Dar es Salaam. Siku moja baada ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kuwataka mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuwajibika endapo kutakuwa na malalamiko ya foleni bila suluhisho la muda mfupi au mrefu, wadau wametoa mitazamo tofauti kuhusu kauli hiyo.

Ulega alitoa agizo hilo jana, Jumapili Novemba 30, 2025, jijini Dar es Salaam alipokagua maendeleo ya upanuzi wa Barabara ya Mbagala Rangi Tatu–Kongowe.

Akizungumza na wananchi wa eneo hilo, Waziri Ulega alisema, “ninaagiza kwa mameneja wote nchi nzima, nikisikia habari za foleni zinalalamikiwa na wananchi na hakuna suluhu ya muda mfupi na ya muda mrefu, hufai kuwa meneja.”

Pia, alisema tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha Sh54 bilioni kwa ajili ya kutatua kero ya foleni kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Leo Jumatatu Desemba mosi, 2025 wadau wa usafirishaji wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Madogo na ya Kati (Tamstoa), Chuki Shabani amesema suala la foleni ni la mtambuka,  kubebeshwa mzigo huo Tanroads pekee ni kuwaonea.

Shabani amesema hata kama zitajengwa barabara sita hadi nane, foleni katika Jiji la Dar es Salaam hazitaisha kama hatua zaidi hazitachukuliwa na kutolea mfano Barabara ya Mandela kuelekea bandarini ambayo foleni yake imekuwa ni kero ya muda mrefu.

Akifafanua zaidi, mwenyekiti huyo amesema haoni sababu za Chuo cha Uhasibu (TIA), Chuo cha Mafunzo Polisi Kurasini, Uwanja wa Maonyesho Sabasaba  na Kambi ya Jeshi   kuwa katika maeneo yale ya  Kurasini ambako shughuli za bandari  zinafanyika.

“Tulishawahi kutoa maoni mara kwa mara, tunapokutana na watu wa Serikali kwamba taasisi ambazo hazihusiani moja kwa moja na shughuli za bandari zingehamishiwa nje ya mji, na maeneo hayo yakatumika kama maegesho ya muda kwa magari yanayotoka nje ya nchi kuja kuchukua mizigo bandarini.

“Hii ni kwa sababu si kila mwenye magari ana uwezo wa kujenga ‘yard’ ndani ya jiji, ukizingatia kwamba bandari yetu inahudumia zaidi ya nchi nane zinazotuzunguka,” amesema.

Pia, Shabani amesema haoni haja ya matenki ya mafuta kuendelea kujengwa bandarini badala yake yangejengwa Bandari Kavu ya Kwala, huku akitolea mfano  Zambia wao wamepeleka mafuta kutoka Dar es Salaam zaidi kilometa 2,000 hadi nchini kwao Kapripoint, itakuwa Tanzania hadi Kwala ambako ni kilometa 60 tu.

Katibu wa Chama cha Tax Mtandao, Nobel Ford amesema haoni kama ni sahihi  Tanroads peke yao kubebeshwa mzigo huo na kueleza kwamba, polisi wa usalama barabarani nao kwa kiasi fulani wanahusika.

“Kuna wakati barabarani unakuta askari wa usalama barabarani wapo na foleni ipo, lakini wao wanafanya mambo yao ikiwamo kuwa ‘busy’ kukamata magari yenye makosa  na kutufanya tuone kwamba,wanafanya kusudi ili waweze kukamata watu kirahisi,” amesema katibu huyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Madereva na Makondakta wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (UWAMADAR), Shukuru Mlawa amesema suala la foleni zingine zinatengenezwa  na madereva wenyewe wa daladala kwa kupandisha na kushusha abiria maeneo yasiyo na kituo.

Amesema katika suala hilo wameendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya tabia hizo ili kuzidhibiti, japokuwa anasisitiza kuwa, kila mtu anapokuwa barabarani ana uamuzi wake binafsi, hivyo kama viongozi hawawezi kuwepo kila mahali kusimamia kila kitendo.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shufwaya Lema amesema wanamuunga mkono Waziri Ulega pamoja na Serikali kwa jumla kwa kutambua tatizo la foleni na kuanza kuchukua hatua.

Amesema foleni hizo, mbali na kuchelewesha wananchi kufika kwenye maeneo yao ya kujitafutia riziki, pia zimekuwa zikichangia kudhoofisha uchumi wa nchi.

Akitolea mfano eneo la Kongowe, Lema amesema kero yake imekuwa ya muda mrefu, mtu unaweza kuchukua hata saa tatu kutoka Kongowe kufika Mbagala wakati dakika kumi zingetosha.

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Yaendayo Mkoani (Taboa), Mustafa Mwalongo anaungana na Ulega katika hilo, akisema anaona Tanroads wamekuwa wakichukua muda mrefu kukamilisha ujenzi wa barabara zao, hivyo kuchangia foleni.

“Hizi barabara zinazotengenezwa ikiwamo ya Morogoro na ile ya Tegeta -Mwenge, zimekuwa zikichukua muda mrefu kuisha licha ya kuwa wanaongeza vipande vifupi tu, wakati wangeweza kufanya jitihada hata ya kuzijenga usiku na mchana ili ziishe kwa wakati.

“Ukiacha barabara wanazojenga, lakini wao ndio wanaotakiwa kutoa ushauri pale wanapoona barabara fulani ni finyu  kwa kuishauri Serikali nini kifanyike ili kuondoa tatizo hilo, kwa hiyo mimi niseme Tanroads hawawezi kukwepa katika adha hii ya foleni,”amesema Mwalongo.

Wakati wasafirishaji wakisema hayo, baadhi ya wananchi wamesema kila anayehusika na barabara anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuwa mwisho wa siku gharama yote inakuja kumwangukia mwananchi wa kawaida.

Iddi Seif, mkazi wa Gongo la Mboto, amesema humlazimu kutumia hadi Sh20,000 kwa siku katika usafiri ili kukwepa foleni kwa kukodi usafiri wa pikiki wakati angeweza kutumia sio zaidi ya Sh2,000 na kuhoji kwa kipato gani anachoingiza kwa siku.

Hata hivyo, amesema anafanya yote hayo ili asiharibu kibarua chake kwa kuchelewa kazini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *