Tunapodai haki, tukumbuke wajibu wa kutii sheriaTunapodai haki, tukumbuke wajibu wa kutii sheria

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera amesema haki lazima iendane na wajibu kwa hiyo ni lazima watu watimize wajibu kwa kutii sheria za nchi na walinde amani na mshikamano wa Taifa. Akipokea taarifa ya maendeleo ya Wilaya ya Namtumbo, Dk Homera alisema Watanzania hawana taifa lingine zaidi ya Tanzania, hivyo wanapaswa kutekeleza sheria za nchi.

Tunakubaliana na kauli hiyo ya Dk Homera kuwa haki inakwenda na wajibu na moja ya wajibu ni kutii sheria za nchi na kanuni zake. Tunachofahamu katika msingi wa taifa lolote lenye amani na mshikamano, utawala wa sheria unachukua nafasi ya pekee na Tanzania ikiwa na historia ya kudumisha umoja na utulivu, inategemea sana uelewa na utiifu wa wananchi kwa sheria zilizowekwa.

Sheria za nchi ni dira inayolenga kuongoza mwenendo wa wananchi na taasisi, hivyo zinapoheshimiwa, kila mmoja anapata haki yake kwa usawa na bila upendeleo. SOMA: Tunapaswa kuchagua amani, si uchochezi

Ni ukweli usiokuwa na mashaka mwananchi anayefuata taratibu za kisheria anakuwa na nafasi pana ya kusikilizwa, kutetewa na kupata haki bila vikwazo, lakini kinyume chake, yaani kutokuzingatia sheria huzaa vurugu, migogoro, ucheleweshaji wa haki na mifumo dhaifu isiyoweza kulinda maslahi ya wote.

Ni muhimu kukumbuka kuwa haki na wajibu ni pande mbili za sarafu moja. Tunapenda kuikumbusha jamii kuwa haiwezekani kudai haki bila kutimiza wajibu wa msingi wa kuzingatia sheria. Mwananchi unapotekeleza wajibu wako wa kutii sheria, unajenga misingi imara ya utawala bora na kuzilinda taasisi zinazopaswa kuwahudumia.

Hata hivyo, jukumu la utekelezaji wa sheria halipaswi kuwa la wananchi peke yake, kwani serikali nayo ina wajibu wa kusimamia sheria kwa haki, kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha mifumo ya utoaji haki haibagui mtu yeyote.

Pale ambapo sheria zinatendeka bila upendeleo, wananchi huongeza imani yao katika serikali na utawala. Ndivyo inavyotakiwa pia kwa Tanzania kuhakikisha inaendeleza utamaduni wa kuheshimu sheria kama njia ya kujenga jamii yenye haki, amani na ustawi.

Kutii sheria si kikwazo, bali ni nguzo inayolinda haki za kila mmoja, ni wajibu wa kila Mtanzania kutambua kwamba ustawi wa taifa letu unategemea utiifu wetu kwa sheria na taratibu tulizojiwekea. Tunaamini kuwa kwa kutii sheria, tunajihakikishia haki na kwa kuheshimu wajibu, tunajenga Tanzania bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *