Unguja. Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen Wasira, amewataka vijana kutokubali kutumiwa kuhatarisha amani ya nchi kwa kivuli cha kudai haki zao.

Amesema kuna baadhi ya taasisi zisizo za kiserikali zinazowahonga vijana kwa fedha ili kuwashawishi kufanya vurugu, huku zikijificha nyuma ya madai ya kutetea haki.

Wasira amesema hayo leo, Jumatatu Desemba 1, 2025, katika mahafali ya 10 ya chuo hicho, Kampasi ya Zanzibar, yaliyofanyika Bububu, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesisitiza kuwa haki haiwezi kupatikana kwa kuvuruga amani ya nchi, badala yake kufanya hivyo kunaweza kusababisha watu kupoteza hata haki za msingi ikiwemo ya kuishi.

Wasira ameongeza kuwa vijana wanapaswa kulinda amani iliyopo ili waweze kupata haki wanazozitaka kwa njia sahihi.

“Nchi hii haina hati miliki ya mtu, ipo kwa ajili ya Watanzania wote, kwa maana hiyo kila mmoja ana wajibu wa kuitunza amani hiyo na vijana msikubali kutumika vibaya,” amesema Wasira. 

Vilevile, amesema Tanzania haina uadui na nchi nyengine yeyote, lakini zipo ambazo zinaichukia na hawapendi maendeleo yanayofanyika kwani wanaamini endapo wakifanya hivyo itakuwa kitovu cha uchukuzi.

Pia, amewataka wahitimu hao wasibweteke waendelee kusoma kwa lengo la kujitofautisha baina yao na ambao hawajasoma kwa kuendelea kuthibitisha umuhimu wa elimu ndani ya jamii.

Sambamba na hilo, amefurahishwa kuona Zanzibar imepiga hatua kubwa zaidi kwa kutoa elimu kwa wanawake tofauti na awali ambapo wengi wao walikosa fursa hiyo.

Awali, akitoa hotuba katika mahafali hayo, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Haruni Mapesa amesema kuwa kwa mwaka wa masomo 2024/25, chuo kimesajili wanafunzi 20,250.

Profesa Mapesa amesema ongezeko hili linadhihirisha imani ya wanafunzi na walimu katika mabadiliko yanayofanyika katika sayansi na teknolojia.

Amesema kuanzia mwaka 2018 hadi sasa, wanafunzi 7,330 wamehitimu kupitia kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho.

Aidha, chuo kinaendelea kutoa mafunzo ya maadili na uzalendo, lengo likiwa kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora wa baadaye, wenye maono ya haki na utawala bora.

Profesa Mapesa pia amebainisha kuwa chuo kimefanikiwa kuunganishwa na mkongo wa Taifa, hatua inayolenga kuwekeza katika sayansi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia.

Sambamba na hayo, jumla ya wanafunzi 1,249 wamehitimu katika mahafali hayo, kati ya hao wanawake 818 sawa na asilimia 65 na wanaume 431 ikiwa sawa na asilimia 35.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *