Serikali ya Marekani imesitisha mara moja maombi yote ya uhamiaji kwa raia wa mataifa 19, hatua ambayo inaashiria kuimarishwa kwa sera kali za udhibiti wa wahamiaji baada ya tukio la kushambuliwa kwa wanajeshi wa kikosi cha National Guard wiki iliyopita.
Kulingana na waraka rasmi wa Idara ya Uraia na Uhamiaji (USCIS), uamuzi huo unahusu maombi ya uraia, kadi za kijani na faida nyingine za uhamiaji kwa watu wanaotoka katika mataifa yaliyoorodheshwa kama yenye hatari kubwa ya usalama.
Hatua hiyo imewakumba raia kutoka Afghanistan, Yemen, Haiti, Somalia, Sudan, Iran, Libya, Myanmar, Chad, Cuba, Venezuela, Turkmenistan, Eritrea, Burundi na mataifa mengine yaliyo kwenye orodha iliyoanzishwa Juni mwaka huu.
Waraka huo unasema watahiniwa kutoka mataifa hayo watawekwa chini ya uchunguzi mkali, ikiwa ni pamoja na kupitia upya maombi yao, kuhojiwa upya, na inapohitajika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria au uhamiaji.
Marekani imeeleza kuwa tukio la kushambuliwa kwa wanajeshi wa kikosi cha National Guard na mtuhumiwa raia wa Afghanistan limeonesha “udhaifu wa taratibu za uchunguzi”, na hivyo kuhitaji usimamizi mkali zaidi.
Shambulio la Washington lachochea msimamo mkali
Taarifa za maafisa wakuu wa serikali zinaonyesha kuwa usimamizi wa uhamiaji utabana zaidi, hali ambayo inafuatia msimamo wa Rais Donald Trump wa kuzuia wahamiaji wanaoonekana kuwa tishio kwa usalama wa taifa.
Trump alitangaza mara tu baada ya tukio hilo kwamba anapanga “kusimamisha kabisa uhamiaji kutoka mataifa yote ya Dunia ya Tatu” hadi mifumo ya Marekani itakapodhibitiwa upya.
Aidha, Waziri wa Usalama wa Ndani alitoa wito wa kupanua orodha ya mataifa yanayokabiliwa na vikwazo vya usafiri, akitoa lugha kali kuhusu wahamiaji wanaoingia nchini humo kwa wingi.
Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti mpango wa operesheni kubwa ya kuwakamata wahamiaji Minnesota, hususan jamii ya Wasomali, hatua ambayo viongozi wa eneo hilo wameikosoa vikali, wakisema hawatatoa ushirikiano.
Tangu shambulio hilo, serikali imetangaza msururu wa hatua mpya, ikiwa ni pamoja na kusimamisha maamuzi ya hifadhi na kutathmini upya maombi ya wakimbizi waliowasili chini ya utawala wa Biden.
Maombi, faida na vibali vya uhamiaji vyatiwa shime katika ukaguzi mpana wa usalama
Pamoja na kusimamisha maombi mapya, USCIS imetangaza kuwa ndani ya siku 90 itaunda orodha ya watu wanaostahili kupitiwa upya, ikiwa ni pamoja na wale ambao tayari walikuwa wamepewa idhini za awali za uhamiaji.
Waraka huo unaeleza kuwa hatua hii inakusudia kuilinda Wamarekani kutokana na kile serikali imekiita “hatari zinazotokana na ukosefu wa uchunguzi wa kina” kwa wahamiaji waliokuwa wakiingia nchini katika miaka ya karibuni.
Serikali imesisitiza kuwa uchunguzi mpya ni muhimu hasa kwa wale waliowasili Marekani kuanzia Januari 20, 2021—tarehe ya kuapishwa kwa Rais Biden—kwa madai ya uwezekano wa pengo katika usimamizi wa usalama wakati huo.
Wakosoaji wa sera hizi mpya wanasema hatua hiyo ni adhabu ya pamoja dhidi ya wahamiaji wasiokuwa na hatia, wakiongeza kuwa inawafanya raia kutoka mataifa fulani kuonekana kama watuhumiwa bila sababu.
Hata hivyo, serikali ya Trump imesisitiza kwamba usalama wa taifa unahitaji hatua kali, na kwamba mabadiliko haya ni sehemu ya juhudi pana za kuilinda Marekani kutokana na vitisho vya ugaidi na uhalifu.
Chanzo: APE, RTRE, AFP