
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imewataka mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya kuchunguza chanzo matukio ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 uliofanyika Oktoba 29, kuhudhuria shauri linalowakabili kesho.
Wajumbe wa tume hiyo wameitwa mahakamani hapo kesho Jumanne, Desemba 2, 2025 kufuatia shauri la maombi namba 30210 ya mwaka 2025, lililofunguliwa dhidi yao la kibali cha kupinga uhalali wake.
Kwa mujibu wa hati ya taarifa kutajwa kwa shauri hilo, iliyosainiwa na kutolewa leo Jumatatu, Desemba Mosi, 2025 na Naibu Msajili, kwenda kwa wajumbe wa tume hiyo ambao ni wajibu maombi katika shauri hilo, limepangwa kusikilizwa na Jaji Hussein Mtembwa.
“Tambua kuwa kesi tajwa hapo imepangwa kutajwa Desemba 2, 2025, saa 3:00, mbele ya Mheshimiwa H.S. Mtembwa. Unatakiwa kuhudhuria bila kukosa kwa njia ya mtandao na unapaswa kuwasilisha nyaraka zote unazokusudia kuzitumia katika kesi yako,” inasomeka taarifa hiyo kwenda kwa wajibu maombi.
Tume hiyo inayoongozwa Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Othman Chande iliundwa na kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Novemba 20, 2025.
Oktoba 29, 2025, makundi ya vijana walioanza kuhamasishana mitandaoni kuandamana siku hiyo kupinga uchaguzi huo, waliingia barabarani na mitaani katika majiji na miji mbalimbali nchini.
Hatua hiyo ilisababisha vurugu na uharibifu wa miundombinu na mali za umma na za watu binafsi na zaidi vifo vya watu kadhaa.
Hata hivyo, siku chache tu baada ya Rais Samia kuunda na kuzindua tume hiyo kuchunguza matukio hayo, imeburutwa mahakamani baada ya kufunguliwa shauri la maombi ya kibali cha kuipinga.
Shauri hilo limefunguliwa na watetezi wa haki za binadamu, Rosemary Mwakitwange na mawakili wawili Edward Heche na Deogratius Majinyila, wakiomba kibali cha mahakama kufungua shauri la kupinga uamuzi na hatua hiyo ya Rais Samia kuunda tume hiyo; kwa utaratibu wa maombi ya mapitio ya mahakama (judicial review).
Wajibu maombi katika shauri hilo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambaye ni mjibu maombi wa kwanza na mwenyekiti na wajumbe wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu, Chande (mwenyekiti) ambaye ni mjibu maombi wa pili.
Wajumbe wengine wa tume hiyo ambao pia ni wajibu maombi katika shauri hilo ni Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue; Radhia Msuya, Balozi Paul Meela na Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu (IGP), Said Mwema.
Wengine ni Balozi David Kapya, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Africa (SADC) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mstaafu, Stergomena Tax.
Shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura ambapo mawakili wa waombaji hao ni Mpale Mpoki, Jebra Kambole, na Hekima Mwasipu.
Mawakili hao wanadai shauri hilo lina udharura mkubwa kwa kuwa kama halitasikilizwa haraka, wajibu maombi (tume hiyo) wataendelea na uchunguzi ambao uundwaji wake, uteuzi na wajumbe wake hauna mantiki, umefanywa kwa nia ovu na ni kinyume cha sheria.
“Zaidi ya hayo, uchunguzi huo unakiuka misingi ya haki ya asili, hususan kanuni ya nemo judex in causa sua (mtu hawezi kuwa hakimu wa kesi yake mwenyewe),” wanasema mawakili hao kuhusiana na udharura wa shauri hilo.
“Umma, ambao una masilahi halali ya kujua sababu halisi na kiwango cha vurugu za wakati na baada ya uchaguzi, utaathirika endapo amri zinazotafutwa hazitasikilizwa na kuamuliwa haraka.”
Katika hati ya maombi, waombaji hao wanaiomba Mahakama hiyo iwape kibali cha kupinga uteuzi wa kamati hiyo, kwa kufungua shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama kuomba amri za kufuta na zuio la uamuzi wa Rais wa uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo.
Wanahoji uhalali wa uteuzi huo, wakidai ulifanywa kwa nia ovu kinyume cha kanuni hiyo ya haki asili.
Pia, wanaomba utolewaji wa kibali hicho utumike kama amri ya kusitisha uendeshwaji wa uchunguzi wa tume hiyo hadi shauri watakalolifungua kuipinga tume hiyo, kama watapewa kibali hicho, litakaposikilizwa na kuamuliwa.
Katika kiapo chao cha pamoja na hati ya maelezo yao, waombaji hao, wanajitambulisha kuwa wao ni wanajamii wazalendo.
Wanadai kama raia, wanatamani kufahamishwa na kupata ufafanuzi kamili kuhusu masuala yote yanayohusiana na ghasia zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 kwa kuwa wana masilahi katika hilo.
Mambo hayo ni pamoja na ukamatwaji kiholela wa watu, kuwekwa kizuizini, ukatili, kutendewa mabaya, watu kupotea, na miili ya watu waliouawa kwa kile kilichoitwa uvunjifu wa amani.
