Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi amesema, ni Marekani ndiyo inayopaswa kurudi kwenye diplomasia kwa kuifanya Iran iwe na imani nayo.

Araghchi ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Toshimitsu Motegi Jumatatu alasiri kujadili matukio ya hivi karibuni ya pande mbili pamoja na masuala ya kimataifa.

Mwanzoni mwa mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alimpongeza mwenzake wa Japan kwa kuteuliwa tena kushika wadhifa huo na akasema, ana matumaini kuwa kutokana historia ya uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili na uzoefu na tajiriba ya kipindi kilichopita wakati Motegi aliposhikilia wadhifa huo, ushirikiano wa karibu, wa ubunifu na ufanisi uliopo kati ya Tehran na Tokyo utaendelea tena katika kipindi hiki kipya.

Akiashiria mwenendo wa hivi karibuni kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran na hatua na misimamo iliyoonyeshwa na Marekani na nchi tatu za Ulaya kuhusiana na suala hilo, Araghchi amesisitiza kwa kusema: “ni Marekani ndiyo inayopaswa kurudi kwenye diplomasia kwa kuifanya Iran iwe na imani nayo.”

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan amesisitizia msimamo wa nchi yake wa kujitolea kutoa mchango wa kujenga katika kuimarisha amani na utulivu katika eneo la Asia Magharibi, na akakaribisha ubunifu wa kisiasa wa kutatua masuala ya kikanda na kimataifa, na kutilia mkazo pia uungaji mkono wa nchi yake wa kutatua masuala kwa njia za kisiasa.

Mawaziri hao wamejadili pia hali ya hivi karibuni ya ushirikiano wa pande mbili, masuala ya kibalozi, na masuala ya huduma za kibinadamu kati ya nchi zao mbili, na kusisitiza haja ya kuendelea kuwa na mashauriano ya mara kwa mara kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa jadi na wa kirafiki kati ya Iran na Japan…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *