Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Othman Chande amesema anajua utendaji wa tume hiyo utapimwa kitaifa na kimataifa, hivyo imejikita kuzingatia Watanzania wanataka nini.
Miongoni mwa mambo waliyobaini amesema Watanzania wanataka uchunguzi ufanyike kikamilifu, uwazi na ushahidi utakaochukuliwa uwe unaotumika iwapo italazimika kufikia hatua hiyo katika muhimili wa kisheria.
Hiyo ni kauli ya kwanza kwa tume hiyo yenye wajumbe tisa, tangu ilipoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuanza kazi Novemba 20, mwaka huu.
Hata hivyo, kuundwa kwa tume hiyo kuliibua upinzani, baadhi wakiipinga kwa kile walichosema, haitakuwa huru hasa pale itakapolazimika kuichunguza mamlaka iliyoiteuwa kwa kuwa kutakuwa na mgongano wa masilahi.
Baadhi ya wanaopinga tume hiyo wamefungua shauri Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Dar es Salaam kupinga uhalali wake kwa hoja kuwa, uteuzi wa wajumbe wake umekiuka haki ya asili.
Shauri hilo la madai mchanganyiko litakalosikilizwa kesho Jumanne, Desemba 2, 2025 lilifunguliwa Novemba 26, 2025 mahakamani hapo na mwanaharakati Rose Mwakitwange na mawakili wa Mahakama Kuu na Mahakama za chini, Edward Heche na Deogratius Mahinyila.
Mahakama hiyo imewataka mwenyekiti na wajumbe wa tume hiyo kuhudhuria shauri linalowakabili.
Kwa mujibu wa hati ya taarifa, shauri hilo lililosainiwa na kutolewa leo Jumatatu, Desemba mosi, 2025 na Naibu Msajili kwenda kwa wajumbe wa tume hiyo, ambao ni wajibu maombi katika shauri hilo, limepangwa kusikilizwa na Jaji Hussein Mtembwa.
“Tambua kuwa kesi tajwa hapo imepangwa kutajwa Desemba 2, 2025, saa 3:00, mbele ya Mheshimiwa H.S. Mtembwa. Unatakiwa kuhudhuria bila kukosa kwa njia ya mtandao na unapaswa kuwasilisha nyaraka zote unazokusudia kuzitumia katika kesi yako,” inasomeka taarifa hiyo kwenda kwa wajibu maombi.
Kuundwa kwa tume hiyo, kumetokana na tukio la maandamano yaliyosababisha vurugu wakati na baada ya Oktoba 29, mwaka huu na kusababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa biashara, mali za watu binafsi na miundombinu ya umma.
Leo, Jumatatu Desemba mosi, 2025 jijini Dar es Salaam, Jaji Chande amekutana na wahariri na waandishi kwa mara ya kwanza tangu kuzinduliwa kwa tume hiyo. Amesema ni dhamira yake na wajumbe wa tume hiyo kufanya kazi kikamilifu, kwa viwango kwa kuwa anajua watapimwa kwa utendaji kutoka ndani na nje ya nchi.
“Tunataka tufanye kazi kikamilifu, kwa kiwango kwa sababu tunajua tutapimwa kwa viwango, ndani na nje ya nchi, hiyo tunajua. Tusipimwe kabla hatujaanza mtihani, tufanye mtihani mtupe maksi,” amesema.
Kwa sababu hiyo, amesema kabla ya kuanza kazi, wameanza kuangalia Watanzania wanataka nini kutoka kwa tume hiyo ili wayazingatie wakati wa utendaji wao.
Katika mambo waliyobaini wananchi wanataka, amesema ni uchunguzi wa kina usiishie nusu, uwazi na ushahidi utakaochukuliwa uwe ule utakaoweza kutumika katika mamlaka za kisheria.
“Kabla hatujaanza kazi kwanza sisi wenyewe tumejiangalia, wenzetu wanataka nini. Tumebaini watu wanataka uchunguzi kamilifu, usifanyike nusunusu, wanataka uwazi kwenye kazi na kama utachukuliwa ushahidi uwe utakaotumika sio ambao hauwezi kutumika,” amesema Jaji Chande.
Sambamba na hilo, Jaji Chande amesema wajumbe wote wa tume hiyo wamekula kiapo, hivyo iko huru na wanaanza kufanya kazi bila shinikizo la yeyote na utendaji wao utajikita kwenye hadidu za rejea na ushahidi utakaowaridhisha.
“Lakini lingine muelewe tume hii ya kisheria wote tumekula kiapo, kwa hiyo inathibitisha uhuru wetu, ndio maana nimesema tunaanza kazi bila shinikizo la mtu yeyote na tunajikita kwenye ushahidi tutakaoridhika nao, halafu ripoti yetu itaonesha,” amesema.
Amesema itakapobainika mmoja wa wajumbe ana mgongano wa masilahi na anapaswa kuchunguzwa na tume, ataombwa kujiondoa au mwenyewe atalazimika kujiondoa katika nafasi yake, kupisha uchunguzi.
Amependekeza ripoti ipatikane kwa umma hasa kwa jambo linalowahusu, ingawa kwa kawaida hiyo ni nyaraka ya mamlaka nyingine.
Kuhusu kauli za viongozi
Jaji Chande amesema wanasikia kauli za viongozi kuhusu sababu za vurugu hizo, lakini wanajikita katika hadidu za rejea na hadi sasa hawana amri ya yeyote na hawana ushahidi, hivyo wanaanza kazi bila kuwa na chochote.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa Amani kabla na baada ya Uchaguzi, Jaji Mohamed Othman Chande akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.
