Niger imeanza kuuza urani yake katika soko la kimataifa baada ya kukata mkono wa Ufaransa katika sekta ya madini hayo nchini humo.

Rais wa mpito wa Niger, Abdourahamane Tchiani, ametangaza kwamba nchi hiyo itauza urani inayozalishwa na kampuni iliyotaifishwa ya Soumir kwenye soko la dunia katika utekelezaji kamili wa mamlaka yake ya kitaifa. Hatua hiyo inachukuliwa baada ya serikali ya Niger kutaifisha kampuni hiyo mwezi Juni mwaka huu.

Abdourahamane Tchiani

Hapo awali, 90% ya hisa za mgodi wa uraniamu wa Somair zilikuwa zikimilikiwa na kampuni ya Ufaransa ya Orano. Kampuni hiyo ya Ufaransa, ambayo iliendesha na kufaidika na migodi ya urani nchini Niger kwa miongo kadhaa, imekiri kwamba imepoteza udhibiti wa uendeshaji wa migodi mitatu mikuu ya urani nchini Niger. Mgodi wa  Imouraren wa Niger unatambuliwa kuwa mojawapo ya akiba kubwa zaidi ya urani duniani, ukiwa na takriban tani 1,300 za urani zenye thamani ya takriban euro milioni 250, na sasa Niger imetangaza kwamba itaweka akiba ya mgodi huo kwenye masoko ya kimataifa.

Hatua hii ya Niger si tu kwamba ni uamuzi wa kiuchumi wa kusimamia vyema rasilimali za nchi, lakini pia ni ishara nyingine ya mwisho wa utawala wa kikoloni wa Ufaransa katika nchi hiyo. Katika miaka ya hivi karibuni, Niger, Burkina Faso, Mali na baadhi ya nchi zingine za Afrika zimechukua mbinu tofauti na ilivyokuwa hapo awali, zikipinga uwepo wa kikoloni wa Ufaransa katika sekta za kijeshi, kiuchumi na kisiasa za nchi hizo na kufukuza vikosi vya majeshi ya Ufaransa katika ardhi zao. Kwa kadiri kwamba, kambi nyingi za kijeshi za Ufaransa katika nchi za Afrika zimefungwa, na makampuni mengi ya Ufaransa yamepigwa marufuku kuwepo katika sekta za kiuchumi za nchi hizi, hasa madini. Kwa hivyo, tangazo la kutaifishwa migodi ya urani nchini Niger, ambalo linaonyesha kukomeshwa kivitendo utegemezi kwa mataifa ya kigeni, linatambuliwa kuwa mabadiliko ya msingi katika uhusiano wa kimataifa na wa ndani wa Niger na nchi zingine.

Hatua hii inapata umuhimu zaidi ikizingatiwa kwamba Ufaransa imekuwepo katika nchi za Afrika, ikiwa ni pamoja na Niger, kwa miongo kadhaa kwa visingizio mbalimbali, na migodi na viwanda vingi vikubwa katika nchi hizo vimekuwa mikononi mwa wawekezaji wa Ufaransa. Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa, sehemu kubwa ya fueli ya mitambo ya nyuklia ya Ufaransa inatokana na urani inayotolewa katika nchi za Afrika kwa bei nafuu sana. Huu unatambuliwa kuwa uhusiano usio na usawa ambao, sambamba na utegemezi wa kisiasa na kijeshi wa nchi hizo kwa Ufaransa, ulisababisha pigo kubwa kwa uhuru na kujitawala halisi bara la Afrika.

Sasa, kutaifishwa mgodi wa urani wa Somair nchini Niger kunaashiria waziwazi hatua ya mabadiliko katika mchakato wa kukomesha kabisa ukoloni katika nchi za Afrika, hasa Niger. Ingawa nchi za Afrika zilipata uhuru wao wa kisiasa kutoka kwa madola ya kikoloni katika nusu ya pili ya karne ya 20, lakini sasa tunashuhudia juhudi za nchi hizo za kupata uhuru wa kiuchumi na kijeshi. Kutaifisha maliasili, hasa rasilimali za kimkakati kama vile urani, ni sehemu muhimu ya mchakato huu.

Inaonekana kwamba, hatua hii ya Niger si tu kwamba inaashiria mwisho wa utawala wa Ufaransa juu ya rasilimali za nchi hiyo, bali pia mwanzo wa enzi mpya ya kujikomboa kiuchumi na kujitawala katika bara la Afrika. Badala ya kutegemea madola ya kigeni, Niger sasa inaweza kuimarisha uchumi wake wa ndani kwa kutumia rasilimali za urani, na kutumia rasilimali hizo kuendeleza miundombinu, kutengeneza ajira, na kuboresha hali ya maisha ya watu wake. Zaidi ni kwamba, Niger itaweza kufunga mikataba ya biashara na nchi zingine, ambayo inaweza kubadilisha pakubwa uhusiano wa kiuchumi na jiografia ya kisiasa ya nchi hiyo.

Pamoja na hayo inatupasa kukumbusha hapa kuwa, mchakato wa kutaifisha maliasili za nchi utakabiliwa na changamoto nyingi. Ili sera hii ifanikiwe, Niger itahitaji mageuzi ya msingi katika miundo yake ya usimamizi na utawala. Uwazi katika michakato ya utaifishaji, kuzuia rushwa na ugavi sahihi wa rasilimali vinaweza kuiweka nchi hiyo kwenye njia sahihi ya maendeleo endelevu. Kama njia hii itafuatwa ipasavyo, Niger inaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine za Kiafrika kuelekea kwenye uhuru na kujitawala kiuchumi na kisiasa.

Hatimaye, kutaifishwa mgodi wa urani wa Somair nchini Niger si tu kwamba ni hatua muhimu kuelekea kwenye uhuru na kujitawala kiuchumi, lakini pia kunaweza kuonekana kama hatua muhimu ya kuelekea kwenye maendeleo makubwa barani Afrika. Afrika haitaki tena kuwa muuzaji tu wa malighafi kwa nchi za Magharibi; inataka kuarifisha upya uhusiano wake na mataifa yenye nguvu duniani ili iweze kutumia rasilimali zake katika njia ya maendeleo na ustawi. Mabadiliko haya yanaweza kubadilisha mustakabali wa bara la Afrika na kupandisha juu nafasi yake katika mfumo wa kimataifa.

Ufaransa inakabiliwa na wimbi jipya la kung’oa mizizi ya ukoloni barani Afrika

Wachambuzi wengi wameutaja mchakato huu kuwa ni nembo ya wimbi la pili la kung’oa mizizi ya ukoloni katika bara la Afrika. Taasisi ya Siasa za Kimataifa ya Austria imeandika katika uchambuzi kwamba hatua zilizochukuliwa na nchi za Kati na Magharibi mwa Afrika ni sehemu ya mchakato mpana wa kujitawala na msisitizo juu ya mamlaka ya kitaifa, ambao unaweza kutambuliwa kama wimbi la pili la kung’oa ukoloni barani Afrika.

Naam, kutaifishwa sekta ya urani nchini Niger si hatua ya kiuchumi tu; bali kwa hakika ni tangazo la kumalizika kipindi cha kihistoria cha utegemezi kwa madola ya kikoloni na mwanzo wa ukurasa mpya wa kujitawala halisi wa bara la Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *