
Hivi karibuni mamlaka na vyombo vya habari vya Kizayuni vimekiri kupata kipigo kikali kutokana na vita vya Ghaza na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya makombora ya Iran na kwamba kukiri huko kunaonesha kwamba makombora ya Iran hayakuvuruga tu milingano ya usalama, bali pia yamesambaratisha mshipa wa kiuchumi wa soko la nyumba la Israel.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars; ripoti mpya zinaonesha kina kirefu cha mgogoro katika soko la nyumba la Israel; mgogoro ambao umekuja baada ya mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran huko Israel kusambaratisha vibaya majengo ya walowezi wa Kizayuni. Soko la nyumba la Israel liko chini ya mashinikizo ya wakati mmoja ya ongezeko la viwango vya juu vya riba, vyanzo vichache vya kifedha kwa wajenzi na kivuli kizito cha vipigo vya makombora ilivyopata Israel kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mambo hayo yamelisababishia soko la nyumba la Israel, moja ya midororo mikubwa zaidi kuwaki kutokea kwenye miaka ya hivi karibuni.
Takwimu zilizotolewa na kampuni tisa kubwa za ujenzi zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Tel Aviv zinaonesha kuwa, mauzo ya nyumba yamepungua kwa karibu robo tangu mwanzo wa mwaka huu na mashirika hayo yameripoti kuporomoka kwa asilimia 24 mauzo hayo ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana. Hayo yote ni ushahidi wa wazi wa kuporomoka soko la nyumba la utawala wa Kizayuni.
Vita vya Ghaza, kujitumbukiza kwenye vita na Iran, na kufanya mashambulizi katika maeneo mengine kama Lebanon, Syria na Yemen yote hayo yameusababishia hasara kubwa utawala wa Kizayuni na kwamba kuanguka ghafla miamala ya nyumba kumepiga kengele za harati kwa uchumi wa Israel.
Katika mahojiano na Globes, Ziv Ein Eli, mchambuzi wa soko la mali isiyohamishika katika taasisi ya IBI Investments, ametoa picha kubwa zaidi ya kushuka thamani kwenye soko la nyumba la Israel na kubainisha kuwa, mwaka 2024 ulikuwa moja ya miaka iliyovunja rekodi ya mauzo ya vyumba, lakini tangu mwanzo wa mwaka huu, Israel imekumbwa na matukio mazito hasi, ambayo yamebadilisha kabisa mwelekeo wa soko lake la nyumba.
Ingawa Ziv Ein Eli amekwepa kusema waziwazi kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya makombora ya Iran yameitia hasara isiyofidika kiurahisi sekta ya nyumba ya Israel, lakini wataalamu wengine wanasema kuwa, madhara makubwa yaliyotokana na mashambulizi ya makombora ya Iran huko Israel ni jambo lisilokanushika.