
Viongozi wa Afrika waliokutana Algiers siku ya Jumapili walitoa wito wa kutambuliwa rasmi uhalifu uliofanyika enzi za ukoloni barani Afrika, ufanywe kuwa ni uhalifu na kulipwe fidia kupitia mchakato unaoungwa mkono na Umoja wa Afrika.
Hatua hiyo inakuja baada ya Azimio la AU lililopitishwa katika mkutano wa kilele mwezi Mei, ambao ulisisitiza kuarifishwa ukoloni kama uhalifu dhidi ya ubinadamu. Sheria ya sasa ya kimataifa haikatazi waziwazi ukoloni.
Washiriki wamemulika uharibifu mkubwa wa kiuchumi uliosababishwa na ukoloni barani Afrika huku mataifa makubwa ya Ulaya yakipora maliasili za bara hilo, kama vile dhahabu, almasi na mpira, na kuziacha jamii zikiwa maskini.
Gharama ya kiuchumi iliyosababishwa na ukoloni barani Afrika inaaminika kuwa ya kushangaza, huku baadhi ya makadirio yakionyesha kuwa gharama ya uporaji huo inafikia matrilioni ya dola.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Ahmed Attaf amesema, kuandaliwa mkutano huo nchini mwake ni ishara na nembo, kutokana na uzoefu mchungu wa Algeria chini ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa. Attaf ameongeza kuwa mfumo wa kisheria utahakikisha fidia hiyo haionekani kama “zawadi wala bakshshi.”
Karibu walowezi milioni moja wa Ulaya walikuwa na maslahi makubwa ya kisiasa na kiuchumi kuliko Waalgeria ingawa kisheria, Algeria ilikuwa sehemu ya Ufaransa.
Kama ilivyokuwa katika nchi nyingine za Afrika, mamia ya maelfu ya Waalgeria waliuawa katika vita vya uhuru vya nchi hiyo. Vikosi vya jeshi la Ufaransa viliwatesa na kuwapoteza watu, na kuharibu vijiji kama sehemu ya mkakati wa kukabiliana na uasi.
Mnamo 2017, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron aliitaja historia ya ukoloni wa Ufaransa kama uhalifu dhidi ya ubinadamu lakini hakuomba msamaha rasmi. Badala yake Macron aliwasihi Waalgeria waache kukariri dhuluma zilizofanywa na Wafaransa katika miaka ya huko nyuma.
Harakati za kutaka fidia za uhalifu uliofanywa na wazungu barani Afrika katika kipindi cha ukoloni zinahusishwa na hatua za mataifa ya Afrika za kuhakikisha kurejeshwa barani humo turathi zilizoporwa na kuwekwa majumba ya makumbusho ya Ulaya.