Mafuriko mabaya yaliyozikumba nchi za Indonesia, Sri Lanka, Thailand na Malaysia yamepelekea zaidi ya watu 1,000 kupoteza maisha katika kipindi cha chini ya wiki moja. Kwa uchache watu 502 wameripotiwa kufariki dunia nchini Indonesia, 335 nchini Sri Lanka, 176 nchini Thailand na watatu nchini Malaysia.

Huku hayo yakiripotiwa, Rais wa Indonesia yuko chini ya mashinikizo makubwa ya kutangaza hali ya hatari ili kukabiliana na mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi ambayo yameitikisa nchi hiyo.

Nasir Jamil, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Indonesia kutoka jimbo la Aceh lililoathiriwa sana pamoja na jimbo la Sumatra, amesema kwamba wanamshinikiza mno Rais wa Indonesia atangaze dharura ya kitaifa ili kuharakisha mchakato wa kurejesha hali nzuri na kuratibu juhudi za misaada kutoka pembe zote.

Huko Aceh, mafuriko makubwa yamebomoa nyumba na madaraja, yameharibu majengo ya serikali na kuacha baadhi ya jamii zikiwa zimekwama kwenye matope na hazina barabara za kutokea.

Hayo yakiwa ni ya Indonesia, huko nchini India nako, mvua za mara kwa mara zimeongezeka katika jimbo la Tamil Nadu na Idara ya Hali ya Hewa ya India imetoa “onyo jekundu” kwa wilaya za pwani za Cuddalore, Chennai, Puducherry na sehemu za Andhra Pradesh. Hayo ni kwa mujibu wa gazeti la The Indian Express.

Kwa huko nchini Sri Lanka muungano mkubwa zaidi wa upinzani bungeni umeishutumu serikali kwa kushindwa kuchukua hatua za tahadhari za kupunguza uharibifu uliosababishwa na mafuriko, licha ya maonyo yaliyotolewa mapema na shirika la hali ya hewa.

Gazeti la Daily Mirror la Sri Lanka limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Mbunge Kabir Hashim ameliambia bunge kwamba uharibifu mkubwa ungeweza kuepukwa kama hatua za tahadhari zingechukuliwa kufuatia maonyo yaliyotolewa na shirika la hali ya hewa Novemba 12, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *