
Dkt. Rajesh Pandav, Mwakilishi mteule wa WHO nchini Sri Lanka amesema “Fedha hizi zitatumika kwa ajili ya timu za hatua za haraka ili kusaidia huduma muhimu za afya kwa jamii zilizoathirika, na pia kuimarisha usimamizi wa taarifa za afya na ufuatiliaji, ambavyo ni muhimu kwa kugundua kwa wakati milipuko ya magonjwa na kuwezesha hatua zifaazo.”
Kimbunga Ditwah kilitua nchini Sri Lanka tarehe 28 Novemba na kusababisha mafuriko makubwa, maporomoko ya ardhi, na uharibifu mkubwa wa miundombinu kote nchini. Vifo kadhaa, watu wengi kukosa makazi, na kusitishwa kwa huduma muhimu na shughuli za maisha vimeripotiwa nchi nzima.
Ufadhili wa WHO, sehemu yake ikitoka katika Mfuko wa Dharura wa Afya wa Ukanda wa Asia ya Kusini-Mashariki (SEARHEF), unasaidia gharama za uendeshaji kwa ajili ya kuhamasisha na kupeleka timu za matibabu na afya ya umma za hatua za haraka ambazo zitatoa huduma za majeraha, msaada wa huduma ya kwanza, kuwaelekeza wagonjwa wanaohitaji matibabu hospitalini, na kuhudumia wanawake wajawazito, watoto, wazee na makundi mengine.
Timu hizi za hatua za haraka zitafanya ukaguzi wa dawa na vifaa tiba, na kutathmini mahitaji ya kitabibu, ubora wa maji, usafi ya mazingira, usalama wa chakula, na hatari za kiafya za kimazingira.
Tathimini ya mahitaji
Kama shirika kuu katika hatua za sekta ya afya, WHO inaunga mkono tathmini ya haraka ya mahitaji inayotekelezwa na mamlaka za kitaifa na washirika, ili kuongoza hatua zinazoongozwa na serikali.
“Tangu janga hili lilipoikumba nchi hii, timu za WHO zimekuwa zikifanya kazi kwa karibu na mamlaka za kitaifa na wadau wake ili kuhakikisha hatua zenye uratibu mzuri.Kuendelea kwa huduma muhimu, kuimarisha ufuatiliaji ili kugundua mapema milipuko yoyote ya magonjwa yanayoenezwa na mbu, na kuhamasisha rasilimali zote zinazowezekana, kunabaki kuwa kitovu cha hatua za WHO”, amesema Dkt. Pandav.
Sri Lanka imetangaza hali ya dharura kufuatia uharibifu uliosababishwa na kimbunga hicho kilichoathiri wilaya zote 25 nchini humo. Nchi imeomba msaada wa kibinadamu na wa awali wa uokoaji kutoka kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na taasisi za kimataifa ili kusaidia katika uokoaji wa haraka.
Sri Lanka pia imeomba msaada wa kimataifa wa sekta mbalimbali katika maeneo kama vile uhakika wa chakula, kujikimu, kilimo, lishe, elimu, maji, usafi, makazi, pamoja na hatua za uokoaji na urekebishaji wa awali.
“WHO inabaki kuwa tayari kikamilifu kuunga mkono hatua za kitaifa na kulinda afya na ustawi wa jamii zote zilizoathirika,” amesema Dkt. Pandav.
Mfuko wa Dharura wa Afya wa Ukanda wa Asia ya Kusini-Mashariki (SEARHEF) ni utaratibu wa kipekee wa ufadhili wa ukanda huu unaosaidia utekelezaji wa huduma za kuokoa maisha mara baada ya janga la kiafya kutokea.