Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) amewafutia mashtaka ya uhaini na uchochezi mfanyabiashara Jennifer Jovin, maarufu Niffer, na mwanaharakati Mika Chavala, waliokamatwa kabla na wakati wa vurugu za Oktoba 29 zilizoambatana na uchaguzi mkuu.

Hatua hii imekuja wakati tume ya uchunguzi wa mauaji katika vurugu hizo ikiendelea na kazi, huku kukiwa na wimbi la mitandaoni linalohamasisha maandamano mengine Desemba 9 mwaka huu.

Ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wamefurika katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu siku ya Jumatano walilipuka kwa vilio vya furaha pindi ilipotangazwa kuwa wawili hao maarufu wameachiwa huru baada ya kukabiliwa na mashitaka mazito ya uhaini.

Uamuzi huo umetolewa baada ya DPP kuwasilisha ombi mahakamani la kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi dhidi ya Niffer na Chavala. Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamua alikubaliana na ombi hilo la upande wa Jamhuri na kutangaza rasmi kuwaachia huru.

Tanzania Dar es Salaam 2024 | Jennifer Jovin, maarufu Niffer, baada ya kuachiwa kutoka gerezani
Niffer, mwenye Buyibuyi nyeusi, akiongozwa na askari baada ya kutoka katika chumba cha mahakama.Picha: Ericky Boniphace/DW

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka gerezani, Jennifer Jovin aliishukuru familia yake, mamlaka mbalimbali na Rais wa nchi, akisema bado anaendelea kuelewa kilichotokea lakini anafurahia kuachiwa kwake.

Wawili hao walikuwa wanakabiliwa na kesi namba 26388/2025 chini ya kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura ya 20, marejeo ya mwaka 2023, wakihusishwa na vurugu za maandamano ya Oktoba 29 na matukio ya kabla ya siku hiyo.

Wanasheria na wachambuzi wachambua ujumbe nyuma ya uamuzi wa DPP

Wakili wa utetezi Peter Kibatala amesema DPP ametumia madaraka yake ipasavyo na kwamba hatua hiyo imefungua ukurasa mpya, ingawa sheria haimlazimishi kueleza sababu za kufuta mashtaka hayo.

Wachambuzi wa masuala ya sheria wamesema uamuzi wa kuwafutia mashtaka unaonyesha mabadiliko katika namna mamlaka zinavyochukulia kesi za uhaini, hasa baada ya hotuba ya hivi karibuni ya Rais iliyoibua mjadala mpana kuhusu vigezo vya kukamata na kufungua mashitaka.

Tanzania Dar es Salaam 2024 | Jennifer Jovin, maarufu Niffer, baada ya kuachiwa kutoka gerezani
Niffer alikuwa anashtaka kwa kosa kubwa kabisaa la uhaini ambalo kisheria linabeba adhabu ya kifo.Picha: Ericky Boniphace/DW

Wakili Mathew Kakamba amesema uamuzi huo unadhihirisha kwamba baadhi ya watu walikamatwa bila kufuata vigezo sahihi, na amempongeza DPP kwa kutambua mapema udhaifu katika mashitaka yaliyowakabili watuhumiwa hao.

Ripoti zinaonyesha kuwa kati ya Novemba 10 na 11, zaidi ya watu 600 walikamatwa nchini na kusomewa mashtaka ya uhaini katika mahakama mbalimbali kutokana na vurugu za maandamano ya Oktoba 29 na matukio yaliyojitokeza kabla ya siku hiyo.

Huku kesi hizo zikiendelea, kuachiwa kwa Niffer na Chavala kunatajwa kama hatua muhimu inayoweza kuathiri mwenendo wa mashtaka mengine na kujenga mjadala mpya kuhusu matumizi ya sheria za uhaini nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *