Dar es Salaam. Mwaka ndiyo huooo unakatika! Ngoma zinazidi kupikwa na kuachiwa na kufanya vizuri kwenye vyombo vya habari na mitandaoni. Wasanii wananufaika pakubwa na kazi hizo kwa kufanya shoo na kuuza nakala hadi mitandaoni, lakini unajua nyuma yake kuna nani?

Hawa ni maprodyuza ambao wanahakikisha mashairi ya wimbo wa msanii unasindikizwa na biti kali. Ndiyo wanaoumiza vichwa kuufanya wimbo uendane na mdundo na kuja kuzalisha ‘hit’.

Wapo maprodyuza (watayarishaji) ambao kazi zao zimewatangaza kwa kiasi kikubwa na kuwa maarufu na nyimbo walizozitengeneza zimevuka mipaka na kuwani tuzo kubwa duniani. Pia zimeleta shoo na kuwapa umaarufu kutokana na ubunifu wao.

Wakati tunakaribia kuuaga mwaka 2025, hawa hapa ni maprodyuza ambao ngoma walizozipika zimependwa sana na mashabiki na kufuatiliwa kwa kusikilizwa au kutazamwa na wengi.

MAPRO 01
  1. B Boy Beats

Amefanya kazi na wasanii kama Harmonize, Ibraah na wengineo na moja ya ngoma kali alizotengeneza ni ‘Me Too’ ya Abigail akimshirikisha Harmonize. Ngoma hii imefikisha watazamaji zaidi ya milioni 27 YouTube, ikiingia pia kwenye tuzo za muziki wa Grammy baada ya kufanya vizuri kwenye majukwaa ya muziki kama Apple Music, Audiomack na nyinginezo.

Utofauti wa biti wa ngoma hiyo na nyingine ndiyo ulioipa ubora kwani wasanii wengi wamekuwa wakitoa zinazofanana na kushindwa kujua ipi kali.

MAPRO 02

2. GeniusJini X66

Ana vipaji vingine vya kuimba na kuandika, lakini kwenye kutayarisha ngoma hashikiki.

Ngoma za Jay Melody akifanya naye pia kolabo katika ngoma tano ikiwemo Far Away, Juu, Sare Sare, Wewe na nyinginezo zimedhihirisha ubora wake.

Kati ya ngoma alizofanya tangu aanze kazi hiyo, mwaka huu ana mbili ambazo zimefanya vizuri zaidi ‘Sella’ ya Alikiba yenye watazamaji milioni mbili na inafanya vizuri zaidi Kenya na ‘Mimi na Wewe’ ya rapa Frida Amani akimshirikisha Jay Melody ambao unaongoza kwa kufanyiwa chalenji na mashabiki kwenye mtandao wa kijamii wa TikTok.

MAPRO 03

3. S2Kizzy

Jina lake ni Salmin Kassim Maengo ‘Zombie’. Ametengeneza ngoma kali ‘hit’ nyingi zaidi mwaka huu, zikiwamo mbili kali za Mbosso, Aviola na Pawa zilizopata umaarufu mkubwa, kutoka katika EP ya Room Number 3 na zimetazamwa na idadi kubwa ya watu YouTube.

Ngoma nyingine zilizopita mikononi mwake zikafanya vizuri ni Sweety ya Nandy aliyomshirikisha Jux na mwezi mmoja tu imeangaliwa na watu zaidi ya milioni tatu YouTube.

Pia ametengeneza ngoma nne za Diamond zilizotoka hivi karibuni ambazo ni Msumari, Nani, Sasampa, Katam ft Bien wa Kenya na Salama aliyoshirikishwa na mkali wa kuimba live, Barnaba Classic. 

MAPRO 04

4. Laizer Classic

Iraju Hamisi ‘Laizer’. Mara ya mwisho kutengeneze ngoma kali ni mwaka 2023 alipopika ‘Yatapita’ na ‘Zuwena’ zote za Diamond Platnumz.

Ndiye mtayarishaji wa nyimbo nyingi za Wasafi katika studio za Wasafi Record na alianza kazi hiyo mwaka 2014.

Hivi karibuni alitengeneza hit lakini kwa mara hii ilikuwa ya msanii Zuchu akimshirikisha Diamond ambaye ni kama amekuwa na kismati naye kila wanapofanya ngoma pamoja.

Tangu ngoma hiyo iachiwe imekuwa maarufu hasa wakati ule wa mashindano ya CHAN na Zuchu alikuwa msanii mkuu waliyepafomu Kenya. Ni kama jukwaa lile lilimuongezea watazamaji wapya kwani ndani ya miezi miwili ina zaidi ya watazamaji Milioni mbili ikiwa audio pekee.

MAPRO 05

5. Mixing Killer, Cukie Dady

Ngoma ya Lala ya  Harmonize na Abigail imetengenezwa na watayarishaji wawili, Cukie Dady na ilimiksiwa na Mixing Killer. Ngoma ni ya Konde Boy na hadi sasa wawili hao wametengeneza zaidi ya kolabo tano na zote zimefanya vizuri kwenye mitandao ya kijamii ikiwa na zaidi ya watazamaji milioni nne na majukwaa ya kusikilizia muziki.

Wimbo huo pia ulikuwa miongoni mwa ngoma nne za Harmonize zilizoingia kwenye mchujo wa tuzo za Grammy zinazotarajiwa kufanyika mwakani, ingawa nayo haikupita.

Wengine ni Kaniba Creator aliyetengeneza ngoma ya Mvua ya Marioo, Chibby aliyezalisha Jirani ya Jaymelody, Pablo aliyefanya ngoma ya Afande ya Dogo Paten na Zuchu kuwa maarufu nchini. Nyimbo zingine ni Dunia ya Marioo iliyotengenezwa na BLVCQ, Pole ya Yammi kutoka kwenye EP yake ya After All ikipikwa na Ma Feeling.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *