Katika kambi ya Al-Dabbah, maelfu ya familia wamehifadhiwa. Wakimbizi wengi wanaishi kwenye mahema ya plastiki au wanalala juu ya mikeka iliyochakaa. Wakimbizi hawa ambao wengi wao wanatoka kati mji wa Elfasher ambao ni mji mkuu wa jimboa la Darfur na unaoshikiliwa na wapiganaji wa RSF wanaishi katika hali mbaya ya maisha.
Madaktari na wahudumu wa afya wanapata wakati mgumu kuwahudumia majeruhi wa vita hivyo ambavyo vinaendelea kuyapoteza maisha ya watu wasio na hatia hasa katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur ambalo sasa wanaudhibiti mji mkuu wa jimbo hilo wa Elfasher.
Kundi la watu 60, likiwa na madaktari, wauguzi na wafamasia, limeanzisha kliniki ndogo ndogo katika kambi hii ikiwa ni pamoja na duka la madawa, maabara, na hema ndogo zinazotumika kama sehemu za kulala wagonjwa. Viti vya plastiki vinatumika pia kama meza za ukaguzi. Magari machache yaliyopatikana kutoka mji jirani yanatumika kama magari ya wagonjwa na kliniki zinazozunguka.
Kila siku, makumi ya wagonjwa huwasili katika kambi hii huku wengi wakiwa na maambukizi katika mifumo ya upumuaji, kuharisha, matatizo ya ngozi au macho. Hali ya msongamano, ukosefu wa maji safi, na ukosefu wa madawa unafanya wagonjwa na wahudumu wa afya kupata taabu sana katika kambi hiyo.
Mwanamke mmoja ambaye pia ni mfamasia, kwa majina ya Elham Mohamed, amesema kwamba wao kama wahudumu wa afya wanafanya hivyo kwa sababu wanawahadumia wenzao waliotoka sehemu moja. Mwanaume mwingine kwa majina ya Ikhlas Abdallah ambaye ni daktari mkimbizi amesema kwamba wanafanya kila jitihada kuhakikisha wanatoa msaada aya matibabu kwa ajili ya kuwaokoa wenzao wenye hali mbaya zaidi.
Huduma kwa wagonjwa zinatolewa kwa changamoto kubwa
Kabla ya kukimbia, Ikhlas Abdallah alikuwa akifanya kazi masaa mengi katika chumba cha uzazi mjini El-Fasher hospitali ambayo wakati huo ilikuwa ya mwisho kufanya kazi mji mzima, ulioathiriwa sana na vita vya Sudan.
Aliukimbia mji huo Oktoba 26 baada ya wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) kuuvamia. Abdallah anasema alikimbia kwa sababu wapiganaji hao hawakuweza kutambua mara moja kwamba yeye na wenzie walikuwa madaktari sababu iliyopunguza hatari ya kifo, utekaji nyara au kukamatwa kwa ajili ya kikombozi hapo baadaye.
Katika safari yao ya kukimbia, madaktari hao na wahudumu wa afya waliendelea kutibu wakimbizi wenzao lakini kwa siri kubwa. Abdallah amesema, wakati RSF walipogundua kuwa watu walitibiwa, waliwakamata, kuwapiga na hata kuuawa. Kwa mujibu wa taarifa za shirika la afya ulimwenguni (WHO), vita hivi vimepelekea takriban mashambulizi 285 dhidi ya vituo vya afya tangu ilipoanza huku wahudumu wa afya 1,2024 na wagonjwa wengi wakipoteza maisha au kujeruhiwa.
Hadi sasa, watu wengi katika kambi hiyo ya wakimbizi na maeneo mengi yaliyoathiriwa na mgogoro huo wanakumbwa na upungufu mkubwa wa misaada: madawa, maji safi, huduma maalum za afya na usalama vimekuwa ni changamoto kubwa. Matokeo yake, maisha ya mamia au maelfu ya wakimbizi yanabaki kuwa hatarini.
