Polisi Uganda wamkaba Bobi Wine katika kampeni za uchaguzi!Polisi Uganda wamkaba Bobi Wine katika kampeni za uchaguzi!

Matamshi ya hivi karibuni ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Uganda, Abbas Byakagaba, dhidi ya mgombea urais wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, yameibua wasiwasi mkubwa kwa wafuasi wa chama kikuu cha upinzani cha National Unity Platform, NUP. Kauli zake zimejikita katika lawama za kukiukwa kwa miongozo ya kampeni na vitisho vya kuchukua hatua kali.

Kwa mara ya kwanza, Byakagaba amekiri wazi kuwa yeye ndiye amekuwa akiagiza operesheni mbalimbali zilizolenga kudhibiti wafuasi wa NUP, ikiwa ni pamoja na msako uliopelekea zaidi ya wafuasi 180 kukamatwa na kufunguliwa mashtaka tofauti yanayohusiana na kampeni za Bobi Wine.

Kauli yake kwamba “hakukuwa na kosa” kwa polisi kutumia mbwa kuwatawanya wafuasi wa NUP imezua mjadala mpana, hasa ikizingatiwa kuwa uchaguzi umesalia takribani siku 44 tu kufanyika. Wafuasi wa NUP wamepinga vikali matumizi hayo ya nguvu wakiyataja kuwa kinyume cha haki za msingi.

Robert Kyagulanyi
Tangu alipojitosa kwenye siasa, Bobi Wine amekuwa mwiba mchungu kwa utawala wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni, kutokana na mvuto mkubwa alionawo hasa kwa vijana wa Uganda.Picha: Emmanuel Lubega/DW

Katika kikao cha waandishi wa habari, Mkuu huyo wa Polisi alidai kuwa Bobi Wine amekuwa akiendesha kampeni zenye mienendo isiyo halali, zikiwemo jitihada za kuandamana bila vibali. Hii imepekelea onyo kali kwamba polisi watachukua hatua kali zaidi ikiwa “uvunjaji wa sheria utaendelea.”

Baada ya matamshi hayo, polisi waliongeza nguvu kwenye kampeni za Bobi Wine, wakirusha mabomu ya machozi zaidi ya kawaida na kumuumiza mgombea huyo mwenyewe. Tukio hilo limeongeza wasiwasi kuwa machafuko yanaweza kuongezeka kabla ya uchaguzi.

Wataalamu wa masuala ya siasa wanasema hatua hizo zinaweza kuleta athari kubwa katika uchaguzi, hasa ikizingatiwa kuwa tayari mtu mmoja ameuwawa kwa kupigwa risasi katika makabiliano ya polisi na wafuasi wa NUP, huku wengine wakijeruhiwa vibaya.

Tuhuma za kumpendelea mgombea wa chama tawala, NRM

Baadhi ya raia wameeleza masikitiko yao wakisema kwamba kampeni hazipaswi kuwa tishio kwa maisha ya watu, na kwamba vurugu hizi zinahitaji kutazamwa kwa kina ili kubaini chanzo chake. Wengine wamesema hakuna mtu anayepaswa kuzuia watu wengine kuendesha shughuli zao za kila siku.

Pamoja na kukosolewa vikali, polisi wamesisitiza kuwa wana mbinu nyingi za kukabiliana na wafuasi wanaokiuka taratibu, wakitaja tukio la kutumia mbwa kama moja ya njia halali. Hata hivyo, NUP imeendelea kusisitiza kuwa polisi wana upendeleo mkubwa kwa chama tawala, NRM.

Kampeni za urais Uganda zavutia umati mkubwa wa watu

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Bobi Wine na wasemaji wake, akiwamo Shamim Nambasa, wameeleza kuwa polisi mara nyingi wanashindwa kuchukua hatua pale ambapo wafuasi wa NRM wanahusika, wakiongeza kuwa mara kadhaa wamepigwa, kutishiwa au kuviziwa bila tume ya uchaguzi kutoa kauli yoyote.

Uchaguzi mkuu nchini Uganda unatarajiwa kufanyika Januari 15, huku Rais Yoweri Museveni akionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda, hasa baada ya zaidi ya wabunge 70 wa chama tawala kukosa wapinzani katika majimbo ya ubunge.

Kwa upande mwingine, mvutano kati ya polisi na NUP unaendelea kuibua maswali kuhusu usalama, usawa wa ushindani, na mustakabali wa demokrasia nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *