Akizungumza mwishoni mwa mkutano wa Baraza la Mawaziri siku ya Jumanne, Trump alisema anapotazama kinachoendelea katika jimbo la Minnesota, anawaona wasomali wakiiba, na akamuagiza waziri wake wa fedha Scott Bessent afuatilie na kuchunguza kinachoendelea.
Trump alisema, “Nasikia Wasomali, waliliibia jimbo hilo mabilioni ya dola…mabilioni. Kila mwaka mabilioni ya dola na hawachangii chochote. Fedha za ustawi wa jamii ni kama 88% ya bajeti jumla na hawachangii chochote. Sitaki waingie katika nchi yetu. Nchi yao si nzuri kwa sababu inanuka. Mtu angeweza kusema, ooh matamshi yangu kuhusu Wasomali si sahihi kisiasa. Mimi sijali. Siwataki katika nchi yetu, na tutaenda vibaya na kuelekea pabaya ikiwa tutaendelea kuingiza takataka nchini mwetu.”
Wiki iliyopita, Trump alisema wakimbizi ndio chanzo kikuu cha matatizo ya kijamii nchini Marekani na akatoa mfano wa Minnesota, akisema jimbo hilo lilikuwa limechukuliwa na “mamia ya maelfu ya wakimbizi kutoka Somalia.” Hapo awali, pia alitangaza mwisho wa mpango wa ulinzi wa Wasomali huko Minnesota, ambao takwimu za sasa zinaonyesha unawaathiri watu mia chache tu.
Trump amshambulia Ilhan Omar
Siku ya Jumanne, Trump alimlenga na kumshambulia kwa maneno makali Mbunge mwanamke wa chama cha Democratic mzaliwa wa Somalia, Ilhan Omar kutoka Minnesota, akimwita yeye na marafiki zake “takataka.” Trump pia alisema Wasomali si watu wanaofanya kazi, watu wasiofanya chochote ila kulalamika; na walikotoka, hawakuwa na chochote. Akataka warudi walikotoka na wakajenge nchi yao.
Matamshi hayo yalikuja wakati wa kesi maarufu ya ulaghai wa fedha za ustawi wa jamii huko Minnesota, ambapo wakazi kadhaa wa Kisomali wanadaiwa kudanganya na kuuhujumu mfumo wa jimbo hilo wa mamia ya mamilioni ya dola chini ya Gavana Tim Walz. Mbunge Ilhan Omar alisema katika mtandao wa X kwamba “upendo” wa Trump kwake ulikuwa “wa kutisha” na alitumai atapata “msaada anaouhitaji sana.
Vyombo vya habari vya Marekani vimekisia kuhusu misako ya idara ya Uhamiaji na Ushuru inayowalenga wahamiaji wa Kisomali katika miji ya Minneapolis na St Paul huko Minnesota. Gazeti la New York Times liliripoti kwamba operesheni hiyo inawalenga mamia ya Wasomali bila hati sahihi za makazi. Maafisa wa jimbo la Minnesota wamewatetea watu wa jamii ya Wasomali dhidi ya mashambulizi ya Trump.
Maafisa wa Minnesota wawatetea Wasomali
Meya wa mji wa Minneapolis, Jacob Frey alisema “Kuwalenga Wasomali kunamaanisha kwamba mchakato unaofaa utakiukwa na makosa yatafanywa. Na tuwe wazi kwamba hii inamaanisha kwamba raia wa Marekani watazuiliwa si kwa sababu nyingine yoyote ile isipokuwa ukweli kwamba wanaonekana kama Wasomali. Hiyo si sasa, na haitakuwa kamwe sababu halali.”
Minnesota ina zaidi ya watu 60,000 wenye asili ya Somalia, wengi wao wakiishi kihalali katika jimbo hilo, na kuifanya kuwa jamii kubwa zaidi ya Wasomali nchini Marekani.
Wakati huo huo, serikali ya Marekani imesimamisha maombi ya uhamiaji kwa raia kutoka mataifa 19 ikiwemo Afghanistan, Yemen na Haiti. Hayo ni kw amujibu wa hati rasmi iliyotolea jana Jumanne, ikiimarisha msako mkali wa taifa dhidi ya uhamiaji.
Mamlaka zilisitisha michakato ya ushughulikiaji wa kadi za kijani na uraia, kulingana na hati hiyo, kwa watu kutoka nchi ambazo tayari zinakabiliwa na vikwazo vya usafiri vilivyotangazwa mwezi Juni na Rais Donald Trump. Mataifa hayo 19 pia yanajumuisha Venezuela, Sudan na Somalia.