Katika kiapo hicho waombaji hao waombaji hao wanadai TLS ni Chama cha Wanasheria Tanganyika, kilichoundwa mwaka 1954 kwa Sheria ya Bunge.
Wanafafanua majukumu ya msingi ya TLS ni kukuza utawala wa sheria, uadilifu na uwazi, kulinda na kusaidia umma kupata haki na huduma za kisheria katika masuala yote yanayohusiana na sheria.
Wanadai kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchunguzi, Sura 32 Marejeo 2023, inamwezesha Rais kuunda, kuanzisha na kuteua tume za uchunguzi, haijaruhusu kutumia neno ‘tume huru.’
“Mamlaka ya uteuzi ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, chama tawala, kilichoshiriki na kushinda uchaguzi uliosababisha ghasia wakati na baada ya uchaguzi, na kwa hivyo kina masilahi katika uchaguzi huo na tume hiyo,” wanadai waombaji hao.
Wanadai masharti ya Sheria ya Tume ya Uchunguzi yanataka mamlaka ya uteuzi kufafanua madhumuni ya kuundwa kwa tume.
Hata hivyo, wanadai tume hiyo aliyoiunda Rais imeundwa kinyume na sharti la kifungu cha 16 cha sheria hiyo, kwa kuwa haifafanui madhumuni yake na haijatangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali, kama Sheria inavyohitaji.
“Madhumuni ya Tume ya Uchunguzi, kama yalivyo kwenye taarifa kwa umma yenye kichwa, “Kuchunguza Uvunjifu wa Amani” hayana ufafanuzi, hayajulikani na yanategemea hisia tu, kinyume na misingi ya Katiba, utawala bora na utaratibu sahihi wa haki, hivyo yanastahili mapitio ya Mahakama,” wanaeleza.
Wanadai mamlaka ya uteuzi imeteua wajumbe wa tume wenye mkinzano mkubwa na hawawezi kuchunguza kwa haki matendo yaliyosababisha ghasia zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi, ambayo yamefichwa chini ya jina la uvunjifu wa amani.
Wanafafanua uteuzi wa tume hiyo haujajumuisha wajumbe, vyama huru vya kitaaluma Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), chama cha madaktari, mashirika ya kijamii, ya kidini au wadau wengine huru, hivyo kuweka hatari kubwa kwa uhuru wa tume.
Badala yake wanadai wajumbe wote ni watumishi wa umma waliostaafu, waliokuwa na nafasi za kuteuliwa na Rais, waliokula kiapo cha siri kwa Rais, ambacho hakijafutwa wakati wa kustaafu au hadi tarehe ya uteuzi kama wajumbe wa tume inayopingwa.
Hivyo, wanadai wajumbe hao hawawezi kuchunguza mamlaka ya uteuzi wao ambaye pia ni mtumishi wa umma (na baadhi ya malalamiko yanahusu tabia yake), na pia watumishi waliostaafu hawawezi kuchunguza tabia za watumishi wa sasa.
Hivyo, wanadai uteuzi huo haukubaliki kwa sababu mamlaka ya uteuzi haikuzingatia masilahi ya umma.
Wanafafanua masilahi hayo ya umma yanadai uteuzi wa wajumbe huru kutokana na ushawishi wowote wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja wa Serikali, wasio na mgongano wa masilahi, kuepuka upendeleo kwa masuala yanayohusiana na mamlaka ya uteuzi.
“Uteuzi huo haukubaliki kwa sababu una msukumo usioeleweka, kwani umepunguza umuhimu wa madhara makubwa, yaani vifo, watu waliopotea na matendo mabaya na ya kikatili, ukilinganisha na jina la uvunjifu wa amani,” wanaongeza waombaji na kusisitiza:
“Kwa hivyo, uteuzi wa Tume ya Uchunguzi unaanza kwa dhana ya awali isiyo sahihi, kwani neno ‘Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani’ linapunguza na kudharau vifo, watu waliopotea, miili iliyopotea, majeraha na athari kubwa kwa umma kwa jumla.”
Wanadai baadhi ya wajumbe ni watuhumiwa mfano Tax ambaye wanaeleza alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati ghasia za uchaguzi zilipotokea, alihusika kwa namna moja au nyingine chini ya wizara yake.
Wanafafanua zaidi wajumbe wawili ambao ni majaji wakuu wastaafu hawawezi kuchunguza kwa haki vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi na baada yake, kwani baadhi ya mali zilizoharibiwa zilikuwa ni mali ya Mahakama waliyoiongoza.
Vilevile wanadai IGP mstaafu hawezi kumchunguza kwa haki, kwa kuwa, IGP aliyepo anaweza kuwa miongoni mwa watuhumiwa.
Wanasisitiza wajumbe wa tume ambao ni watumishi wa umma wastaafu, waliowahi kuteuliwa na mamlaka ya uteuzi wao na wanaostahili pensheni, hawawezi kumchunguza mamlaka ya uteuzi ambaye ndiye mkuu wa utumishi wa umma aliyepo madarakani.