
Dar es Salaam. Macho na masikio ya wananchi yataelekezwa tena Dar es Salaam, ambako Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kulihutubia Taifa kuhusu yanayoendelea nchini, ikiwemo masuala ya usalama na kuliponya Taifa.
Hotuba hiyo itakayotolewa kesho Jumanne, Desemba 2, 2025, inakuja katikati ya hofu ya usalama waliyonayo baadhi ya wananchi kutokana na maandamano yaliyozaa vurugu ya Oktoba 29 na mengine yanayopangwa kufanyika Desemba 9, 2025, kupitia mitandao ya kijamii.
Katika vurugu hizo, baadhi ya watu walipoteza maisha, kujeruhiwa, biashara na mali za watu binafsi ziliharibiwa, kadhalika miundombinu ya umma vikiwemo vituo vya polisi, ofisi za Serikali za mitaa, ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM), Mahakama na vituo vya mafuta vilichomwa moto.
Ni hotuba inayosubiriwa kwa hamu, kwa sababu ndiyo itakayoamua ama kuponya majeraha yaliyomo miongoni mwa Watanzania, au kuja na hatua zitakazojenga mustakabali mwema wa Taifa.
Hotuba hiyo inaibua shauku zaidi hasa ukizingatia inatolewa nyakati ambazo tayari Rais Samia ameshaunda tume kuchunguza kiini cha vurugu na ameshawasamehe vijana kadhaa waliokamatwa kwa kuhusika na matukio hayo.
Novemba 20, 2025, Rais Samia alipoizindua tume hiyo yenye wajumbe wanane ikiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Othuman Mohamed Chande, aliiagiza kwenda kusaka kiini cha tatizo hilo na kuja na mapendekezo yatakayoweka msingi wa maridhiano.
Rais Samia alisema tume hiyo itafanya kazi kwa miezi mitatu sawa na siku 90: “Mapendekezo yatakayotoka huku (Tume ya Uchunguzi) ndiyo tutakayokwenda kuyafanyia kazi kwenye Tume ya Maridhiano. Kwa hiyo, mapendekezo yenu ndiyo yatafanya ajenda za Tume ya Maridhiano.”
Wakati wadau wakisubiri majibu ya tume, leo Jumatatu, Desemba 1, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amekutana na waandishi wa habari ofisini kwake na kueleza kuwa kesho Jumanne, Rais Samia atazungumza na wazee wa mkoa huo.
Chalamila amesema kupitia wazee wa Dar es Salaam, Rais Samia atalihutubia Taifa katika ukumbi wa Julius Nyerere kuanzia saa 5 asubuhi. Amesema mkuu huyo wa nchi ataambatana na viongozi wa Serikali na wasio wa Serikali ambao watakuwa na mchango mkubwa kwenye mazungumzo hayo kwa mustakabali wa Taifa.
“Ni mkutano mwafaka, unaorejesha matumaini na kuendelea kuponya pale ambapo Watanzania waliumia,” amesema Chalamila.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi waliozungumza na Mwananchi baada ya Chalamila kutoa taarifa yake wamekuwa na mitazamo tofauti hasa ikizingatiwa haikutarajiwa tena kama atazungumza.
Mwanahistoria wa siasa za kimataifa, Dk Azikiwe Boraufe, amesema taifa liko katika “hali tete” inayohitaji hatua za haraka za kurejesha imani.
“Kabla Rais hajaongea na wazee, alitakiwa kwanza kukaa na viongozi wake na wasaidizi wake. Lazima tujiulize tumefikaje hapa na tunahitaji nini kutoka hapa tulipo,” amesema.
Boraufe ametaja tatizo kubwa la viongozi kupuuza ishara za mgawanyiko katika jamii na taasisi, akitolea mfano mpasuko ndani ya CCM uliowahi kuonekana wakati wa marehemu Bernard Membe na kuibuka upya mwaka huu kupitia mchakato wa kumpitisha mgombea wa urais.
“Hivi vitu tuliviona kama vidogo, lakini sasa vimetuletea majeraha makubwa. Mwangwi wa baadhi ya wanachama kupinga mchakato wa mwanzo wa mwaka huu ulikuwa tahadhari ya wazi,” amesema.
Amesema mfululizo wa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa wanasiasa umeongeza hasira, huku akisema Rais anapaswa kutumia hotuba hiyo kurejesha matumaini.
“Sasa hatuhitaji kuunganisha vigae vilivyovunjika. Tunahitaji kuchimba udongo mpya na kufinyanga chungu kipya,” amesema.
Boraufe pia amependekeza kufutwa kazi kwa watumishi wote waliohusika na mauaji ya raia wasio na hatia Oktoba 29.
Mwanaharakati wa haki za binadamu, Dk Hellen Kijo Bisimba, amesema hotuba ya Rais Samia ni hatua nzuri, lakini imekuja nje ya wakati.
“Alitakiwa kuzungumza na Taifa mapema sana, hata siku ya kuapishwa Dodoma. Zaidi baada ya viongozi wa dini kukumbushia tukio la mauaji ya Oktoba 29. Mimi namuonea huruma,” amesema.
Kuhusu hali ya nchi kwa sasa, Bisimba, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), amesema mizizi ya tatizo imo kwenye uchaguzi wa mwaka huu, ambao matokeo yake yalipingwa na makundi mbalimbali.
“Uchaguzi haukuwa wa haki. Matokeo yaliyomtangaza Rais Samia yameacha mashaka makubwa. Ndiyo maana tunashuhudia hasira na mpasuko mkubwa wa kijamii,” amedai.
Kwa upande wake, mtaalamu wa uchumi, Hamduny Marcel, amesema kuliponya taifa ni pamoja na kuonesha msimamo kwa kusema hapana katika baadhi ya mambo.
Amesema wananchi wa sasa hawapendi kuendeshwa kilaini, bali wanataka kuona kiongozi anayechukua hatua za haraka jambo linapotokea, jambo atakalosaidiwa kwa kuwa na watendaji wenye kasi wanaoshughulikia matatizo ya watu kwa wakati.
Pia amesema kuhutubia Taifa mara kwa mara ni moja ya njia inayoweza kusaidia kuliponya Taifa kwa kutumia hotuba zilizobeba sauti kali zenye msisitizo wa maneno.
“Ukisema mimi ni mama ni sawa, lakini kuna watu hawataki umama, wanataka kusikia sauti ya mwanamke wa chuma mwenye uamuzi wa chuma na utendaji wa chuma. Ukitoa uamuzi hakikisha unafanyika, watu wanataka kusikia sauti ya uamuzi wenye kuendeleza nchi.
“Nilitamani kuona mawaziri wote wanafanya kazi inayoonekana. Kama hawafuatilii mambo waondolewe, kwa sababu watu wapo wanaoweza kuongeza kasi, kwani watu wanataka kuona matokeo kuliko uwepo wa mtu,” amesema.