Makadirio haya mapya yanaweka idadi ya waliyoathirika duniani kote kuwa watu milioni 50 huku wanawake na watoto wakiendelea kuwa wenye hatari kubwa zaidi.

Utumwa wa kisasa ni doa kwa dhamira ya binadamu na ni shambulio la moja kwa moja kwa utu wa binadamu,” amesema msemaji wa ILO akiongeza kuwa “Utumwa huo unatokea kila kanda, kila kundi la kipato, na katika sehemu nyingi za kazi.

Janga lililojificha peupe

Ingawa haujaelezwa kisheria, “utumwa wa kisasa” ni neno pana linalojumuisha kazi za kulazimisha, usafirishaji haramu wa binadamu, ndoa za shuruti, madeni ya lazima na unyonyaji mwingine ambao mtu hawezi kuepuka kutokana na vitisho, vurugu, udanganyifu au ukandamizaji wa udhaifu.
ILO inasisitiza kuwa tatizo hili lipo karibu kila nchi, likivuka tamaduni, dini na madhehebu ya jamii.

Kwa mujibu wa shirika hilo la kazi Zaidi ya nusu ya kazi zote za kulazimishwa sawa na asilimia 52 na robo ya ndoa za kulazimishwa zinatokea katika nchi zenye kipato cha kati na cha juu.

Faida kutokana na kazi za shuruti ilifikia dola bilioni 236

Kwenye ripoti yake mpya ya “Faida na Umasikini” au Profits and Poverty, ILO inaonya kuwa kazi za shuruti zimekuwa biashara yenye faida kubwa duniani zikizalisha dola bilioni 236 kila mwaka pesa zinazoibiwa kwa wafanyakazi ambao hawawezi hata kulipa mahitaji yao ya msingi”.

Mtaalamu wa ILO amesema “Huu ni unyonyaji kwa kiwango cha viwanda, ukitajirisha mitandao ya uhalifu huku ukisukuma familia kuwa maskini zaidi. Serikali pia zinapoteza mapato muhimu ya kodi, kudhoofisha hifadhi za kijamii na utawala wa sheria.”

Kwa mujibu wa ILO wafanyakazi wa kigeni wanateseka zaidi, kwani fedha zao zilizopotea zinamaanisha wanatuma kidogo nyumbani kwa familia zao.

Hakuna kanda iliyosalimika

ILO ilirekodi watu milioni 27.6 katika kazi za shuruti mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko la watu milioni 2.7 kutoka 2016.
Asia na Pasifiki zinashikilia idadi kubwa zaidi, watu milioni 15.1, zikifuatiwa na:

  • Ulaya na Asia Kati  watu milioni 4.1
  • Afrika watu milioni 3.8
  • Amerika watu milioni 3.6
  • Nchi za Kiarabu  watu milioni 0.9

Kwa mujibu wa uwiano, Nchi za Kiarabu zinaongoza kwa waathirika 5.3 kwa kila watu 1,000.

Kiasi cha asilimia 86 ya kazi zote za kulazimisha kinasababishwa na wajanja binafsi, wakiwemo:

  • Asilimia 63 kwa ukandamizaji wa kazi
  • Asilimia 23 kwa unyonyaji wa kingono

Kazi za kulazimisha zinazotolewa na serikali zinachangia asilimia 14 pekee.

Sekta zilizoathirika zaidi ni viwanda, huduma, kilimo na kazi za majumbani ambazo zinawakilisha asilimia 89 ya kesi zote.

Watoto wanaendelea kuathirika

Duniani mtoto mmoja kati ya watoto kumi hufanya kazi, wengi wakikumbwa na unyonyaji wa kiuchumi.
Ajira kwa watoto inawaibia watoto mustakabali wao. Ni ukiukaji wa haki, si fursa, ILO inasema, ikisisitiza ahadi za chini ya Mkataba wa Haki za Mtoto.

Usafirishaji haramu wa binadamu nao bado ni moja ya njia mbaya zaidi za utumwa
Chini ya Itifaki ya Umoja wa Mataifa, kuajiri, kusafirisha au kukaribisha watu kwa ajili ya unyonyaji ni jinai na watoto wanachukuliwa kuwa wahanga hata bila kuthibitisha kulazimishwa.

Msemaji wa ILO ameongeza kuwa Usafirishaji haramu unaharibu jamii kimsingi. Unalenga wanyonge, unakuza uchumi wa uhalifu na unaharibu maisha”.

Wito wa hatua za haraka

Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Utumwa inaadhimisha kupitishwa kwa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa 1949 wa kupinga usafirishaji wa binadamu na unyonyaji. Lakini ILO inasema kuwa mgogoro wa leo unahitaji ahadi mpya ya kimataifa.

Itifaki yake ya kisheria inayolazimisha kuhusu Kazi za shuruti, iliyokuwa ikitumikia tangu 2016, imekusudiwa kuimarisha juhudi za kimataifa lakini mapengo ya utekelezaji bado yapo.

Tunajua kinachofanya kazi, ulinzi madhubuti, ajira za haki, kuwajibisha wachukuaji na kusaidia waliyoathirika. Sasa tunachohitaji ni utashi wa kisiasa, ILO imesisitiza.

“Utumwa wa kisasa hauwezi kuepukika. Ni chaguo ambalo jamii zinachagua na lazima tuukatae mara moja.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *