“Mgogoro huu unazidi kuzorota kwa kasi ya kutisha,” amesema Mwakilishi wa UNHCR nchini Msumbiji, Xavier Creach. “Ghasia zinasambaa, familia zinakimbia kwa hofu, na uwezo wetu wa kukidhi mahitaji hauendani tena na kiwango cha mahitaji kilichopo.”

Tulitoroka gizani walipokuwa wakiteketeza kila kitu

Watu walioweza kuingia maeneo salama wamesimulia mashambulizi ya usiku dhidi ya vijiji vyao, ambapo makundi yenye silaha yalichoma nyumba na kuwashambulia raia.

“Wametueleza jinsi walivyokimbilia usalama katika giza totoro wakati watu wenye silaha walipovamia vijiji vyao,” amesema Creach. “Wengi walikimbia bila chochote. Wazazi walipoteza watoto katika hali ya taharuki. Wazee wengi walibaki nyuma kutokana na mkanganyiko. Kwa baadhi yao, hii ni mara ya pili au ya tatu wanalazimika kukimbia mwaka huu.”

Mgogoro huu, ulioanza Cabo Delgado mwaka 2017, tayari umewafurusha watu zaidi ya milioni 1.3.

Lakini UNHCR inasema mwaka 2025 umeshuhudia mabadiliko ya hatari, huku mashambulizi yakitokea kwa wakati mmoja na kuenea hadi jimbo la Nampula eneo ambalo hapo awali lilikuwa kimbilio kwa maelfu ya wanaokimbia ghasia.

Mama na wavulana watatu wakiwa wamejihifadhi darasani baada ya kukimbia vurugu kaskazini mwa Msumbiji.

© UNHCR/Isadora Zoni

Mama na wavulana watatu wakiwa wamejihifadhi darasani baada ya kukimbia vurugu kaskazini mwa Msumbiji.

Raia wakimbilia kwenye shule na maeneo ya wazi

Kwa kukosa taarifa za mapema, familia zinafikia katika makazi ya muda Nampula yakiwemo shule, makanisa na maeneo ya wazi bila nyaraka, bila mahitaji ya msingi na bila usaidizi.

Creach amesema “Watu wanakimbia wakiwa wamebanwa na hofu kali, wakitembea kwa siku kadhaa bila chakula, maji au ulinzi. Wanawake na wasichana kwa namna ya pekee wako katika hatari kubwa ya manyanyaso na ukatili.”

Wimbi hili la ufurushwaji linakuja wakati dunia ikiadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, ukikumbusha wa jinsi mizozo inavyoongeza hatari kwa wanawake na wasichana.

Licha ya uhaba mkubwa wa rasilimali, timu za ulinzi zimeimarisha mifumo ya kuripoti kwa usiri na huduma kwa manusura wa ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, mahitaji yanaendelea kuongezeka zaidi ya uwezo uliopo.

Watoto wanawasili wakiwa hoi na peke yao

Timu za misaada ya kibinadamu zinaripoti kuwa watoto wengi wanafika wakiwa wamechoka kupindukia, wamedhoofika, wakiwa na kiwewe na miguu iliyovimba baada ya kutembea kwa siku kadhaa.

Wengine wamewasili bila ndugu, baada ya kutengana na familia zao wakati wa hofu.

“Watoto hawa wanatufikia wakiwa na hofu na wakikabiliwa na hali ya kutokuwa na mtu wa kuwaangalia. Wanahitaji ulinzi, ufuatiliaji wa familia na msaada wa haraka wa kisaikolojia.”amesema afisa huyo wa UNHCR

Vituo vya usaidizi vimeanzishwa ili kutoa ushauri nasaha, kugawa vifaa vya kujistiri, kusaidia watu wenye ulemavu na kusaidia familia kupata upya nyaraka zao za utambulisho kwa kushirikiana na mamlaka za eneo.

Jamii zinazowapokea zimezidiwa uwezo

Wimbi hili la ghafla la wakimbizi wa ndani linaweka mzigo mkubwa kwa jamii zinazowapokea ambazo nazo pia zinakabiliwa na changamoto za kiusalama.

Maeneo ya malazi ya muda yakiwa yamefurika kupita kiasi yanazalisha hatari mpya.

“Wanawake na wasichana wanalala nje bila mwanga wala faragha. Wazee na watu wenye ulemavu wako katika maeneo yasiyo rafiki kwao,” ameonya Creach..

Utoaji misaada umefika ukingoni

UNHCR inasema operesheni ya kibinadamu kaskazini mwa Msumbiji iko karibu kuzidiwa uwezo.

“Kwa kuongezeka kwa wahamiaji kila siku na ufadhili kukaribia kuisha, huduma muhimu  kuanzia ulinzi hadi maji, chakula na malazi zimefikia kiwango cha hatari,” kwa mujibu wa Creach.

Kwa jumla, mashirika ya kibinadamu, mashirika ya Umoja wa Mataifa, NGOs, taasisi za serikali, sekta binafsi na jamii zenyewe “hawawezi kuendelea bila msaada wa haraka zaidi.”

Mtoto ambaye familia yake ilikimbia ghasia kaskazini mwa Msumbiji amepumzika kwenye eneo la watu waliokimbia makazi yao.

© UNHCR/Isadora Zoni

Mtoto ambaye familia yake ilikimbia ghasia kaskazini mwa Msumbiji amepumzika kwenye eneo la watu waliokimbia makazi yao.

UNHCR yaomba msaada wa dharura jumuiya ya kimataifa

UNHCR inatoa wito wa ufadhili wa haraka ili kuimarisha jitihada za kukabiliana na mgogoro, kusaidia jamii zinazowapokea wakimbizi na kuzuia hali isiwe mbaya zaidi.

“Wakati mahitaji yakiwa katika kiwango cha juu zaidi, sisi tunaishiwa rasilimali,” amesema Creach. “Ikiwa msaada hautapatikana sasa, hali itadorora kwa kasi.”

Shirika hilo linahitaji dola milioni 38.2 mwaka 2026 ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kaskazini mwa Msumbiji. Lakini ufadhili wa 2025 umesimama kwenye asilimia 50 tu ya dola milioni 42.7 zinazohitajika.

Creach ameonya kuwa “Bila ufadhili wa ziada, maelfu ya familia zitabaki katika hali ya sintofahamu”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *