Akizungumza na waandishi habari Jumatatu, Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House, Karoline Leavitt amesema Rais Trump atakutana na marais hao siku ya Alhamisi katika mkutano unaotarajiwa kukamilisha utiaji wa saini makubaliano yaliyofikiwa mwezi Juni na kusainiwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Rwanda na Kongo, na mfumo wa kiuchumi uliokubaliwa mwezi Novemba.

”Siku ya Alhamisi, Rais Trump atakutana na marais wa Jamhuri ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kwa ajili ya kusaini makubaliano ya kihistoria ya amani na kiuchumi ambayo ameyasimamia,” alifafanua Leavitt.

Mapigano yameendelea

Mwezi Juni, Rais Trump alikutana katika Ikulu ya White House na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili, wakati ambapo walisaini makubaliano ya awali, na tangu wakati huo, amekuwa akijigamba kwamba Kongo ni mojawapo ya nchi kadhaa ambako amevimaliza vita vyake.

Lakini mapigano yamekuwa yakiendelea, huku pande zote mbili zikitupiana lawama. Ghasia ziliongezeka mwezi Januari wakati ambapo kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda lilipoyateka maeneo kadhaa ya Kongo, ikiwemo miji ya Goma na Bukavu.

Tina Salama, Msemaji wa Rais Felix Tshisekedi amethibitisha kuwa kiongozi huyo wa Kongo atasafiri kuelekea Washington kwa lengo la ”kusaini makubaliano ya amani na Rwanda.” Kulingana na Salama, pia kutakuwa na makubaliano kuhusu ujumuishaji wa kikanda ambao Rais Tshisekedi amekuwa akiutaka tangu alipoingia madarakani.

Rumangabo, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo 2023 | Waasi wa M23
Waasi wa M23 walioko mashariki mwa KongoPicha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Amebainisha kuwa hata hivyo, heshima kwa makubaliano hayo ina maana ya heshima kwa uhuru wa Kongo, kuondolewa kwa vikosi vya Rwanda kutoka kwenye maeneo ya Kongo, na kuwepo tena kwa imani kwa pande zote.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, amelithibitishia Shirika la Habari la Ufaransa, AFP kwamba Rais Kagame atasafiri kwenda Washington, lakini akakataa kutoa taarifa zaidi. Wiki iliyopita, Rais Kagame aliishutumu hadharani serikali ya Kongo kwa kuchelewesha kusainiwa kwa makubaliano ya amani.

Aina ya makubaliano yatakayosainiwa

Haikufahamika wazi mara moja jinsi makubaliano ya ngazi ya urais yatakavyokuwa tofauti na makubaliano ya mwezi Juni. Katika mazungumzo ya mwezi uliopita wa Novemba mjini Washington, Rwanda na Kongo zilikiri na kutambua kusuasua katika utekelezaji wa makubaliano ya Juni, lakini zilikubaliana kufanya kazi kwa pamoja ya kupunguza mvutano.

Eneo la mashariki mwa Kongo lenye utajiri wa madini muhimu kwa ajili ya kutengenezea vifaa vya kiteknolojia, limekumbwa na vita kwa miongo mitatu, ambavyo vimeyagharimu maisha ya maelfu ya watu. Rais Trump ameonyesha matumaini ya kupata madini kutoka mashariki mwa Kongo, na kuipa Marekani nguvu zaidi dhidi ya China.

(AFP, Reuters)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *