Dar es Salaam. Tatizo la Usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya dawa (Uvida) linazidi kukua nchini, huku takwimu zikionesha mwaka 2021 lilisababisha vifo vya watu 42,196.
Idadi hiyo ya watu walifariki dunia baada ya dawa kushindwa kuwatibu, kutokana na vimelea vya magonjwa waliyokuwa nayo kuwa na usugu dhidi ya dawa zilizotumika kuwatibu.
Akizungumza katika mafunzo maalumu yaliyotolewa na Serikali kwa wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari Novemba 30, 2025 mdau wa Usugu wa Vimelea vya Magonjwa (AMR), Siana Mapunjo amesema idadi hiyo ni kati ya watu 236,128 waliopata tatizo la maambukizi katika damu lijulikanalo kama Sepsis.
Amesema idadi hiyo ni kati ya wale waliofanyiwa uchunguzi kupitia maabara zenye uwezo wa kupima ufanisi wa dawa kimatibabu.
“Kati ya watu 236,128 waliougua tatizo la maambukizi kwenye damu 70,251 walipata maambukizi ya bakteria katika damu, 42,196 walifariki kwa tatizo lililothibitishwa moja kwa moja na usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.
“Wengine 9,231 walifariki kwa maambukizi yanayosababishwa na vimelea (bakteria, virusi, fangasi au parasiti) ambavyo havijibu tena matibabu ya kawaida ya dawa, kwa sababu vimelea hivyo vimejenga usugu,” amesema.
Amesema kwa sasa nchini watu wamekuwa wakitumia mpango wa mwaka 2023/28 kupambana na Uvida na tangu kuanza kwa mapambano hayo mwaka 2017, changamoto kadhaa wanapambana nazo ikiwamo uwezo wa maabara kubaini bado ni chache.
Pamoja na hayo, amesema rasilimali fedha bado ni changamoto kubwa.
“Tatizo bado ni kubwa kuna watu wengi wanafariki kutokana na dawa kushindwa kufanya kazi,” amesema Mapunjo.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Afya Bugando-Cuhas, Profesa Jeremiah Semi amesema Tanzania ina maabara zenye uwezo wa kubaini usugu wa vimelea dhidi ya dawa katika ngazi zote za juu, kanda na hospitali za rufaa za mikoa.
“Maabara tunazo zenye uwezo wa kupima vimelea na kubaini ni wa aina gani na kwa dawa mbalimbali kubaini usugu kwenye hospitali zote za rufaa za kanda saba na maalumu za mikoa, zina uwezo wa kupima hawa vimelea na sasa tunaenda mpaka ngazi za chini kwa maana ya hospitali za wilaya,” amesema Profesa Semi.
Amesema kipimo hicho kinahitaji fedha na uwekezaji mkubwa, hivyo Serikali imedhamiria kushusha kipimo hicho mpaka ngazi za hospitali za wilaya.
Pia, amesema kwa sasa kuna hospitali 10 zinazotekeleza mpango mkakati wa ufuatiliaji wa Uvida, tangu mwaka 2020 walianza na wagonjwa 9,000 na kufikia mwaka jana wamefanya ufuatiliaji kwa wagonjwa 49,000 kwa mwaka 2024 pekee.
Kufuatia mafunzo maalumu yaliyotolewa na Serikali kwa vyombo vya habari, wananchi nchini wanatarajiwa kunufaika na taarifa sahihi kuhusu matumizi ya dawa, hatua inayotarajiwa kusaidia kupunguza vifo vinavyotokana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Afya Moja, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Salum Manyata amesema ili kupambana na changamoto hizo, sekta ya afya inapaswa kuungana na nyingine ili kuhakikisha wanalinda usalama wa afya.
“Sekta zote lazima zishirikiane, na kuhakikisha kwamba tunawasiliana mfano kuna changamoto ya ugonjwa fulani kama brusela unaoathiri kupitia maziwa lazima wawaambie wenzao sekta ya afya ili kupambana na changamoto hiyo,” amesema.
Yanayochangia Uvida
Dk Manyata amesema matumizi holela ya dawa za antibaotiki ni changamoto kubwa inachangia tatizo hilo.
Ametaja matumizi mabaya na kupindukia ya dawa, kuchukua antibiotiki bila ushauri wa daktari, kuanza dawa na kuziacha kabla ya muda uliopendekezwa.
Pia, ametaja kutoa dawa kwa magonjwa ambayo hayahitaji antibiotiki, kama mafua ya kawaida (virusi) na kumeza dawa za mgonjwa mwingine au kutumia dawa zilizobaki.
“Chanzo kingine cha tatizo hili ni kutotumia dawa sahihi kwa kiwango sahihi, kuchagua aina ya antibiotiki isiyoendana na maambukizi na kipimo (dose) au kuwa kidogo mno au muda wa matibabu kuwa mfupi,” amesema.
Mbali na hayo, hatua ya baadhi ya wagonjwa kuacha dawa pindi wanapohisi nafuu imeendelea kuongeza changamoto hiyo.
“Unapoacha dozi nusu, bakteria wanaobaki wanakuwa na uwezo wa kuhimili dawa mara inayofuata. Hapo ndipo usugu unapoanza,” ameeleza.
Sekta ya mifugo imepewa pia lawama. Wataalamu wanasema matumizi ya antibiotiki kwa wingi kwenye kuku, ng’ombe na samaki ili kuongeza uzalishaji huibua vimelea sugu vinavyoweza kuhamia kwa binadamu kupitia chakula au mazingira.
Zaidi ya hayo, dawa bandia na duni zinazouzwa kwenye baadhi ya maduka yasiyosajiliwa zimeendelea kuongeza mzigo wa usugu wa dawa nchini. Wataalamu wanatoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanapata dawa katika vituo vinavyotambuliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Hospitali nazo haziko salama. Ripoti zinaonesha kuwa kutofuata kikamilifu taratibu za usafi kama kunawa mikono, kutumia glavu na kusafisha vifaa, huongeza kasi ya kusambaa kwa vimelea sugu miongoni mwa wagonjwa.
Wataalamu wanasisitiza kuwa, hatua madhubuti zinahitajika ili kulinda tiba zilizopo.
Wananchi wanahimizwa kutojipa dawa kiholela, kukamilisha dozi wanazopewa, na kuzingatia usafi wa mikono na mazingira.
“Tusipochukua hatua leo, tutakuja kuishi katika dunia ambayo hata maambukizi madogo hayatibiki. Hili si jambo la kutishwa ni uhalisia unaotukabili, hata hivyo tutaingia gharama za kutengeneza dawa zingine,” amesema Dk Manyata.
Serikali inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa maambukizi sugu, kuweka sheria kali kwa matumizi ya dawa na kuhamasisha tafiti zaidi ili kubaini ukubwa wa tatizo nchini.