
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Dkt. Denis Mukwege amelaani mchakato wa amani unaoendelea kati ya serikali ya Kinshasa na waasi wa M23 unaolenga kukomesha mapigano mashariki mwa DRC.
Katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki, Mukwege aliuita mpango huo unaoongozwa na Washington na Doha kuwa “haramu, usio na uhakika na usioweza kuhakikisha amani ya kudumu.”
Mukwege ameashiria kile alichokiita “mienendo ya uwindaji” ya wahusika wa kigeni wanaowania rasilimali kubwa za madini katika eneo hilo.
Amesema makubaliano hayo yanapuuza sababu za msingi na mienendo ya kikanda ya mzozo huo, na badala yake yanahudumia maslahi ya kijiografia ya nchi za kigeni.
Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel amesema, watu wa mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini wametengwa katika mazungumzo hayo na bado “wananyimwa haki zao za msingi.”
Mukwege amekosoa mchakato wa amani unaoendelea kwa sasa akisema hauna uwazi, dhamana au ratiba iliyo wazi.
Mukwege anasema, ili kuweza kuhakikisha amani ya kudumu, makubaliano yoyote lazima yajumuishe jamii zilizoathiriwa katika majadiliano na kuweka haki zao mbele ya maslahi ya kigeni na kiuchumi.
Wakati huo huo viongozi wa upinzani nchini DRC wamemtaka Rais FĂ©lix Tshisekedi kuuweka mkataba huo hadharani kabla ya kuusaini na kuonya dhidi ya kukubali chochote “kitakachodhoofisha mamlaka ya kujitawala ya DRC.”
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Marais Felix Tshisekedi wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame wiki hii wanatarajiwa kutia kusaini makubaliano ya mwisho yanayolenga kufikia amani ya kudumu mashariki mwa Congo.