Pooja, ungependa kutushirikisha safari yako? Tuambie hadithi ya maisha yako

Hadithi yangu inaanzia nilipokuwa na miaka 15, nilipoolewa kwa ndoa ya kupandwa na familia. Baada ya miaka miwili ya ndoa nikiwa na miaka 17 ndipo nilipogundua kuwa nina VVU. Nilianza dawa za ART nikiwa na umri wa miaka 19. Kipindi hicho kilikuwa kigumu sana kutokana na umri wangu, na wakati ule hakukuwa na msaada mzuri wala harakati mahsusi za vijana.

Baba yangu alikuwa kwenye jeshi, na familia yetu ilikuwa na hamasa sana kuhusu masuala ya ulinzi tangu nikiwa mdogo. Nami nilikuwa na ndoto hiyo niliendelea na maandalizi yangu hata baada ya ndoa. Lakini habari za VVU zilipokuja ghafla, zilikuwa mshtuko ambao mpaka leo hatuwezi hata kuuelezea vizuri. Sikuwahi hata kufikiria kitu kama hicho kingeweza kunitokea.

Hali iliathiri sana afya yangu ya akili. Kwa miaka miwili sikupata dawa za ART, na kwa sababu hiyo afya yangu ilizidi kudhoofika. Nilikuwa dhaifu kimwili na kiakili.

Baadaye nilikutana na baadhi ya wanajamii wenzangu. Kupitia wao na usaidizi wa familia yangu, hatimaye nilianza ART. Lakini baada ya kuanza dawa, maswali yalikuwa mengi mstakabali wangu utakuwaje?

Nitaweza kupata kazi? Je, nitaweza kuishi maisha ya kawaida? Nitaishi hadi lini? Nilitamani sana angekuwepo msichana wa umri wangu kunielekeza au kunitia moyo lakini msaada wa namna hiyo haukuwepo.

Baadaye niliungana na Kituo cha huduma kama mfanyakazi wa uhamasishaji. Nilifanya hivyo ili nijitafutie shughuli, niondokane na msongo wa mawazo, na nijenge nguvu ya kiakili. Kuanzia ngazi ya wilaya, nikapanda hadi ngazi ya jimbo. Kila nilipofanya kazi na jamii, nilihisi amani fulani ya ndani.

Kisha nikapata nafasi kufanya kazi kwa muda katika taasisi ya Jharkhand State AIDS Control Society, lakini sikupata kile nilichotafuta. Nilihisi bado nataka kufanya zaidi hasa kwa ajili ya vijana ili hakuna kijana mwingine apatwe na maumivu niliyopitia. Nilihisi nataka wawe na msaada, mwongozo, na huduma kwa wakati.

Hatimaye nikaanza kufanya kazi katika ngazi ya kitaifa kama Mratibu wa Vijana. Leo, zaidi ya vijana 1,800 kutoka majimbo yote ya India wanaunganishwa nasi moja kwa moja. Tunao mabalozi wa vijana kila jimbo, na nashukuru kuwa sasa tunaweza kuwafikia vijana ambao hapo awali hawangeweza kutufikia kabisa.

 

Changamoto zako kuu zilikuwa zipi, na uliitoa wapi nguvu ya kuzishinda?

Changamoto yangu kubwa ilikuwa unyanyapaa niliokuwa nimeubeba moyoni, pamoja na ule wa jamii. Wakati fulani nilipoenda kwa daktari binafsi, aliniambia maneno ya kunidhalilisha hata siwezi kuyatamka hapa. Fikiria tayari hauna uelewa wa kutosha kuhusu VVU, halafu unaambiwa maneno ya kukushusha hadhi. Nilivunjika moyo sana, nikafikia hatua ya kukata tamaa hata kuhusu kuanza matibabu.

Lakini kwenye kituo cha ART nilikutana na wanajamii wenzetu. Waliniambia, “VVU si mwisho wa maisha. Unaweza kufanya kila kitu unachotaka.” Hapo ndipo mara ya kwanza nilipohisi nguvu ya kuendelea mbele.

Kabla ya kuungana na jamii, niliwahi kufanya kazi katika hospitali ndogo ili tu nijiweke na shughuli nyingi.

Mwezi wa kwanza ulikuwa mzuri, nilifanya kazi vizuri. Lakini baadaye nikaingiwa na hofu ikiwa hali yangu ingemuathiri mtu siku moja? Singeweza kuishi na hatia hiyo. Kwa hiyo niliamua kuwaambia ukweli. Ndani ya siku 15, nikaambiwa niondoke. Walinichukulia kama mkosaji.Lakini tukio hilo lilinijengea msimamo nilijua lazima nipambane.

Daktari wangu wa ART ndiye alinionesha mwelekeo mpya. Akanipa moyo kila siku. Kisha viongozi wetu wa jamii walinisaidia sana kunifariji, kunisimamia, na kunijengea uwezo. Hatimaye nilipofika ngazi ya kitaifa, viongozi wengi waliendelea kuninyanyua. Kwao wote, nimefika hapa nilipo leo.

Ulipogundua una VVU, familia yako ilikusaidia vipi?

