KOCHA wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi leo ana mtihani mgumu mbele ya Florent Ibenge anayeinoa Azam, wakati timu hizo zitakapocheza mechi ya Ligi Kuu Bara.
Mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar kuanzia saa 3:00 usiku, inazikutanisha timu zilizotoka kucheza mechi za Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.
Azam ambayo imepoteza mechi mbili mfululizo za Kundi B mbele ya AS Maniema ya DR Congo na Wydad Casablanca ya Morocco, itaikaribisha Singida Black Stars iliyoambulia pointi moja katika mechi za Kundi C, ikifungwa na CR Belouizdad na kutoka 1-1 dhidi ya Stellenbosch.
Mtihani wa Gamondi alionao mbele ya Ibenge leo ni kuusaka ushindi wa kwanza kwa Singida Black Stars nyumbani kwa Azam kwani mara nne timu hizo zilipokutana uwanjani hapo tangu Singida inaitwa Ihefu, haikuwahi kushinda, iliambulia vichapo.
“Daima tunachukua tahadhari tunapokutana na timu yoyote. Lakini unapokutana na timu yenye ubora kama Azam FC, ni lazima kuongeza umakini. Hata hivyo, tusisahau Singida pia ni timu yenye ubora. Tuna wachezaji bora, tunaonyesha kiwango kizuri, hali ya timu ni nzuri na motisha kwa wachezaji ipo juu, Naamini kutakuwa na mchezo mzuri siku ya kesho (leo).
“Nafikiri timu zetu zinafanana kwa kiwango kikubwa. Ingawa Singida ni timu changa, katika misimu ya hivi karibuni imejitambulisha kama moja ya timu nne bora, na ninaamini kwa sasa tupo kwenye kiwango kinachokaribiana. Azam FC pia bila shaka atachukua tahadhari dhidi yetu.
“Kwa upande wangu, jambo linalonitia wasiwasi zaidi ni hali ya utimamu wa mwili wa wachezaji wangu, kwa sababu hatujakuwa na muda wa kutosha. Bila shaka kutakuwa na pambano la kiufundi, lakini ubora wa mchezaji mmoja mmoja unaweza kuamua mchezo wakati wowote,” amesema Gamondi.
Hii itakuwa mechi ya tisa timu hizo zinakutana katika Ligi Kuu Bara tangu 2020 Singida ikifahamika kama Ihefu, huku rekodi zikionyesha timu hiyo imeshinda mara mbili tu mbele ya Azam ikiwamo mechi ya mwisho msimu uliopita.
Wakati Azam ikipoteza mechi mbili dhidi ya Singida, yenyewe imeshinda sita, hakuna sare kati yao hali inayoonyesha tunakwenda kushuhudia mechi yenye rekodi ya kupata mshindi.
Katika msimamo wa ligi, Azam ina pointi tano, huku Singida Black Stars inazo saba, zote zikishuka dimbani mara tatu. Singida katika mechi hizo tatu, imefunga mabao matatu ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila mechi, wakati Azam imefunga manne. Katika kujilinda, Azam imeruhusu mabao mawili, Singida moja.
JKT TANZANIA VS MTIBWA
Kabla ya mechi hiyo, itatanguliwa na ile itakayochezwa saa 12:30 jioni kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni jijini Dar na wenyeji na vinara katika msimamo wa ligi hiyo, JKT Tanzania itaikaribisha Mtibwa Sugar.
JKT iliyotoka kuichapa Fountain Gate kwao mabao 2-0, inasaka mwendelezo bora wa ushindi na kujikita zaidi kileleni mwa msimamo itakapoikaribisha Mtibwa Sugar ambayo nayo mechi ya mwisho imeichapa TRA United mabao 2-1.
Huo ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Kocha Yusuf Chipo tangu atue Mtibwa Sugar akiiongoza katika mechi mbili, akianza na matokeo ya 0-0 dhidi ya KMC, kisha ushindi wa 2-1 mbele ya TRA United.
Chipo ana mtihani wa kusaka ushindi nyumbani kwa JKT Tanzania inayonolewa na Ahmad Ally kwani timu hiyo haijawahi kupoteza mechi nne dhidi ya Mtibwa.
Mtibwa imeambulia sare mbili nyumbani kwa JKT Tanzania, huku ikipoteza mbili za mwisho.
Safu ya ulinzi ya Mtibwa Sugar inayoongozwa na nahodha, Erick Kyaruzi, itakuwa na kazi kubwa kumzuia kinara wa ufungaji, Paul Peter mwenye mabao matano na Saleh Karabaka aliyefunga manne.