Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchi hizo tatu za bara Asia, mafuriko na maporomoko ya ardhi yamewaua watu 604 nchini Indonesia, 366 nchini Sri Lanka na 176 nchini Thailand.
Rais wa Indonesia, Prabowo Subianto, ameahidi kujenga upya miundombinu wakati akitembelea maeneo yaliyoathirika. Baadhi ya maeneo bado hayafikiki, barabara zikiwa zimeharibiwa na nyaya za simu kukatika na kusababisha changamoto kubwa ya mawasiliano.
Wakazi Indonesia wanapokea misaada kupitia ndege zinazosambaza mahitaji muhimu ya binaadamu katika maeneo yaliyoathirika huku watu 464 wakiwa hawajulikani walipo. Mafuriko hayo yamesababisha pia waindonesia 290,700 katika mikoa ya Sumatra Kaskazini, Sumatra Magharibi na Aceh, kukosa makazi hii ikiwa ni kwa mujibu wa Shirika la Kitaifa la Usimamizi wa Maafa.
Akizungumza na waandishi habari, rais Prabowo amesema ni wakati wa kuchukua hatua za haraka kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tunapaswa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa ufanisi. Serikali za mitaa lazima zichukue jukumu kubwa katika kulinda mazingira na kujiandaa kwa hali mbaya ya hewa itakayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi nchi.”
Nchini Sri Lanka, serikali huko imesema timu ya waokoaji inawatafuta watu 367 ambao pia hawajulikani walipo. Takribani watu 218,000 wako kwenye makazi ya muda baada ya kukumbwa na mvua hiyo kubwa iliyosababisha maporomoko hayo ya ardhi, hasa katika maeneo ya kilimo cha chai kwenye milima ya kati.
Nako nchini Thailand, msemaji wa serikali Siripong Angkasakulkiat, amesema malipo ya fidia ya kwanza yalipangwa kuanza leo Jumatatu (01.12.2025), ambako dola milioni 7.4 zitagawanywa kwa watu 26,000. Angkasakulkiat ameongeza kuwa mamlaka zinafanya kazi kurejesha miundombinu ikiwemo maji na umeme katika maeneo ya kusini ambako watu milioni 3.9 wamethirika na mafuriko hayo.