Familia yangu ilikuwa nguzo yangu. Hawakuninyanyapaa kamwe. Hawakunifanya nijione tofauti. Walikuwa nami kila hatua kutoka kunipa dawa, kunipeleka kituo cha ART, hadi kunitia moyo.

Walikuwa pia na hofu na hatia fulani kwamba niliingia kwenye ndoa nikiwa mdogo sana, na kisha changamoto ya VVU ikaongezeka. Labda kwa sababu hiyo, waliamua kunisimamaia kikamilifu.

Naamini kuwa msaada wao ndiyo uliyonisimamisha tena na kunipa nguvu ya kuendelea.

Pooja anasema kwamba baadaye yake sasa imeunganishwa kikamilifu na mtandao wa wenzake wenye hali kama yake: “Maono au dhamira yoyote niliyo nayo, naiiona kupitia mtandao huu.”

© Pooja Mishra

UNAIDS na mashirika mengine yalikusaidiaje?

Nilifika UNAIDS (shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na VVVU) kwa mara ya kwanza nikiwa na mmoja wa viongozi wetu. Tulipokuwa tukieleza changamoto za vijana, ma’am alituskiliza kwa makini sana. Kusikilizwa kwa dhati kunakupa hisia ya kuunganishwa nilihisi anatuona, anatuelewa.

Baadaye tulipoendeleza harakati za vijana, msaada wa kiufundi tuliopata kutoka UNAIDS ulikuwa mkubwa sana. Tuliwahitaji kwa matukio mbalimbali walikuwepo. Walitupa mwongozo, mbinu bora, na njia za kuwafikia vijana.

Uwepo wao umekuwa msaada sio tu kwa maisha yangu binafsi, bali kwa mtandao wetu wote.

Nini kinakupa hamasa ya kuwasaidia vijana wenzako wanaoishi na VVU?

Kitu cha kwanza ni kuongeza uelewa. Tunaposhirikiana kama jamii tunasimulia hadithi zetu, hofu zetu, safari zetu wengine pia hufunguka. Wanatuambia wazi, Na wanahisi kuwa jukwaa letu ni salama.

Tukiwa tunaingia ‘mubashara’ mitandaoni, watu 400–500 hujiunga papo hapo. Tunawaunganisha na mtandao wetu na tunawafuatilia kwa karibu.

Tunao viongozi wa vijana kutoka mikoa mingi Maharashtra, Gujarat, Bihar, West Bengal, Assam, Punjab, na kwingineko. Tuwafikia hata kupitia majukwaa kama Grindr na Tinder mahali ambapo wengi hawafiki kwenye vituo vya kupima.

Kazi yetu haishi kwenye kupima tu. Tunawaunganisha na ART, kuhakikisha hawakosi dawa, na kubaki na mzigo mdogo wa virusi.

Tunatambua umuhimu wa msaada wa marafiki wa karibu kwa sababu sisi wenyewe tumewahi kupitia maumivu na hofu hizo.

Ungependa watunga sera wafanye nini? Ni mapengo gani bado yapo?

Tumegundua kuwa pale ambapo jamii inashirikishwa kikamilifu, mambo mengi yanaboreka. Sisi tusichukuliwe kama wanufaika tu tushirikishwe kama washirika wa kufanya uamuzi.

Changamoto kubwa tuliyonayo sasa ni uendelevu wa mtandao wetu. Tumeshaunda harakati hii, lakini kuiendeleza kwa muda mrefu ni changamoto. Bila mtandao wenye nguvu, hatutaweza kuwafikia vijana wala kutoa msaada wa kijamii.

Kwa hiyo tunaiomba serikali na washirika wote tupewe msaada endelevu, hasa katika afya ya akili, kupima, matibabu, na uelimishaji wa matibabu. Na tushirikishwe kila ngazi.

Unaona aje maisha yako ya baadaye? Maono yako ni yapi?

Baadaye yangu sasa imeunganishwa kabisa na mtandao wetu. Ndoto yangu yote iko hapa.

Kuna wakati nilihisi maisha yangu yameisha. Lakini leo, ninapoona wengine wakitabasamu na wakisema, “Asante, kwa sababu yako niliweza kujinusuru,” napata amani ambayo sijawahi kuipata mahali pengine.

Maisha yangu sasa ni kwa ajili ya jamii. Ni kwa ajili ya vijana ambao wanapotea kimya kimya hasa wale wanaopitia changamoto za afya ya akili.

Ninaahidi, ma’am, nitasimama na wote wanaopitia msongo wa mawazo hasa vijana wetu. Sitaki mtu yeyote ahisi upweke kama nilivyohisi mimi.

Ni ujumbe gani ungependa kutoa kwa wengine wanaoishi na VVU, hasa katika Siku ya Ukimwi Duniani?

Ujumbe wetu ni mmoja tu: Msijifiche. Kama huwezi kuieleza Dunia sawa. Sio lazima ujitangaze kila mahali.

Lakini jamii ipo kwa ajili yako. Njoo uongee nasi, usikae kimya, usijitenge. Ukikaa peke yako, hofu itaongezeka. Lakini ukituungana, utagundua kuwa huko peke yako una jeshi la watu lina kusimamisha.

Na muhimu zaidi: Ahidi kwamba utatumia dawa zako maisha yote. Usikatishe ART. Dawa zako ndizo kinga yako kubwa zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *