Akizungumza Jumanne katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika karibu na eneo kulipotokea mripuko katika bandari ya Beirut mwaka 2020, Papa Leo amewasihi viongozi wa Mashariki ya Kati kuondokana na mawazo ya kulipiza kisasi na ghasia, na kufungua ukurasa mpya kwa ajili ya upatanisho na amani.
Katika mahubiri yake kwenye Misa hiyo iliyohudhuriwa na Rais wa Lebanon, Joseph Aoun na waumini wapatao 150,000, Papa Leo amesema wana matumaini ya kuihusisha Mashariki ya Kati yote katika roho ya udugu na kujitolea kwa amani, ikiwa ni pamoja na wale ambao kwa sasa wanajiona kuwa maadui.
Jumuiya ya kimataifa iendeleze juhudi za mazungumzo
Ameonya kuwa mustakabali wa maisha ya binadamu uko hatarini kutokana na migogoro inayoongezeka duniani.
”Kutoka kwenye uwanja huu, naiombea Mashariki ya Kati, na watu wote ambao wanateseka kwa sababu ya vita. Pia ninaomba hasa kwa ajili ya Lebanon. Ninaiomba jumuiya ya kimataifa kwa mara nyingine tena ifanye juhudi zozote katika kukuza michakato ya mazungumzo na maridhiano,” alisisitiza kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani.
Papa Leo pia amewataka wenye madaraka ya kisiasa na kijamii nchini Lebanon na katika nchi zote zinazokumbwa na vita na ghasia, kusikiliza kilio cha wananchi wao wanaoomba kupatikana kwa amani.
Aidha, ameitaka Lebanon kushughulikia migogoro ya miaka mingi ya kisiasa na matatizo ya kiuchumi, na kukomeshwa kwa mashambulizi na uhasama. Amewatolea wito viongozi wakuu wa madhehebu ya kidini kuungana ili kuiponya nchi hiyo na kuwasihi viongozi wa kisiasa kuendelea na juhudi za amani baada ya vita vikali vya mwaka jana kati ya Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, na mashambulizi ya Israel yanayoendelea.
Guinea-Bissau na Hong Kong zakumbukwa katika maombi
Papa Leo ameiombea pia Guinea-Bissau kutokana na mzozo wa kisiasa uliotokea hivi karibuni baada ya mapinduzi akitaka suluhisho la amani lipatikane, na amewakumbuka waathiriwa wa janga la moto lililotokea Hong Kong, pamoja na familia zao.
Ziara ya siku tatu ya Papa Leo nchini Lebanon imekamilika Jumanne, ambapo ilikuwa ni kituo cha pili cha ziara yake ya kimataifa ya kitume iliyoanzia nchini Uturuki. Hata hivyo, muda mfupi kabla ya kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Rafic Hariri, mjini Beirut kurejea mjini Roma, Papa Leo amesema ameshindwa kulizuru eneo la kusini mwa Lebanon, kwa sababu kwa sasa linakabiliwa na hali ya migororo.
(AFP, DPA, AP, Reuters)