
Kibaha. Wasimamizi wa kemikali 170 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi katika Kanda ya Mashariki wameanza mafunzo ya siku tatu mjini Kibaha, mkoani Pwani.
Mafunzo haya yanakusudia kuongeza uelewa na kuimarisha usimamizi salama wa kemikali, ili kulinda afya za wananchi na mazingira, hasa ikizingatiwa ongezeko la kasi la matumizi ya kemikali nchini.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) Kanda ya Mashariki, na yanakuja wakati ambapo matukio ya madhara yanayotokana na matumizi yasiyo sahihi ya kemikali yanaendelea kuripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akifungua mafunzo hayo leo, Jumatatu Desemba 1, 2025, Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Afya, Rahimu Masombo amesema kuwa shughuli za kila siku za binadamu haziwezi kutenganishwa na matumizi ya kemikali, kwani ni nyenzo muhimu katika sekta nyingi za maendeleo.
Ameeleza kuwa kemikali hutumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa dawa za binadamu, uchujaji na utibuaji wa maji ya kunywa, pamoja na kutumika kama vitendanishi katika uchunguzi wa kimaabara.
Hata hivyo, Masombo ameonya kwamba matumizi yasiyo sahihi ya kemikali yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya na mazingira, baadhi yake yakijitokeza baada ya miaka mingi na wakati mwingine kuwa vigumu kubaini chanzo chake.
Masombo amewataka washiriki kusikiliza kwa makini na kuzingatia mada zote zitakazowasilishwa, ili kuongeza uelewa na kurejea katika maeneo yao ya kazi wakiwa na uwezo mkubwa zaidi wa kutoa huduma kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko, amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuongeza utaalamu na kuimarisha utendaji kwa wataalamu wa usimamizi wa kemikali, hususan katika kipindi hiki ambacho dunia inashuhudia ongezeko kubwa la matumizi ya kemikali katika sekta mbalimbali.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Frank Mwanjisi, amesema anaamini kuwa yatamjengea uelewa mpana na kumsaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa mwaka 2016 unaonyesha kuwa takribani vifo milioni 13.7 vilihusishwa na athari za kemikali, ikiwa ni sawa na asilimia 24 ya vifo vyote duniani.
Aidha, utafiti huo unaonesha kuwa athari za kemikali zilichangia asilimia 23 ya mzigo wa magonjwa duniani.
WHO inakadiria kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi, kwani uzalishaji wa kemikali duniani unatarajiwa kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2050 mwenendo unaoongeza umuhimu wa kuwa na mifumo madhubuti ya usimamizi wa kemikali, hususan katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.