“Najua kuna kauli hizi zinatolewa za hivi na vile na hisia mbalimbali, lakini tusiwe na wasiwasi,” amesema.
Alipoulizwa umri wa wajumbe, amekiri wana umri mkubwa, lakini unaendana na uzoefu na watakuwa na mbinu mbalimbali za kuwashirikisha vijana wa matabaka yote.
Hata hivyo, amesema sheria ya tume hiyo na nyingine zote za uchunguzi katika nchi za jumuiya ya madola, zinasema mamlaka ya kuunda tume ni ya Rais wa nchi husika.
Amesema tofauti na mataifa kama Afrika Kusini na Kenya, jambo hilo lipo kwenye katiba, lakini kwa Tanzania ipo kwenye sheria.
Hadidu za rejea
Kuhusu hadidu za rejea, amezitaja ni kuchunguza na kubaini chanzo cha msingi cha matukio hayo, wakati na baada ya uchaguzi na kuchunguza lengo lililokusudiwa walioshiriki matukio hayo.
Lingine, amesema watachunguza na kubainisha madhara yaliyojitokeza, ikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na miundombinu na madhara ya kiuchumi na kijamii.
Pia, amesema ni kuchunguza mazingira na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali na vyombo vyake na taasisi katika kubaini na kukabiliana na yaliyotokea.
Jukumu lingine, amesema ni kupendekeza maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi ili kuongeza uwajibikaji na utawala wa raia wenye kuzingatia haki za binadamu, majadiliano ya kisiasa, hadi kufikia maridhiano ya kitaifa.
Amesema tume hiyo pia itachunguza jambo lolote ambalo itaona ni muhimu na linaendana na majukumu yake.
“Kuna ile namba sita akiba kama tunaona jambo linahusiana, basi tume imepewa uhuru wa kusema na hili pia tunashughulika nalo, hatuna haja ya kibali cha mtu mwingine yeyote,” amesema.
Jaji Chande amesema tume hiyo pia ipo huru kutafsiri hadidu za rejea na katika kutekeleza majukumu yake itazingatia sheria ya tume na mamlaka waliyopewa kisheria.
Mamlaka ya tume
Jaji Chande amesema tume kama hizo huwa na mwenendo wa kimahakama kwa kuwa, mtu anapotoa ushahidi anaapa ili baadaye utumike.
Pia, amesema tume hizo huwa huru kuandaa taratibu zake na hazifuati ufundi kama ilivyo katika Mahakama na ina mamlaka ya kutoa wito.
“Pamoja na tume kuomba ushirikiano, lakini ina mamlaka ya kushurutisha ushirikiano, lakini sisi hatwendi huko,” amesema Jaji Chande.
Katika utekelezaji wa shughuli zao, amesema watatumia njia za mapitio ya uchambuzi wa nyaraka mbalimbali, mahojiano ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandaoni, dodoso la mtandaoni, baruapepe, barua za kawaida, kutembelea uwandani, ushauri wa kitaalamu, mijadala ya makundi mbalimbali, simu na jumbe fupi za maandishi.
Kwa upande wa wadau watakaokutana nao, amesema ni waathirika kwa sababu tume imejikita kuponya, hivyo hao ni wadau muhimu.
Pia, amewataka watuhumiwa walioshiriki matukio hayo kuwa wao hawana mamlaka ya kijinai hawatamshitaki mtu.
Makundi mengine, amesema ni vyama vya siasa, asasi za kiraia, wasimamizi wa uchaguzi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), viongozi wa dini, bodaboda, machinga, wafanyabiashara na wajariamali, washirika wa maendeleo, serikali za mitaa, vijiji na kata, vyombo vya ulinzi na usalama, sekta binafsi, wanahabari, watafiti, wataalamu wa sekta na fani mbalimbali.
“Kusema kweli ni kwamba, pamoja na uchungu mkubwa uliotupata, majibu ya mambo mengi, karibu yote, tunayo sisi wenyewe, tusaidiane tu, kujibu hadidu za rejea kwa umakini, basi ndio utakuwa msingi wa mijadala ya mbele, tunakwenda wapi, tunamuwajibisha nani, kwanini na kwa muda gani,” amesema.
Ameeleza katika utendaji wao wanatarajia kupata ushirikiano kutoka kwa makundi yote na ingawa wanatambua kuna wale wasiotaka kutoa ushirikiano, watawaomba hata mara tatu itakapobidi.
“Sio jambo la ajabu, watu kutoshirikiana na tume za uchunguzi za aina hii, kwani nimeshafanya kazi katika tume nyingi. Hapa watabembelezwa na wataombwa na kwamba hatuendi kuwashurutishana kwa kuwa, wana nafasi kubwa na kwa kuwa hatuangalii yaliyotokea tu bali safari ya tunakokwenda,” amesema.
Amesema katika utendaji wao, watalazimika kurudi nyuma ili kupata kiini halisi cha tatizo, huku akidokeza iwapo Desemba 9 kutatokea tukio kama hilo na tume ikaona linaendana na uchunguzi wake, litajumuishwa.
Akizungumzia hilo, mchambuzi wa siasa, Said Majjid amesema ni muhimu yaliyosemwa yaendane na utendaji wa tume husika, akisisitiza itaongeza imani ya wananchi kwa nyingine zitakazoundwa.
“Shida ya wengi ni hofu kuwa tume itakuwa na mgongano wa kimasilahi. Ni wajibu wa tume yenyewe kulifuta hili kwa kuhakikisha inasimama imara na inatenda haki na inaonesha uhuru,” amesema.
Amesisitiza yaliyosemwa na Jaji Chande ni mazuri na sahihi, muhimu ni kuzingatiwa na kutekelezwa wakati wa utendaji wa tume husika.