mapambano dhidi ya Ukimwi, Serikali kupitia vyanzo vyake vya ndani imeweza kutoa kiasi cha Sh189 bilioni katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vitendanishi na usafirishaji wa sampuli za maabara.

“Kiasi hiki cha fedha kimechangia kufanya hali ya upatikanaji wa ARV kuwa asilimia 100 ambapo hakuna mteja aliyefika kituo cha kutolea huduma za afya na kukosa dawa. Aidha, dawa zilizopo kwa sasa na zile tunazotegemea kuzipokea ndani ya miezi sita ijayo, zitatosheleza matumizi kwa kipindi cha hadi Oktoba 2026,” amesema Dk Samizi.

Pia ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi wote wanaoendelea kupata huduma kwenye vituo vya afya, waendelee kufika katika vituo kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kuendelea kupata huduma, ambazo zinatolewa bila malipo yoyote.

Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), Leticia Moris ametoa shukurani na pongezi kwa Serikali kwa jitihada kubwa na sera madhubuti katika kusimamia uboreshaji wa huduma, upatikanaji wa dawa pamoja na mabadiliko ya sera.

“Waviu wote tumeendelea kupata tiba na matunzo bila kuathiri ubora wake ikiwemo upatikanaji wa ARV, tumekuwa tukipewa dawa kwa wakati, Nacopha tunaitaka jamii kutokuwa na hofu kwani dawa zipo za kutosha na zinapatikana,” amesema Leticia.

Pia Leticia ameiomba Serikali kuingiza teknolojia mpya za matibabu ikiwemo sindano za lenacapavir na upatikanaji wa chaguo zaidi za kinga zitakazosaidia kupunguza maambukizi mapya ya VVU na kutoa machaguzi zaidi kwa vijana.

Naye Kaimu wa Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania, Tacaids, Dk Samwel Sumba amesema zaidi ya watu milioni 1.5 wanaishi na maambukizi ya VVU nchini, hivyo taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na wadau wengine kuhakikisha wanaendeleza afua muhimu.

“Ili kukabiliana na athari za kupungua kwa fedha za ufadhili kwa mwaka wa fedha 2025/2026 mfuko wa ATF unatakiwa kukusanya Sh237 bilioni na kati ya hizi fedha asilimia 70 zitashughulikia VVU na asilimia 30 zitakwenda kwenye mfuko wa bima ya afya kwa wote,” amesema Dk Sumba.

Naye mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya Ukimwi (UNAIDs), Dk Grace Malya amesema licha ya kuendelea kupungua kwa vifo na maambukizi, hatua kubwa imepigwa lakini bado janga lipo na linaathiri wengi hususani vijana.

“Changamoto ya upungufu rasilimali fedha kidunia, iliongeza kwa kiasi kikubwa wasiwasi wa kupoteza mafanikio, tunaipongeza Tanzania imefanya mwitikio wa haraka wa kuongeza rasilimali za ndani kuhakikisha kunakuwa na mwendelezo wa mafanikio yake,” amesema.

Amesema ili kumaliza Ukimwi lazima uwekezaji ufanyike hasa eneo la kinga kwa wasichana wadogo na vijana balehe walio kwenye hatari zaidi ya maambukizi na kuendelea kuwezesha jamii ambayo ipo kwenye hatari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *