Tunapaswa kuchagua amani, si uchocheziTunapaswa kuchagua amani, si uchochezi

KAULI ya Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba kuwataka Watanzania wakatae kushawishiwa na wanaharakati wanaochochea vurugu si kauli ya kawaida. Ni kauli iliyobeba uzito wa hali halisi ya dunia na mazingira yetu ya sasa, kwani taarifa, mitazamo na propaganda husambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii na hata mikusanyiko ya jamii.

Katika mazingira haya, kila raia anapaswa kuwa na uwezo wa kutofautisha kati ya uhuru wa kutoa maoni unaolenga kujenga, na uchochezi unaolenga kubomoa msingi wa utulivu wa kitaifa. Kwa nukuu yake, “Nimekuja kuwapa pole wananchi wenzangu… Rais Samia anatambua mambo yanayoendelea,” ujumbe huu unaonesha wazi kuwa serikali inafuatilia kwa karibu hisia, changamoto na maoni ya wananchi.

Hii inaonesha kuwa uongozi wa juu unatambua kwamba si kila kelele ni uasi, bali nyingine ni kilio cha wananchi kutaka kusikilizwa. Pamoja na hilo, anasisitiza kuwa ndani ya maoni hayo kuna kundi dogo la watu wanaotumia changamoto hizo kuhamasisha vurugu, na hilo ndilo linalopaswa kukataliwa kwa nguvu zote.

Ni muhimu kama taifa kutambua tofauti kati ya wanaharakati wanaotoa hoja za kujenga na wale wanaochochea mgawanyiko. Tanzania imekuwa na historia ndefu ya watu wanaopigania haki, maendeleo na uwajibikaji na hawa wana mchango mkubwa katika ustawi wa demokrasia.

Lakini pale harakati zinapogeuzwa kuwa jukwaa la kuchochea chuki, kuvuruga utulivu na kupanda mbegu za mashaka, hapo ndipo wananchi wanapopaswa kuwa makini kwa sababu vurugu, kwa namna yoyote ile, huwa hazitoi majibu, hazijengi bali zinabomoa.

Historia duniani inadhihirisha hilo kwa sababu yapo mataifa yaliyokumbwa na migogoro ya ndani mara nyingi hujikuta yakipoteza uwekezaji, kushuka kiuchumi, kushindwa kutekeleza mipango ya maendeleo, na wananchi ndiyo huteseka zaidi.

Najua tunajua kama Tanzania imebarikiwa utulivu ambao nchi nyingi zingetamani kuwa nao na ndiyo maana hoja ya Waziri Mkuu inapaswa kuangaliwa ndani ya sura hiyo pana si kama onyo la kisiasa, bali kama tahadhari ya kitaifa. SOMA: Viongozi wa dini wasisitizwa kuomba amani, utulivu

Hata hivyo, amani si kutokuwapo kwa migogoro pekee bali ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanasikilizwa, uongozi unawajibika, changamoto zinajibiwa, na haki inatendeka. Ile kauli ya ‘mkatae uchochezi’ iwe na nguvu lazima pia kuwe na mazingira yanayowapa wananchi uhuru salama wa kueleza changamoto zao bila kuonekana kama wapinzani wa nchi.

Hili ndilo litazidisha imani, litazidisha umoja, na kupunguza nafasi ya watu wachache kupenyeza mbegu za migogoro. Kipitia kauli yake ya kuwa serikali iko tayari kuwasikiliza ni msingi muhimu wa kujenga maridhiano na kuzuia watu wanaotumia silaha ya maneno kupotosha au kuchochea taharuki.

Wananchi wanapojua kuwa serikali inajali na inafanya jitihada kutatua changamoto zao, huwa vigumu kwa mtu kuwapotosha kwa maneno ya haraka haraka. Hivyo basi, ni wajibu wa wananchi nao kuhakikisha wanachukua hatua za kuilinda amani kwa kuepuka kusambaza taarifa zisizothibitishwa, kutofanya maamuzi kwa misukumo ya hasira, kutafuta taarifa sahihi kutoka vyanzo vya kuaminika, kukataa kushiriki maandamano, mikusanyiko au mijadala inayolenga kuvuruga hali ya nchi na kujenga utamaduni wa kuzungumza kwa hoja, si kwa jazba.

Natambua jitihada za serikali katika kuimarisha na kulinda amani lakini nashauri iendelea kuimarisha mifumo ya ushirikishwaji, uwajibikaji na mawasiliano ya wazi.Wananchi wanapokosa majibu au wanapohisi kama hawasikilizwi, ndipo pengo linalotumiwa na wachochezi huzaliwa.

Mambo kama hayo hupunguza urasimu, kuongeza uwazi katika maamuzi ya kitaifa, kuboresha ustawi wa kijamii, na kuimarisha haki za wananchi vitasaidia zaidi kuinua imani kwa serikali na kudhibiti uchochezi.

Ni rahisi kudhani kuwa amani ni jukumu la viongozi pekee, lakini kwa kweli amani ni kazi ya kila mtu kuanzia raia wa kawaida, kijana, mwanaharakati, mwanasiasa, kiongozi wa dini na hata mtaalamu mwenye taaluma, hivyo tunapochagua kuheshimiana, kusikilizana, kutoa hoja bila kuchochea chuki, basi tunachagua kulinda mustakabali wa vizazi vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *