Rais Samia: “Vurugu zilikuwa mpango wa kuiangusha Serikali”Rais Samia: “Vurugu zilikuwa mpango wa kuiangusha Serikali”

Katika hotuba yake maalumu jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa tathmini nzito kuhusu matukio ya vurugu yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, akisema yameathiri taswira ya Tanzania kama taifa la amani. Alisisitiza kuwa amani ndiyo utambulisho wa taifa, lakini matukio ya hivi karibuni yanaanza kuuteteresha msingi huo.

Rais Samia aliweka bayana kuwa vurugu hizo hazikuwa za ghafla, bali “tukio la kutengeneza” lililosukwa kwa makusudi na watu wasiolitakia mema taifa hilo. Alieleza kuwa baadhi ya wahusika waliyalenga matukio hayo yafanane na machafuko yaliyowahi kuikumba Madagascar, jambo analosema lingehatarisha ustawi wa nchi.

Kwa mujibu wa Rais huyo, watu kadhaa wamelipwa ili kushiriki maandamano, kushambulia miundombinu, na kuchochea ghasia. Alitaja uharibifu wa vituo vya mafuta, majengo binafsi, na vituo vya polisi kama ushahidi kwamba lengo halikuwa maandamano ya amani, bali kuleta taharuki kitaifa.

Rais Samia alijibu hoja kuwa serikali ilitumia nguvu kubwa, akisema kiwango cha nguvu hutegemea ukubwa wa tishio. Alihoji iwapo wakosoaji hao walitaka serikali “iutazame umati ukikamilisha walichotumwa,” jambo aliloliona kama kutowajibika kwa serikali.

Tanzania Dar es Salam 2025 | Rais Samia Suluhu Hassan kabla ya kuhutubia mkutano wa Baraza la Wazee wa Dar es Salaam.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Makamu wake, Dk. Emmanuel Nchimbi (kushoto) Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba (Kulia) kabla ya kuhutubia Baraza la Wazee wa Dar ee Salaam, Desemba 02, 2025.Picha: Courtesy of State House

Amebainisha kuwa ndani ya makundi ya waandaaji, kulikuwa na mawasiliano yaliyopendekeza maandamano mengine yahamishwe kutoka Desemba 9 hadi Desemba 25 kwa madai kuwa serikali ilikuwa imejipanga vya kutosha. Hata hivyo, Rais alisisitiza kuwa serikali “iko tayari wakati wote.”

Masharti kwa serikali, waratibu wa nje, na nafasi ya taasisi za dini

Rais Samia alisema baadhi ya wahusika wamekuwa wakitoa masharti kwa serikali ili kuanzisha mazungumzo, akisisitiza kuwa serikali huru haiwezi kuamrishwa. “Serikali haipewi masharti,” alitangaza, akisema maridhiano hayawezi kuendeshwa kwa msukumo wa nje.

Alidai pia kwamba waratibu wa vurugu wanaishi nje ya nchi, na uchunguzi unaendelea kuwabaini zaidi. Kwa wale walio ndani ya nchi, alisema baadhi ni wanasiasa waliopoteza mwelekeo, waliofarakana ndani ya vyama vyao, au wanaolipwa kutekeleza ajenda za kushusha nchi.

Katika hatua isiyo ya kawaida, Rais Samia alitoa ukosoaji mkali kwa taasisi za dini, akisema baadhi zimejiingiza katika kutoa matamko yanayoashiria kuunga mkono mkondo wa kisiasa. Alisisitiza kuwa Tanzania haina dini rasmi na hakuna dhehebu lililopewa mamlaka ya kuzungumza kwa niaba ya mengine.

Rais Samia atoa wito wa mshikamano wa kitaifa

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Akilitaja Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), alisema limekuwa likitoa matamko mengi—takriban manane—na hata ndani ya taasisi hiyo wapo wanaohoji uhalali wake. Alisisitiza kuwa viongozi wa dini wanapaswa “kuvaa majoho yao” na kuendelea na majukumu ya kiroho badala ya kuingizwa kwenye siasa za misukumo.

Kauli yake ameitoa siku moja baada ya katibu mkuu wa baraza la maaskofu katoliki nchini TEC, Padre Charles Kitime kufanya mkutano na waandishi wa habari na kukosoa jinsi nguvu kubwa zilivyotumika kuzima maandamano ya makundi ya vijana. Alitaka wale waliohusika katika mauwaji ya viaja hao kuwajibika au kuwajibishwa.

Madai kwamba serikali iliwazuia wapinzani kushiriki uchaguzi pia yalijibiwa. Samia alisema hakuna aliyezuiwa, na kwamba waliokataa kushiriki walifanya hivyo kwa hiari zao. Alishangazwa kwamba vurugu zilitokea siku ya uchaguzi pekee, akisema hilo linaibua maswali kuhusu lengo la maandamano hayo.

Ushindi wa CCM, wanaowageuka serikali, na wito wa kutibu jeraha la taifa

Rais Samia alitetea matokeo ya uchaguzi yaliokipa chama tawala CCM ushindi wa asilimia 97, akisema wanaouhoji hawakushiriki uchaguzi. Alisema waliojitokeza kupiga kura waliamua hivyo, na kwamba ushindi huo haupaswi kutiliwa shaka.

Akigusia masuala ya historia ya kisiasa, Samia alisema baadhi ya watu wanaoishutumu serikali leo ni wale wale aliowasaidia mwaka 2020 kwa kuwafutia kesi, kuwapa posho, na kuwagharamia wakati wakiwa nje ya nchi. Alisema licha ya kuwanyooshea mkono wa rehema, sasa ndiyo wanamgeukia na kumfanya adui.

Tansania Dar es Salaam 2025 | Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza mbele ya Wazee wa Dar es Salaam.
Rais Samia Suluhu Hassan akizumgumza mbele ya Wazee wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu masuala mbalimbali yanayolikumba taifa la Tanzania, Desemba 02, 2025.Picha: State House

Licha ya ukosoaji wake mkali, Rais Samia aliwaletea Watanzania ujumbe wa maridhiano. Alisema matukio ya vurugu yameacha jeraha, na jeraha hilo “litapona tu kwa Watanzania wenyewe” kupitia majadiliano, busara na kukataa kutumiwa na watu wasioitakia mema nchi.

Amehimiza wazee kuwa mstari wa mbele katika mazungumzo ya maridhiano, huku akiwasihi vijana kutokubali kujengewa chuki au kutumiwa kama nyenzo ya vurugu. Amesema ujenzi wa nchi hauwezi kufanywa na watu wa nje bali na Watanzania wenyewe.

Katika hitimisho lake, Rais Samia alisisitiza kuwa serikali itaendelea kulinda amani bila kuyumba, na kwamba Tanzania itaendelea kusimama ikiwa wananchi watashirikiana, kuzungumza, na kutibu majeraha ya kisiasa yanayotishia mshikamano wa taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *