
Timu ya mashirika ya msaada ya Umoja wa Mataifa iliyoko nchini Msumbiji imesema, raia wameuwawa kwa kukatwa vichwa na takriban 100,000 wamekimbia eneo la kaskazini mwa Msumbiji linalokabiliwa na machafuko.
UN yaeleza wasiwasi kuhusu machafuko Kaskazini mwa Msumbiji
Timu hiyo ilitowa taarifa ya tahadhari jana Jumanne kufuatia mgogoro mkubwa unaoendelea wa watu walioachwa bila makaazi, uliosababishwa na mashambulizi yaliyoongezeka dhidi ya jamii za maeneo hayo.
Afisa wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa mataifa UNHCR- Xavier Creach ambaye yuko katika mkoa wa Nampula amesema mamia ya watu wamekimbia machafuko ndani ya siku mbili.
”Niko Erati Kaskazini mwa Msumbiji ambako takriban watu 100,000 walioachwa bila makaazi wamewasili. Wanatokea wilaya jirani ya Memba. Wilaya hiyo imeshuhudia mashambulio katika kipindi cha siku na wiki kadhaa, yakifanywa na kundi la wanamgambo ambao wameshambulia raia, kuchoma nyumba na wakati mwingine kuchoma moto kijiji kizima,raia wameuliwa na wengine hata kukatwa vichwa”
Shirika hilo la UNHCR lina wasiwasi na mashambulio ambayo yanashuhudiwa mfululizo hivi sasa na kusambaa nje ya mkoa wa Cabo Delgado na kufika hadi Nampula.